Watano kortini wakidaiwa kumuua dereva bodaboda Geita

Geita. Watu watano wamefikishwa katika Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Geita, wakikabiliwa na shitaka la mauaji ya kukusudia ya dereva bodaboda, Aloyce Deus (36), na kupora pikipiki yake.

Washtakiwa hao ni Shukuru Yohana (34), Kulwa Deus (34), Nonga Adam (29), Cosmas Charles (29) na Shukrani Jumapili (30). Wanadaiwa kutenda kosa hilo kinyume na Kifungu cha 196 na 197 cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, iliyorejelewa mwaka 2022.

Mwendesha mashitaka wa Serikali, Deodatha Doto, ameieleza Mahakama kuwa tukio hilo lilitokea Julai 12, 2024, katika eneo la Shinde, Mjini Geita, ambapo marehemu Aloyce Deus, aliuawa kisha pikipiki yake kuporwa.

Kwa mujibu wa maelezo ya upande wa mashitaka, jioni ya siku ya tukio marehemu alipokea simu kutoka kwa mteja wake aitwaye Ester Kichele, aliyemuomba amsaidie kubeba mzigo wa kuni.

Wakiwa njiani, walivamiwa na washtakiwa na kuanguka na pikipiki kabla ya kuanza kushambuliwa.

Inadaiwa kuwa baada ya ajali hiyo, Ester ambaye alikuwa abiria, alikimbilia kwenye pori la Nshinde kujificha.

Washtakiwa wawili walimfuata na kumpora Sh20,000 alizokuwa nazo, huku wakijaribu kumbaka, lakini alifanikiwa kukimbia na kupata msaada wa dereva wa bajaji aliyempeleka mjini.

Mwili wa marehemu ulipatikana baadaye, huku pikipiki ikiwa imefichwa kwenye pori la Nshinde.

Upande wa mashitaka umeeleza kuwa utaleta mashahidi 25 na vielelezo tisa kuthibitisha shitaka hilo, huku washtakiwa wote wanatarajiwa kujitetea wao wenyewe.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *