Mwanza. Gugumaji jipya jamii ya Salvania SPP limebainika katika Ziwa Victoria, ambalo lina uwezo wa kuzaliana zaidi ya mara mbili hadi tatu kila baada ya siku nane, hivyo kufanya ongezeko lake kuwa kubwa ndani ya kipindi kifupi.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo Jumapili, Machi 2, 2025, Meneja wa Baraza la Taifa la Usimamizi na Hifadhi ya Mazingira (NEMC) Kanda ya Ziwa Victoria, Jarome Kayombo, amesema sababu kubwa ya kuzaliana kwa gugumaji hilo ni ongezeko la virutubisho ndani ya ziwa, jambo linalosababishwa na shughuli za kibinadamu zisizozingatia utunzaji endelevu wa mazingira.
“Agosti 2024, wavuvi katika mialo ya Buyagu Wilaya ya Sengerema, Chole, Nyahiti na Mbarika Wilaya ya Misungwi walianza kuona gugumaji jipya jamii ya Salvania SPP. Taarifa zinatanabaisha kwamba, kutokana na upepo, gugumaji hilo jipya lilianza kusambaa maeneo tofauti kutegemea mwelekeo wa upepo,” amesema Kayombo.
Januari 2025, ilishuhudiwa ongezeko kubwa la gugumaji hilo na kuanza kuleta athari mbalimbali kwenye sekta ya uvuvi na vyombo vya usafiri, hususan vivuko katika eneo la Kigongo-Busisi, na kuzorotesha huduma ya usafiri kati ya Mkoa wa Mwanza na maeneo mengine yanayotegemea kivuko.

Amesema baada ya athari hizo, ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza iliunda kikosi kazi kilichojumuisha wataalamu kutoka ofisi yake, Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB), NEMC, Mamlaka ya Afya ya Mimea (TPHPA) Kanda ya Ziwa, Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (TAFIRI), Chuo cha Uvuvi Mwanza, kwa lengo la kubaini aina ya gugumaji na namna ya kukabiliana nalo kwa haraka.
Wataalamu wengine walitoka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Halmashauri za Misungwi na Sengerema, TAMESA, Mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) na Vikundi vya Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU).
“Kikosi kazi kimebaini aina ya gugumaji, tabia za uzalianaji na usambaaji, mambo yanayosababisha kushamili na maeneo ambayo tayari yameshavamiwa na gugumaji hilo. Pia, kikosi kazi kilifanikiwa kuopoa zaidi ya tani 36 za gugumaji katika eneo la Kigongo-Busisi,” amesema.
Ameeleza kasi kubwa ya ongezeko la gugumaji hilo inatokana na shughuli za kilimo, utupaji holela wa taka maji na taka ngumu kutoka viwandani na majumbani, ujenzi wa makazi, shughuli za uvuvi na ufugaji samaki zinazofanyika bila kuzingatia taratibu za utunzaji wa mazingira, mahoteli au viwanda kandokando ya ziwa bila kuwa na miundombinu ya kukusanya taka.
Sababu nyingine ni ukataji miti na shughuli za uchimbaji madini bila kuzingatia dhana ya maendeleo endelevu, na kuvamia eneo tengefu la mita sitini kutoka kwenye kingo za mito au ziwa. Hali hii inachangia ongezeko la virutubisho kwenye ziwa na hivyo kasi kubwa ya ongezeko la gugumaji.
“Pamoja na madhara ya gugumaji jipya (salvinia spp) ambayo tayari yameshatukumba, gugumaji hili linaathiri pia maisha ya viumbe hai majini (wakiwemo samaki) kwa kukosa hewa (oxygen), ubora na upatikanani wa maji, shughuli za uvuvi, shughuli za ufugaji samaki, usafirishaji kwa njia ya maji, mifumo ikolojia na bioanuai,” amesema.
Amesema: “Kwa kifupi, gugumaji jamii ya Salvinia lina athari kubwa kwenye sekta za uvuvi, usafiri na usafirishaji kwenye ziwa, usambazaji wa maji safi na salama, shughuli za utalii na afya za binadamu. Hivyo, jitihada za pamoja zinahitajika kati ya Serikali, taasisi zisizo za kiserikali, mashirika ya kimataifa, wadau wa maendeleo na wananchi wote ili kuokoa uchumi wa nchi na changamoto za kijamii na kimazingira.”
Amesema ili kukabiliana na changamoto hiyo, NEMC kwa kushirikiana na wadau wana hakikisha uwekezaji kando na ndani ya Ziwa Victoria unazingatia sheria zote za nchi, ikiwemo kufanya tathmini ya athari ya mazingira kabla ya kuanza uwekezaji ili kupunguza uchafuzi kwenye ziwa.
Amesema baraza hilo limeandaa mpango kabambe na limeshaanza kufanya kaguzi maalum 134 katika maeneo yote yanayozunguka Ziwa Victoria, hususan viwanda, mashamba, hoteli, migodi, na miundombinu ya maji taka na ukusanyaji wa taka ngumu ili kubaini vyanzo vya uchafuzi wa ziwa hilo.
“Baraza limeandaa mpango kabambe wa ukaguzi na utoaji elimu kwa wafugaji wa samaki kubaini wale wote waliozingatia matakwa ya kisheria na kufuga kwa mujibu wa miongozo waliyopewa, yaani kuzingatia uwezo wa eneo na kiasi ya samaki kinachotakiwa kufugwa (carrying capacity), na kuzingatia misingi yote ya utunzaji wa ubora wa maji ya ziwa,” ameeleza.
Amesema baraza hilo kwa kushirikiana na LVBWB, mamlaka za serikali mitaa litaendelea kusimamia wajibu wa kuacha mita 60 kwa mujibu wa sheria ya mazingira ya mwaka 2004 na kanuni zake katika eneo tengefu hususani kwenye kingo za mito na ziwa, ambayo husaidia kuchuja uchafu hususani kipindi cha mvua na kupunguza uchafuzi wa ziwa.
“Baraza linatoa onyo kali kwa wawekezaji wote wanaowekeza kando au ndani ya ziwa ambao wanafanya uwekezaji bila kufuata matakwa ya kisheria.
“Mathalani, uwekezaji bila kufanya tathmini ya athari ya mazingira, ambao ni mchakato pekee unaowaleta wadau wote pamoja wakiwemo wananchi ili kujiridhisha namna bora ya uendeshaji miradi na kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji,” amesema.
Mvuvi eneo la Luchelele, Kulwa Joseph, ameomba wadau mbalimbali kulitokomeza gugumaji hilo kwa kuwa linaathiri mazalia ya samaki na kufanya samaki aina ya sangara kukimbilia kina kirefu zaidi, na kufanya upatikanaji wake kuwa wa shida.