Moshi. Ikiwa imepita takribani miaka miwili tangu Rais Samia Suluhu Hassan azindue filamu ya The Royal Tour, viongozi wa hifadhi tatu kubwa nchini wanatamani kuona filamu hiyo, au nyingine ikifanyika.
Lengo ni kuendelea kuonesha vivutio mbalimbali duniani. Wamesema tangu filamu hiyo ilipozinduliwa Aprili 18, 2022, na Rais Samia, imeendelea kuchagiza ongezeko la watalii kutoka pande zote za dunia.
Rais Samia alianza kurekodi filamu hiyo Agosti 29, 2021, kwa lengo la kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia vivutio vya utalii. Mbali na kuzinduliwa nchini Marekani, pia alifanya uzinduzi katika Mkoa wa Arusha, Dar es Salaam na Zanzibar.
Wakati akirekodi filamu hiyo pamoja na mwongozaji maarufu wa filamu, Peter Greenberg, Rais Samia alitembelea na kuonyesha kwa wageni vivutio mbalimbali vya utalii, uwekezaji, sanaa na utamaduni vilivyopo nchini.

Hifadhi hizo ni Kilimanjaro (Kinapa), Serengeti (Senapa) ya mkoani Mara, na Tarangire iliyopo mkoani Manyara. Viongozi wa hifadhi hizo wamesema mwitikio umekuwa mkubwa kila mwaka wa watalii kufika kujionea vivutio mbalimbali kwenye hifadhi hizo.
Wameelezea hali hiyo mbele ya waandishi wa habari waliotembelea hifadhi hizo na kuzungumza na watalii pamoja na waongoza watalii.
Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (Kinapa), Angela Nyaki, amesema uongozi wa hifadhi hiyo umeanza kuboresha miundombinu ili kuendana na ongezeko la wageni wanaoongezeka kila mwaka.
“Tumeshuhudia idadi kubwa ya watalii wanaokuja Kilimanjaro baada ya kutazama The Royal Tour. Hii imetufanya tuanze mikakati ya kuimarisha malazi na huduma nyingine kwa wageni wetu ili kuwavutia zaidi na zaidi,” amesema Angela, ambaye ni Kamishna Msaidizi Mwandamizi.
“Lengo ni kuijulisha jamii na dunia kuwa Mlima Kilimanjaro upo Tanzania. Hii ni kwa sababu baadhi ya majirani hudai mlima huo ni wao. Lakini kufanywa kwa filamu hii na Rais kulionesha kabisa umiliki wa mlima huu kuwa upo Tanzania,” anasema Angela.
Amesema filamu hiyo imeisaidia Tanzania kufahamika zaidi kimataifa na itaendelea kufanya hivyo, hususan kutokana na ardhi na rasilimali nyingi ambazo Mungu ametujaalia.
Amesema”Filamu hiyo ililenga zaidi masoko ya utalii barani Amerika na Ulaya: “Na kwa hifadhi ya Kilimanjaro, wageni wanaoongoza ni kutoka Amerika, hasa Marekani, kwa hiyo sisi hiyo filamu ilikwenda kwa walengwa kabisa.”
Kamishna huyo amesema kabla ya filamu hiyo, mwaka 2018/19 walipokea watalii 49,000, na idadi kubwa zaidi ya wageni waliowahi kupokea ilikuwa 54,000.
“Lakini baada ya Royal Tour, mwaka 2021 idadi ya watalii iliongezeka, na mwaka 2022/23 tulipata wageni 53,000, na mwaka 2023/24 tulipata wageni 63,000. Mpaka sasa, kutoka Julai 2024 hadi Februari 2025, tumepata wageni 55,000, na mpaka Juni kufunga mwaka wa fedha tutakuwa tumepokea wageni wengi zaidi,” amesema Angela.
Akigusia mapato, amesema mara ya mwisho kabla ya Royal Tour walikusanya kama Sh81 bilioni, lakini baada ya kufanyika kwa filamu hiyo ikapanda hadi Sh79 bilioni baada ya Uviko -19, na mwaka wa fedha uliopita walikusanya Sh93 bilioni. Kuanzia Julai 2024 hadi Machi 2025, wamekusanya Sh92 bilioni, na hadi Juni itakuwa imeongezeka.
