Wataja vinavyokwamisha vijana kujitosa kwenye uongozi

Dar es Salaam. Katika hali ambayo ushiriki wa vijana na wanawake katika uongozi bado uko chini, wadau wa usawa wa kijinsia wamewahimiza makundi hayo kujitokeza na kushiriki kikamilifu katika kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.

Ili kufanikisha hilo, vijana na wanawake wanahimizwa kujiamini, kuondoa hofu na woga na kushiriki kikamilifu katika siasa, taasisi na asasi mbalimbali.

Kauli hiyo imetolewa leo Machi 25, 2025, jijini Dar es Salaam, katika semina ya wadau iliyoandaliwa na Shirika la Mazingira na Haki za Binadamu na Jinsia (Envirocare). Semina hiyo imewakutanisha wanawake, vijana na viongozi wa kiserikali kwa ajili ya kujadili masuala ya uongozi.

Semina hiyo ni sehemu ya mradi wa kuhamasisha ushiriki wa wanawake na vijana katika mifumo ya uongozi, pamoja na kuimarisha uwajibikaji na uwazi katika utawala. Pia, inalenga kuongeza uelewa wa jamii kuhusu masuala ya uongozi.

Akizungumza katika semina hiyo, Dennis Ngonyani kutoka Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), ametaja changamoto kadhaa zinazowakabili vijana katika kushiriki kwenye uongozi.

Miongoni mwa changamoto hizo ni imani potofu, mila na desturi za baadhi ya makabila, changamoto za kiuchumi, hofu, na ukosefu wa kujiamini.

“Vijana wengi wanaamini kuwa uongozi ni wa wazee pekee, ilhali wazee wenyewe wanatamani kusaidiwa na vijana,” amesema Ngonyani.

Ameeleza kuwa, ingawa vijana wameanza kuonyesha mwamko kama ilivyoonekana katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024, bado juhudi zaidi zinahitajika.

“Haya mafunzo kutoka Envirocare yanasaidia kuwajengea vijana ujasiri na kuwafanya watambue kuwa nao wanaweza kuthubutu na kushiriki katika nafasi za uongozi,” amesema.

Magreth Msuya kutoka Chama cha Wananchi (CUF) amewahimiza vijana kuwa na moyo wa kujitolea ili waweze kuendelea. Ametoa rai kwao kutokata tamaa.

Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) Kinondoni, Emanuela Andrea amesema  changamoto kama vikwazo vya kifedha na kukatishwa tamaa zimekuwa kikwazo kwa wanawake, hususan wenye umri mdogo.

“Mimi nilikuwa mwanafunzi wakati nilipogombea, nilikumbana na changamoto kama ukosefu wa fedha, lakini kwa sababu nilionyesha nia na uthubutu, nikaonekana nina uwezo na nikachaguliwa,” amesema.

Msimamizi wa Miradi wa Envirocare, Godlisten Muro amesema shirika hilo kwa sasa linaendesha mradi wa miezi 21 wenye lengo la kuhamasisha ushiriki wa wanawake na vijana katika uongozi.

“Mpaka sasa tumefikia vijana takribani 300 tangu kuanza kwa awamu hii ya mradi kupitia mafunzo mbalimbali. Tumewawezesha vijana hawa kwa mafunzo ya uongozi na wengi wao wamepata ujasiri wa kushiriki kikamilifu katika nafasi mbalimbali za uongozi,” amesema Muro.

Amesema utafiti uliofanywa na shirika hilo, umebaini kuwa changamoto kubwa ni vikwazo vya kiuchumi, mila na desturi potofu, ambazo ingawa zimepungua, bado zinahitajika juhudi zaidi kuziondoa kabisa.

Muro amesema mojawapo ya mbinu zinazotumiwa ni kushirikiana na serikali kuwahamasisha vijana kutumia fursa za mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu ili kuwajengea uwezo wa kiuchumi.

“Tunaamini kuwa vijana wakijijenga kiuchumi wataweza kushiriki vizuri katika uchaguzi mkuu ujao kwa nafasi za madiwani, wabunge, na hata urais. Uchaguzi unahusisha gharama, hivyo ukosefu wa fedha unaweza kuathiri ushiriki wa vijana, tofauti na wazee ambao mara nyingi wana rasilimali zaidi,” amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii katika Manispaa ya Kinondoni, Alex Ntiboneka amesema kuwa juhudi zinaendelea kufanyika ili kupunguza vikwazo vinavyokwamisha ushiriki wa vijana katika uongozi.

“Hatua kubwa ni kuhakikisha vijana wanakuwa na shughuli za kiuchumi. Tunawahimiza vijana kutumia fursa za mikopo ya serikali ya asilimia 10 ili waweze kujitegemea. Kijana akiwa na uwezo wa kifedha, anakuwa na ujasiri wa kugombea nafasi za uongozi badala ya kuwa tegemezi,” amesema Ntiboneka.

Amesisitiza kuwa kila kijana akitumia fursa zilizopo, atakuwa na mchango mkubwa kwa taifa na hatimaye kuongeza ushiriki wa vijana katika uongozi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *