Wastaafu watarajiwa wapewa mbinu kabla ya kustaafu kazi

Unguja. Imebainika kuwa ili mstaafu aishi maisha mazuri baada ya kustaafu, anahitaji angalau asilimia 70 ya mapato aliyokuwa akipata kabla ya kustaafu.

Kutokana na hilo, wataalamu wanashauri kuwa maandalizi yanapaswa kuanza kati ya miaka 20 hadi 30 kabla ya kustaafu, kwa kuwekeza katika biashara walizokuwa na ndoto nazo.

Hayo yameelezwa leo Jumatatu Machi 3, 2023 na mkuu wa mafunzo ya muda mfupi kutoka Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Dorah Chenyambuga, wakati akiwasilisha mada kwa wastaafu watarajiwa wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF), mjini Unguja.

“Mstaafu anatakiwa kuanza maandalizi mapema, angalau miaka 20 hadi 30 kabla ya kustaafu, kwani inakadiriwa kuwa ili aishi vizuri, anahitaji asilimia 70 hadi 80 ya mapato aliyokuwa akipata kabla ya kustaafu,” amesema Dorah.

Aidha, amesema katika miezi mitatu ya kwanza baada ya kustaafu, ni muhimu wastaafu kupumzika kwa ajili ya kujiandaa vizuri kiuchumi, kisaikolojia na kijamii, ili waweze kuwekeza fedha zao katika maeneo yatakayowaletea faida.

Ameeleza pia kuwa wastaafu wasipojiandaa ipasavyo, wanaweza kukumbwa na changamoto za kiafya, ikiwemo msongo wa mawazo na hofu ya maisha yao ya baadaye.

“Kuna wastaafu ambao kwa kutokuwa na maandalizi, wanapata msongo wa mawazo na hata hofu ya kufa kila wakati. Hili linaweza kuepukwa kwa kuwa na mpango madhubuti wa maisha baada ya kustaafu,” amesema Dorah.

Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Dk Saada Mkuya akizungumza katika mafunzo ya maandalizi ya kustaafu kwa wastaafu watarajiwa wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF).

Ameonya kuwa baadhi ya wastaafu huingia kwenye biashara wasizozifahamu vizuri, jambo linalowasababishia hasara. Vilevile, ameeleza kuwa nidhamu ya matumizi ya fedha na utaratibu wa kuwekeza ni mambo muhimu katika kuhakikisha maisha bora baada ya kustaafu.

“Tatizo kubwa ni kwamba watu wengi hawana nidhamu ya fedha, wala ndoto ya maisha baada ya kustaafu. Matokeo yake ni kutumia fedha kiholela na baadaye kujikuta katika hali ngumu,” amesema Dorah.

Kwa upande wake, mshiriki wa mafunzo hayo, Maryam Rabia, amesema elimu waliyoipata imewapa mwanga mpya kuhusu jinsi ya kusimamia fedha zao baada ya kustaafu.

“Mojawapo ya mambo tuliyojifunza ni umuhimu wa kutotumia fedha za kiinua mgongo kwa kuwapa watoto bila mpangilio wa kibiashara. Badala yake, tunapaswa kuzihifadhi benki huku tukifikiria mipango sahihi ya kuzitumia,” amesema Maryam.

Naye Hamza Juma Hamza, mshiriki mwingine wa mafunzo hayo, amesema hana hofu ya kustaafu kwa sababu alishajipanga mapema na hakuwa mtu wa kutegemea mshahara pekee.

Hamza amewashauri wafanyakazi kuachana na mtazamo wa kuona kuwa sehemu ya kazi ni mahali pa kuishi milele, bali wawe karibu na jamii zao ili kujenga mazingira mazuri ya baadaye.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Dk Saada Mkuya, amesema changamoto kubwa inayowakumba wastaafu ni ukosefu wa elimu na miongozo ya kuzitumia fursa zilizopo.

“Hakuna sababu ya wastaafu kuishi maisha magumu baada ya kustaafu, kwani fedha wanazopata kutoka kwenye kiinua mgongo na mafao zinatosha kuwaimarisha kiuchumi,” amesema Dk Saada.

Ameonya kuwa baadhi ya wastaafu huwekeza fedha zao katika taasisi ambazo hazijasajiliwa, jambo ambalo linawaweka katika hatari ya kupoteza akiba zao.

Mkurugenzi Mtendaji wa ZSSF, Nassor Shaaban, amesema mfuko huo unaendelea kuwahamasisha wastaafu kuhusu maandalizi yao ya baada ya kustaafu.

“Tumeimarisha mifumo yetu, na sasa mafao yanapatikana ndani ya siku 14, tofauti na awali ambapo ilichukua hadi miezi miwili baada ya mshahara kupokelewa,” amesema Nassor.