
WACHEZAJI wakongwe wa soka visiwani Zanzibar watakaovaa na mastaa wa zamani wa Brazili wamefahamika baada ya waratibu wa pambano hilo lililopewa jina la ‘Match of the Legends’ kuweka hadharani leo Alhamisi visiwani hapa.
Mechi ya kimataifa ya kirafiki baina ya wachezaji hao wa zamani wa Brazili wakiongozwa na Ronaldo de Assis Moreira ‘Ronaldinho Gaucho’ dhidi ya wale wa Zanzibar itafanyika Julai 27 katika Uwanja mpya wa Amaan kuanzia saa 2:00 usiku.
Kwa mujibu wa Balozi wa Heshima wa Brazil wa Zanzibar, Abdulsamad Abdulrahim, mechi hiyo itawakutanisha wachezaji maarufu duniani akiwemo Ronaldinho Gaucho na wengine wa zamani kutoka Brazili, huku Zanzibar ikitarajiwa kuongfozwa na Abdallah Juma Alley (Abdulwakati Juma), Murtala Ahmad Kibamba, Bakari Masoud, Nassoro Mwinyi Bwanga na wengineo.
Abdulrahim amesema, nyota wote wa zamani kutoka Brazil watawasili Zanzibar Julai 26 watafanya mazoezi na vijana wenye vipaji vya soka visiwani humo.
Amesema, mechi hiyo itarushwa mubashara duniani kote na inatarajiwa kufikiwa na zaidi ya watazamaji bilioni mbili.
Amesema, mechi hiyo ni tukio la kihistoria katika michezo, likiwa na lengo la kuitangaza Zanzibar kimataifa, hususan huko Brazil, sambamba na kukuza utalii na michezo.
Ameongeza kuwa tukio hilo litachangia maendeleo ya soka Zanzibar na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Kwa mujibu wa Abdulrahim ni kwamba, Ronaldinho mwenye wafuasi zaidi ya milioni 70 kwenye mitandao ya kijamii, ataisaidia Zanzibar kujitangaza kimataifa.
“Hili pia ni sehemu ya kuhamasisha uwekezaji Zanzibar na kuleta msisimko wa maendeleo soka ikiwa pamoja na kuinua na kuendeleza vipaji vya soka kwani Zanzibar. Ni wazi kuwa Zanzibar ina wachezaji wengi wenye vipaji ambao malengo makuu ni kuwaendeleza na kuwa kama akina Ronaldihno,” amesema Abdulrahim.
Kwa upande wa Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Mudrik Ramadhan Soraga, amesema tukio hilo litaongeza mwonekano wa Zanzibar katika soko la utalii la kimataifa, hasa kwa kuwa wawekezaji kadhaa kutoka Brazil wanatarajiwa kuhudhuria.
Soraga ameongeza, serikali itaunga mkono kikamilifu maandalizi ya tukio hilo na kuhakikisha linafanyika kwa mafanikio makubwa.
“Maandalizi ya mechi hii yatakuwa kipimo cha uwezo wa Zanzibar kuandaa mashindano makubwa ya kimataifa, ikiwemo fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2027 na mashindano mengine. Zanzibar tupo tayari kwa Match of the Legends,” amesema Soraga.
Rais wa Klabu ya Yanga, Injinia Hersi Said aliyehudhuria hafla ya utambulisho wa mechi hiyo visiwani hapa, amesema ushiriki wa klabu hiyo katika tukio hilo ni katika kuongeza thamani na kutambua mchango wa muda mrefu wa Yanga katika kukuza soka Zanzibar.
“Hili ni tukio la kihistoria kwa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla. Wachezaji wa hadhi ya juu duniani watatua Zanzibar kwa mara ya kwanza. Ronaldinho ni mchezaji maarufu sana, na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inamleta hapa kwa mara ya kwanza. Tunatarajia mechi ya kusisimua itakayovuta hisia za wengi,” ameema Hersi.
Hersi ameeleza kuwa, tukio hilo halihusu soka pekee, bali linahusisha pia fursa za uwekezaji na burudani mbalimbali ikiwemo onesho la Samba baada ya mechi.
“Yanga tutatumia jukwaa hili kujenga mahusiano na vilabu vya Brazil na kuleta wachezaji kushiriki kwenye tukio hilo,” ameongeza Hersi.