“Ukiangalia, wageni wameongezeka, mapato yanaongezeka. Bado wageni wanaoendelea kututembelea wanatoka Marekani, na filamu hiyo ilizinduliwa kwao. Mimi natamani hata irudiwe, iwe Royal Tour ya namna nyingine au hii hii, tuendelee kuitangaza zaidi na zaidi,” amesema Kamishna Angela.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Watalii Hifadhi ya Tarangire, Upendo Massawe, anasema Tarangire ni hifadhi ya tatu kwa kupokea watalii wengi na idadi ya mapato ikichangia asilimia 11, ikitanguliwa na Serengeti inayoongoza na Kilimanjaro inayoshika nafasi ya pili.

Upendo, ambaye pia anakaimu mkuu wa hifadhi, amesema kumekuwa na ongezeko kubwa la watalii kila mwaka pamoja na mapato. Mathalani, mwaka 2018/19 walipata watalii 216,996, lakini sasa wanakaribia zaidi ya 600,000.
Naye Kaimu Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Serengeti, ambaye pia ni ofisa Mhifadhi Mkuu, Victor Ketansi, amesema hifadhi hiyo ndiyo inayoongoza kwa kuwa na watalii wengi kuliko nyingine yoyote, ikichangia asilimia 54 ya mapato yote yanayokusanywa kwenye hifadhi.
“Ili utalii wa eneo uweze kukua, mambo matatu ni muhimu: vivutio, ufikikaji wa kivutio, na huduma zinazotolewa. Tunapoongelea kukua kwa Hifadhi ya Serengeti, tunazungumzia maeneo hayo matatu,” amesema Ketansi.
Amesema jitihada zaidi zinahitaji kuendelea kufanyika ili kuhakikisha wageni wanaendelea kumiminika nchini, hususan Serengeti, ili kujionea vivutio mbalimbali, huku akitoa wito kwa wadau wengine wanaohusika na utalii kuwakirimu wageni ili kuwa na molari ya kurejea tena.
Wakisemacho watalii
Kim Suk Verheyden, raia wa Uswisi aliyekuwa anashuka kutoka Mlima Kilimanjaro, amesema aliamua kuja nchini kupanda mlima huo mkubwa barani Afrika baada ya kuona filamu kwenye televisheni ikionesha vivutio mbalimbali.
“Niliona filamu ya The Royal Tour kwenye televisheni na nikavutiwa na uzuri wa Mlima Kilimanjaro. Nilihamasika kuja hapa, na nimefurahia kila kitu. Ningependa kuona mwendelezo wa filamu hii ili kuendelea kugundua vivutio vingine vya Tanzania,” amesema Kim.
Kiongozi wa wapandisha watalii Mlima Kilimanjaro, Rogath Mtuy, amesema filamu hiyo imechagiza ongezeko la watalii zaidi ya mara kumi na kuvutia hata watalii kutoka Asia, Iran, na Indonesia.
“Ushiriki wa mama kwenye filamu hii umefanya hata viongozi wengine wa Serikali kuongeza bidii katika maeneo yao. Lakini hii Royal Tour ni vyema iendelee miaka na miaka, kwani kila siku watoto wanazaliwa, na kila siku habari zinapaswa kuwa mpya.
“Kwa hiyo, ni vyema ikarudiwa na ikirudiwa tena, tupeleke tamaduni zetu. Kwa mfano, Wamasai au Hadzabe waambatane na mama ili kuonesha uhalisia wetu,” anasema Mtuy, ambaye mwaka 2000 alitumia saa 14:50 kupanda na kushuka Mlima Kilimanjaro.
Magreth Maina, aliyekuwa na wanafunzi kutoka nchini Canada waliofika Hifadhi ya Tarangire, amesema: “Royal Tour imekuwa sababu ya wao kutembelea Hifadhi ya Tarangire na Ngorongoro ili kujionea kwa macho kile ambacho Rais alikionesha kwenye filamu. Niwasihi Watanzania wenzangu tutembelee vivutio vyetu.”