Watafiti waeleza changamoto za mfumo wa usajili mikopo asilimia 10

Musoma. Mfumo wa usajili wa maombi na taarifa za wanufaika wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kupitia mtandao wa ‘Wezesha Portal’ umekumbwa na changamoto kubwa, hasa kwa vikundi vya vijijini kutokana na ukosefu wa mtandao wa uhakika katika maeneo mengi.

Katika kikao kilichofanyika Februari 14, 2025, mjini Musoma, wakati wa uwasilishaji wa matokeo ya utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius Nyerere cha Kilimo na Teknolojia (MJNUAT) kuhusu ufanisi wa mikopo hiyo, wadau walipendekeza suluhisho la changamoto hizo ili kuhakikisha mikopo inawanufaisha walengwa ipasavyo.

Itakumbukwa Aprili 13, 2023, Serikali ilisitisha utoaji wa mikopo hiyo ili kufanya maboresho, ikiwa ni pamoja na kuandaa mfumo mpya wa utoaji wake. Baada ya maboresho hayo, mikopo ilianza kutolewa tena Julai mosi, 2024.

Mshiriki kutoka MJNUAT, Dk Lekumok Kironyi, alizungumza na Mwananchi leo Jumapili Februari 16, 2025, amesema kusema kuwa pamoja na changamoto ya mtandao, usajili wa maombi unahitaji vifaa vya kielektroniki kama kompyuta au simu janja, ambavyo wanufaika wengi hawana.

“Wengi wanategemea simu janja kwa usajili, lakini si kila mtu anamiliki simu hizo. Kuna vikundi ambavyo hakuna hata mmoja anayemiliki simu ya kisasa, hivyo wanalazimika kwenda kwenye vituo vya huduma za ofisi (stationery). Swali ni je, huduma hizo zinapatikana kila mahali, hasa vijijini?” amehoji Kironyi.

Mkazi wa Serengeti, Mungere Majura, amesema wanufaika wanakabiliwa na gharama kubwa za usajili zinazofikia kati ya Sh10,000 hadi Sh25,000 kulingana na eneo, hali inayoongeza mzigo wa kifedha katika mchakato huo.

“Wanatozwa fedha nyingi ili wafanikishe usajili. Kwa kuwa hawana njia mbadala, wanalazimika kulipa, vinginevyo hawawezi kusajiliwa, jambo linalowakwamisha kupata mikopo,” amesema.

Wadau pia wamebainisha kuwa tafsiri ya ulemavu bado ni changamoto, wakisema hakuna mwongozo rasmi unaobainisha sifa za walengwa wa mikopo katika kundi la watu wenye ulemavu, hususan wale wenye ulemavu usioonekana moja kwa moja.

Hata hivyo, Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, Zakaria Mrope, amependekeza kuwepo kwa mwongozo rasmi wa kutambua watu wenye ulemavu ili kurahisisha utoaji wa mikopo kwa kundi hilo.

Mratibu wa Utafiti kutoka MJNUAT, Dk Joel Joshua, amesema changamoto zilizobainika wakati wa utafiti zimeshughulikiwa katika maboresho ya mwaka jana.

“Baadhi ya marekebisho yaliyofanyika ni pamoja na suala la umri, mtu binafsi kukopa na ushirikishwaji wa taasisi za kifedha. Tunaamini maboresho haya yataongeza manufaa ya mikopo kwa walengwa na jamii kwa ujumla,” amesema.

Dk Joshua amesema utafiti huo uliofanywa kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) tangu mwaka 2022, ulilenga kutoa mapendekezo ya namna bora ya kuwawezesha vijana na wanawake kuanzisha biashara na kuzalisha ajira kupitia mikopo isiyo na riba.

Naye, Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala Bora kutoka Tamisemi, Stephen Motambi, amehimiza watafiti kuendelea kufanya tafiti zaidi kuhusu uboreshaji wa mfumo wa utoaji mikopo.

“Endeleeni kufanya utafiti kuhusu Wezesha Portal na changamoto zake kwa watu wa vijijini ili tuweze kuboresha zaidi mfumo huu na kufanikisha malengo yake,” amesema.

Amesema kati ya Novemba na Desemba 2024, mikopo yenye thamani ya zaidi ya Sh22 bilioni ilitolewa kwa wanufaika 2,076 nchini kote.