
Dar es Salaam. Wakati Serikali ikitangaza mlipuko wa ugonjwa wa homa ya nyani unaosababishwa na virusi vya Mpox, wataalamu wamefafanua jinsi ya kujikinga na ugonjwa huo, huku wakishauri hatua za kuchukua kwa sasa.
Ugonjwa huo ulioripotiwa jijini Dar es Salaam ni mara ya kwanza kutokea nchini, huku ukiwa umeripotiwa mara kadhaa katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Uganda.
Jana, Machi 10, 2025, Waziri wa Afya, Jenister Mhagama, alitoa taarifa kwa umma akibainisha kuwa watu wawili waliohisiwa na kutengwa katika eneo la Majani ya Chai, Kipawa, Ilala kwa ajili ya matibabu, walibainika kuwa na ugonjwa wa Mpox.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), ugonjwa huo unaosababishwa na virusi vya Mpox unasambaa kwa njia za matone ya mfumo wa njia ya hewa, ngozi kupitia kugusana na kujamiiana na mtu mwenye maambukizi.
Pia, ugonjwa huo unaenea kutoka kwa mnyama kwenda kwa binadamu. Mpox husambaa kupitia majimaji ya mwili, ikiwemo mate, matapishi, jasho na mkojo.
Akizungumza kuhusu ugonjwa huo, Mratibu wa Huduma za Afya ngazi ya jamii katika Wizara ya Afya, Dk Norman Jonas, ametaja dalili za ugonjwa huo kuwa ni upele, malengelenge au vidonda kwenye mwili, hasa mikononi na miguuni, kifuani, usoni na wakati mwingine sehemu za siri.
Amezitaja dalili nyingine kuwa ni homa, maumivu ya kichwa, misuli, mgongo, uchovu na kuvimba mitoki.
Namna ya Kujikinga
Amesema ili kujikinga, watu wanapaswa kuepuka kugusa majimaji ya mwili wa mtu mwenye maambukizi, kusalimiana kwa kukumbatiana, kubusiana, kushikana mikono au kugusana na mtu mwenye dalili za ugonjwa huo.
Amesema ni muhimu kusafisha na kutakasa vyombo vilivyotumika na mhisiwa au mgonjwa pamoja na maeneo yote yanayoguswa mara kwa mara.
“Kuvaa barakoa iwapo itabidi kukaa na kuongea kwa karibu na mtu mwenye dalili za Mpox, kuwahi vituo vya huduma za afya unapoona dalili za ugonjwa wa Mpox. Watoa huduma za afya wanatakiwa wazingatie miongozo ya kuzuia kusambaa kwa maambukizi (IPC) wakati wote wanapowahudumia wagonjwa,” amesema Dk Norman.
Wataalamu wa afya wamesisitiza umuhimu wa mamlaka kutoa elimu ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo.
Wamesema, kulingana na njia zinazochangia maambukizi na aina ya maisha ya watu wa jiji hilo, ni rahisi zaidi kutokomeza maambukizi kwa kutoa elimu kwa wananchi juu ya namna ya kujikinga.
Chama cha Madaktari
Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) kimezitaka mamlaka kuhakikisha zinatoa elimu kuhusu dalili na jinsi ugonjwa huo unavyoambukiza, pamoja na hatua za kuchukua wanapoona dalili kwa kuwahi vituo vya kutolea huduma vilivyoainishwa.
Rais wa MAT, Dk Mugisha Nkoronko, amesema kuna umuhimu wa kufuata kanuni za kujikinga, kwani Mpox ni ugonjwa unaoharibu mwonekano wa mtu kwa kutoka vipele kwenye mwili wake, vinavyotoa majimaji na kugusana na mtu mwingine, hivyo kusababisha maambukizi.
“Serikali iongeze jitihada za ufuatiliaji wa ugonjwa huu, pia kuimarisha uchunguzi mipakani. Ni vizuri kuendelea kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa ya mlipuko, kwani siku zijazo, kulingana na mabadiliko ya tabianchi, yataibuka magonjwa mengi zaidi,” amesema Dk Nkoronko.
