Kahama. Watu watano wakiwemo watatu wa familia moja wamefariki dunia baada ya kuzama kwenye dimbwi la maji lililopo jirani na makazi yao katika Kata na kijiji cha Bulige Halmashauri ya Msalala Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga.
Akithibitisha tukio hilo leo Jumanne Februari 18, 2025, Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wilayani Kahama, Stanley Luhwago amewataja waliofariki dunia ni Zawadi Nkwambi (13), Khadija Nkwambi (11), Rahel Peter(11), Samike Peter (1) pamoja na mama mzazi wa Samike, Hoja Kubo (29) aliyefariki wakati akijaribu kuwaokoa wanaye wawili.
Mama aliyepoteza watoto wake wawili katika tukio hilo, Prisca Luchagula amesema lilitokea Februari 15, 2025 saa 10 jioni, watoto wawili kati yao walipoanza kuogelea baada ya kutoka shambani.
Amesema wakati wakiendelea kuogelea, maji yaliwazidi nguvu na kuzama hali iliyosababisha mama aliyekuwa jirani kutumbukia kwa lengo la kuwaokoa watoto hao ndipo naye akazama na watoto wake wawili waliokuwa pembeni nao wakaingia kutaka kumwokoa mama yao nao pia wakazama na kufariki.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Bulige, Allen Mahanga amesema dimbwi hilo ni miongoni mwa mashimo yaliyokuwa yakitumiwa na wanakijiji kuchimba madini ya ujenzi, kwa ajili ya ujenzi wa makazi yao.

Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita akitoa pole kwa familia zilizofikwa na watu watano wakiwemo watatu wa familia moja waliozama kwenye dimbwi la maji katika shimo lililokuwa likitumiwa kuchimba madini ya ujenzi kijiji na kata ya Bulige, Halmashauri ya Msalala. Picha na Amina Mwambo
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Bulige, Emmanuel Mhina amesema bwawa hilo lilikuwa sehemu iliyojificha na hivyo ilikuwa ngumu wao kuliona na kuliwekea uzio kama yalivyo mengine na wamegundua wananchi walilitumia kufua na kuoga hali iliyowafanya watoto kuingia na kuogelea.
Akitoa pole kwa familia hizo, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita amewataka viongozi wa vijiji na vitongoji wilayani humo kuhakikisha wanayambua maeneo yote yenye madimbwi au mabwawa ya maji ili yalindwe kwa kuwekewa uzio, mlango wa kuingia na kutokea ili kuzuia maafa zaidi yasiendelee kutokea.
Mhita amewataka Tarura na Tanroads, kuwasimamia makandarasi wanaotekeleza miradi hususani ya barabara wilayani humo kuhakikisha wanatengeneza mazingira salama wanapomaliza shughuli zao ili kuzuia maafa kama hayo.
“Jukumu la kutengeneza uzio katika maeneo wabebe, wasichimbe wakaacha wazi, kwa hiyo tutaongea na Tanroads na Tarura, kwa makandarasi wote ambao wanafanya ujenzi wa barabara kwenye maeneo kuhakikisha maeneo yote ambayo wao wamechimba waweke uzio,” amesema Mhita.