Dar es Salaam. Madaktari bingwa kutoka barani Ulaya wameanza kuwajengea uwezo wataalamu wa afya nchini Tanzania mbinu za kutibu uvimbe kwenye mishipa na matatizo kwenye sakafu ya ubongo, lengo kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi.
Kufuatia mafunzo hayo wagonjwa wenye matatizo hayo kwa asilimia 90 hadi 95 nchini watakuwa wanatibiwa nchini.
Tayari wataalamu kutoka Shirikisho la Wataalamu wa Mishipa barani Ulaya, wapo nchini kwa ziara ya siku tano kwa ajili ya kutoa mafunzo hayo kwa wataalamu wa ndani.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Idara ya Tiba katika Wizara ya Afya, Dk Hamad Nyembea, wakati akifungua mafunzo ya wataalamu wa upasuaji wa mifumo ya fahamu na uti wa mgongo leo Jumapili, Mei 18, 2025, jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Tiba Wizara ya Afya Dk Nyembea
“Mafunzo haya yanahusisha nchi 17 za Afrika na yamekuja wakati ambao Serikali ina uhitaji mkubwa wa wataalamu wenye ujuzi wa hali ya juu, hasa ikizingatiwa kuwa tayari uwekezaji mkubwa umefanyika katika sekta ya afya, hususan katika huduma za kibingwa na ubobezi.
“Tuna hospitali saba zinazotoa huduma za ubobezi. Kupitia mafunzo haya, wataalamu wetu watajengewa ujuzi wa upasuaji wa mishipa ya ubongo, ambao hatukuwa nao awali. Wagonjwa wengi walilazimika kusafirishwa kwenda nje kwa matibabu hayo,” amesema.
Kutokana na changamoto hiyo, Dk Nyembea amesema mafunzo hayo yatawawezesha wataalamu katika hospitali hizo saba kuanza kutoa huduma hiyo ndani ya nchi.
Ameeleza magonjwa yasiyo ya kuambukiza, yakiwemo shinikizo la damu, kiharusi, uvimbe na saratani, yameongezeka, jambo ambalo limechangia kuongezeka kwa matatizo yanayohitaji upasuaji kwenye mishipa ya ubongo.
Hali hiyo imesababisha Serikali kutumia gharama kubwa kuwasafirisha wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi.
“Tunataka hospitali zetu ziwe na uwezo mkubwa kwenye eneo hili, na ndiyo maana tumewaalika wenzetu kutoka Ulaya kuja kusaidia kuimarisha uwezo wa wataalamu wetu wa ndani,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), Dk Mpoki Ulisubisya, amesema kupitia mafunzo hayo, asilimia 90 hadi 95 ya wagonjwa wenye matatizo hayo watakuwa wanatibiwa nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dk Mpoki Ulisubisya
“Mafunzo haya yatawanufaisha hata wanafunzi waliopo vyuoni wanaosomea ubingwa na ubobezi kwa nchi za Afrika.
Wataalamu hawa wote wamehitimu na wanafanya kazi hizi kwa sababu magonjwa yanabadilika, na hivyo tunaboresha mbinu za matibabu. Wagonjwa sasa watakaa hospitalini kwa muda mfupi zaidi,” amesema.
Kwa upande wake Daktari wa mishipa ya fahamu kutoka MOI, Dk Nicephorous Rutabasigwa amesema kwa kila watu 100,000, 10 wanasumbuliwa na tatizo la uvimbe kwenye mishipa na sakafu ya ubongo.

Mkurugenzi wa Tiba Wizara ya Afya, Dk Hamad Nyembea katikati na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) Dk Mpoki Ulisubisya, wengine pichani ni wataalamu kutoka Ulaya ambao watatoa mafunzo kwa wataalamu hao nchini na nje ya nchi.
Amesema kwa MOI kila wiki wanapokea wagonjwa wawili hadi watatu wanaosumbuliwa na tatizo hilo na kwa mwezi wanafanya upasuaji kwa wagonjwa 15 wenye matatizo hayo.
“Matatizo ya uvimbe unasababishwa na shinikizo la juu la damu kwa wagonjwa ambao hawajui kama wana shida hiyo na mishipa ya damu ikipasuka mgonjwa hufariki,”amesema.