
Dodoma. Serikali ya Tanzania imetenga jumla ya Sh207 bilioni katika mwaka wa fedha 2025/26 kwa ajili ya kuwalipa wastaafu wanaodai fedha zao wakiwemo askari wa magereza wanaodai malipo na malimbikizo.
Kauli hiyo imetolewa bungeni leo Jumanne Mei 13, 2025 na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais- Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deus Sangu ambaye amewaagiza wakurugenzi kuwalipa wastaafu waliopandishwa madaraja kisha hatua hizo kusitishwa mwaka 2016.
Ametoa kauli hiyo wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum, Esther Matiko aliyeuliza ni lini Serikali itawalipa fedha askari Magereza waliostaafu lakini hawajalipwa malipo yao ikiwemo nauli.
Katika swali la msingi, Mbunge wa Nyasa (CCM), Stella Manyanya ameuliza ni lini Serikali itawalipa wastaafu waliopandishwa madaraja kisha hatua hizo kusitishwa.
Naibu Waziri amekiri kuwa Serikali inatambua uwepo wa watumishi ambao walipandishwa vyeo na barua zao za kupandishwa vyeo kuingizwa kwenye Mfumo wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara na baadaye upandishwaji vyeo huo kusitishwa Juni 2016 ili kupisha uhakiki.
“Kundi hili linajumuisha pia watumishi waliostaafu kazi kabla ya Serikali kuruhusu tena upandishaji wa vyeo kuanzia Novemba, 2017 na tunaendelea kuwalipa ambapo hadi sasa tumelipa Sh2.7 bilioni kwa watumishi 1,200,” amesema Sangu.
Amesema kufuatia hatua hiyo, Serikali iliridhia na kuelekeza watumishi wastaafu wa aina hiyo ambao wanastahili kulipwa madai ya malimbikizo ya mishahara ya kuanzia walipopandishwa vyeo hadi tarehe walipostaafu kazi, walipwe madai yao ya malimbikizo ya mishahara.
Amesema malipo ya madai hayo yamekuwa yakifanywa na Serikali kwa wastaafu hao kupitia kwa waliokuwa waajiri wao.