Pia, amewataka watoa huduma za afya kuhakikisha wanafuata miongozo ya kujikinga ili kuepuka kupata maambukizi wao binafsi na wagonjwa wanaowahudumia.
“Chama cha Madaktari kinawaomba watoa huduma wote kutumia kwa usahihi vifaa vya kuzuia maambukizi, kuhakikisha wanavaa vifaa kinga na kuweka mikakati ya kubaini na kudhibiti maambukizi, hasa wakati wa kusafirisha mgonjwa kutoka kituo alichopo mpaka vituo vilivyoanishwa na Serikali,” amesema.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani na Mfumo wa Upumuaji kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Elisha Osati, amesema jiji la Dar es Salaam lina msongamano mkubwa wa watu, hivyo hatua za haraka za kukinga ugonjwa huo zisipochukuliwa, ukisambaa itakuwa vigumu kuudhibiti.
“Mwingiliano wa watu ni mkubwa, cha msingi ni kuhakikisha tunajilinda na kujikinga kama mwongozo uliotolewa na Wizara ya Afya unavyotutaka. Pia, tuna uzoefu tangu Uviko-19, tumekuwa tukipewa maelekezo namna ya kujikinga na haya magonjwa ya mlipuko, na namna ya kujikinga ni ileile.
“Wizara pia itoe elimu ili mtu akihisi dalili za ugonjwa, aende hospitali haraka na pia kuepuka kuambukiza wengine,” amesema Dk Osati.
Dk Osati amesema pia mamlaka za jiji zinapaswa kuchukua hatua za kutoa taarifa sahihi kwa wananchi na kuhakikisha elimu ya afya inatolewa kwenye mikusanyiko, ikiwemo shule na masoko. “Wasije wakapuuzia na mwishowe tukajikuta tumepata mlipuko mkubwa zaidi,” amesema.
Zahanati ya Kipawa
Mwananchi ilifika katika Zahanati ya Kipawa, jijini Dar es Salaam, eneo ambako hivi karibuni kwenye mitandao ya kijamii kulisambaa video ikionyesha kuwa kuna mgonjwa wa Mpox. Katika eneo hilo, huduma nyingine zinaendelea kama kawaida, huku upande mmoja wa jengo la hospitali ukiwa umezungushiwa utepe mwekundu.
Mmoja wa viongozi wa hospitali hiyo, ambaye hakutaka kutajwa jina, alipoulizwa kuhusu utepe huo, amesema wameweka alama hiyo ili kuwakinga watu kwa sababu ya rashers (vipele).
Mwananchi iliyokaa eneo hilo kwa zaidi ya saa moja, ilishuhudia watu wachache wakiingia na kutoka kwenye eneo lililozungushiwa utepe, huku magari mawili ya wagonjwa yakiwa yamepaki mbele ya geti kuu karibu na eneo hilo.
Baadhi ya watu wanaoishi mita 200 kutoka eneo hilo wamesema kuwa, licha ya kusikia taarifa za ugonjwa huo, hawana hofu kwa kuwa wameambiwa hauambukizi kwa njia ya hewa.
“Tulisikia tu kwamba kuna mgonjwa wa Mpox alipatikana hapo, na mara kadhaa tumeona gari la wagonjwa likiingia na kutoka, lakini sisi haturuhusiwi kusogea kwenye eneo hilo,” amesema Rajabu Shabani.
Mathayo Mabula, amesema pamoja na kusikia taarifa hizo, hawana wasiwasi. “Ingekuwa ni kwa njia ya hewa, tungeomba ulinzi zaidi, lakini hapo pembezoni (akionyesha ukuta wa jengo hilo) kama una ndugu yako yumo ndani unaweza kumpigia simu akatoka mkaongea naye wewe ukiwa upande wa barabara hakuna shida.”
Mpox, iliyojulikana awali kama Monkeypox, ilitambulika kwa mara ya kwanza kwa binadamu mwaka 1970 katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na kihistoria umekuwa ukipatikana katika maeneo ya Afrika ya Kati na Magharibi.