Watano wawekewa vipandikizi maalumu kwenye uume

Dodoma. Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) imeweka vipandikizi maalumu kwenye uume (Penile Implantation), kwa wanaume watano ili kukabiliana na changamoto za nguvu za kiume.

Huduma hiyo ilianzishwa Juni mwaka 2023, gharama yake ikiwa ni kati ya Sh6 milioni hadi Sh10 milioni, tofauti na nje ya nchi ambapo inatozwa hadi Sh50 milioni.

Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Profesa Abel Makubi ameyasema hayo leo Jumanne Machi 4,2025 wakati akizungumzia mafanikio ya miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita na mwelekeo wa hospitali hiyo.

“BMH imefanikiwa kuweka vipandkizi kwa wanaume watano ambao walikuwa changamoto za upungufu wa nguvu za kiume, ikiwa ni hospitali ya kwanza kutoa hii huduma hapa nchini.”

Amesema watu wote waliopatiwa huduma hiyo wanaendelea vizuri na hakuna aliyelalamika changamoto yoyote.

“Changamoto ninayoiona ni gharama za upatikanaji wa huduma. Tatizo ni kubwa na tafiti zetu zinaonyesha takriban asilimia 40 hadi 45 ya wanaume wana some point (wana dalili) ya matatizo hayo.”

“Tungetamani kuwafanyia wengi lakini shida inakuwa ni gharama kubwa na wananchi wengi wanashindwa kuzimudu,”amesema.

Hata hivyo, amesema Serikali inachofanya sasa ni kuona jinsi ya kupunguza gharama kwa kuhudumia vifaa na hivyo mgonjwa kugharamia kiasi kidogo cha fedha.

Amesema wengi wenye tatizo hilo ni vijana wenye umri wa kati ya miaka 20 hadi 45 na miongoni mwa sababu ni magonjwa ya kuambukizwa (infection) na magonjwa yasiyoambukizwa.

Gazeti hili liliwahi kumnukuu Dk Anna Sarra wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, akisema miongoni mwa maradhi yanayosababisha changamoto ya kupungua kwa nguvu za kiume ni kisukari, shinikizo la damu, uti wa mgongo na kuharibika kwa mishipa kutokana na upasuaji.

Jinsi vipandikizi vinavyowekwa, ufanyaji kazi wake

Huduma hiyo hutolewa kwa mgonjwa kuwekewa vipandikizi vya plastiki vinavyoitwa silicone kwenye uume, hivyo kuwa na uwezo wa kushiriki tendo la ndoa kama kawaida, ambapo husaidia misuli ya uume kuwa imara.

Vipandikizi hivyo ambavyo ni plastiki vinaingizwa kwenye misuli ya uume na vitaendelea kuwapo kwa maisha yote ya muhusika. Upasuaji hufanyika kwa muda wa saa moja na nusu.

Ambapo baada ya upasuaji huo, siku saba za awali zinakuwa za uponyaji na muhusika anatakiwa asubiri kwa mwezi mmoja ndipo aanze kushiriki tendo la ndoa.

Imeelezwa kuwa mwanaume anayewekewa vipandikizi hategemei mtu amvutie kihisia au agusweguswe ndipo uume usimame, hisia zake zinabaki palepale, kama atahitaji watoto awaweza kwa kuwa utoaji wa mbegu hauathiriki.

Mbali na hilo, Profesa Makubi amesema hospitali hiyo inakusudia kuanzisha huduma za matibabu ya mfumo wa fahamu bila upasuaji na kitengo cha kiharusi (Neurology and Stroke Unit).

Amesema vijana wengi wamekuwa wakipata changamoto ya kiharusi na kuwa kila baada ya siku tatu wamekuwa wakipokea mgonjwa wengi wakiwa vijana kati ya miaka 30 hadi 50.

“Hii ni kwa sababu ya matatizo ya kisukari na presha pamoja na mabadiliko ya mtindo wa maisha kwa hiyo ni bora kuwa na kitengo cha kiharusi kama wizara ya afya imekuwa ikipenda kulifanya hili,”amesema.

Aidha, Profesa Makubi amesema wataanzisha huduma kwa ajili ya wazee ambayo haipo hapa nchini.

“Hawa wazee wetu wakishafika miaka 65 hakuna madaktari wa kuwahudumia, wana matatizo yao ambayo ni very unique ( ya kipekee) kwa hiyo tunataka kubobea kutoa huduma hii kwa kuwajali wazee wetu,”amesema.

Kuhusu huduma ya upandikizaji mimba amesema ni sehemu ya huduma za kibingwa na kibobezi zinazotolewa katika hospitali hiyo.

Amesema wengi ni wenye umri wa miaka 35 hadi 50 ndio kundi kubwa ambalo linajitokeza kuhitaji huduma ya upandikizaji wa mimba.

Amesema mwelekeo wa hospitali hiyo mbali na mambo mengi ni kuipandisha hadhi kufikia kiwango cha hospitali ya Taifa, kuimarisha mifumo ya Tehama katika kuboresha huduma ikiwepo matumizi ya akili mnemba (AI)  katika huduma za kusaidia wauguzi, upasuaji wa kutumia roboti (robotic surgeries) na upasuaji wa matundu.