
Dar es Salaam. Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imesema Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imeondoa hitajio la visa kwa raia wa Tanzania wanaoingia DRC kuanzia Machi 20, 2025.
Taarifa kwa umma iliyotolewa na wizara hiyo leo Machi 22, 2025 imesema baada ya DRC kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Julai 2022, Septemba 2, 2023 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliondoa utaratibu wa malipo ya visa kwa raia wa DRC kwa matarajio ya nchi ya Taifa hilo pia kufuta utaratibu wa kutoza malipo ya visa kwa msingi wa kuungana mkono.
“Serikali ya Tanzania inaamini uamuzi huu wa Serikali ya DRC ni hatua nzuri katika kuimarisha mtangamano na utakuwa na manufaa, ikizingatiwa kuna mwingiliano mkubwa wa wananchi wa nchi hizi mbili katika masuala mbalimbali ya kijamii na kibiashara.
“Vilevile, kuondolewa kwa hitajio la visa kutachochea ukuaji wa uwekezaji, biashara na kupunguza gharama,” imesema taarifa hiyo ya wizara.
Wizara imesema hatua hiyo ni moja ya mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na ujirani mwema kwa vitendo.
“Ni ishara ya Tanzania kuzingatia miongozo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA)” imesema taarifa hiyo.