
Unguja. Tathimini ya uwiano wa wagonjwa na wahudumu wa afya Zanzibar mwaka 2023/24 imeonesha kuwa kila daktari mmoja anatibu wagonjwa 3,904 ambapo kwa mwaka 2021/22 takwimu zilionesha kuwa kila daktari mmoja alitibu wagonjwa 4,445.
Kwa upande wa wauguzi tathimini ya mwaka 2023/24 muuguzi mmoja alihudumia wagonjwa 1,089 ikilinganishwa na takwimu za mwaka 2021/22 zilizoonesha kuwa kwa kila muuguzi mmoja alihudumia wagonjwa 1,258.
Hayo yamebainishwa leo Februari 28,2025kwenye Baraza la Wawakilishi na Naibu Waziri wa Afya Zanzibar, Hafidh Khamis Hassan wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Mwanakwerekwe, Ameir Abdalla Ameir.
Mwakilishi huyo, alitaka kujua tathimini ya uwiano wa wagonjwa na wahudumu wa afya na kwa vipi inachochea ustawi bora katika upatikanaji huduma za afya.
Akijibu, swali hilo, Naibu Hafidh amesema kwa viwango vya kimataifa vinaeleza kuwa kila daktari mmoja anatakiwa kutibu wagonjwa 10,000 na kila muuguzi mmoja anatakiwa kuwahudumia wagonjwa 6,000.
“Kwa mwaka 2021/22 takwimu zinaonesha kila daktari mmoja alitibu wagonjwa 4,445 ikilinganishwa na mwaka 2023-2024 ambapo kila daktari mmoja alitibu wagonjwa 3,904.
“Kwa upande wa wauguzi kwa mwaka 2021/22 takwimu zinaonesha kila muuguzi mmoja alihudumia wagonjwa 1,258 ambapo kwa mwaka 2023/24 kila muuguzi mmoja amehudumia wagonjwa 1,089,” amesema Hafidh.
Amesema, tathimini hiyo inaonesha kuwa uwiano wa Zanzibar unaweza kuchochea upatikanaji bora wa huduma za afya kwa kiwango cha ziada ya wahudumu wa afya kwa takriban asilimia 64.04 kwa madaktari.
Pia, amesema kwa upande wa wauguzi ni asilimia 22.17 ikilinganishwa na kiwango (ratio) ya Shirika la Afya Duniani (WHO) vinavyoelekeza kila daktari mmoja anatakiwa kutibu wagonjwa 10,000 na kila muuguzi mmoja anatakiwa kuwahudumia wagonjwa 6,000.
Amesema, hali hiyo inaonesha kuwa kiwango (ratio) cha watoa huduma za afya Zanzibar ni kikubwa ikilinganishwa na kiwango (standard) inayotakiwa kimataifa.