Na Malima Lubasha, Serengeti
Jumla ya watumishi wastaafu serikalini 123 katika Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, wameshauri benki ya Azania kupunguza asilimia ya riba kwa mikopo inayosomeka tarakimu mbili na kupendekeza isomeke tarakimu moja ili kuwapa nafuu ya kukopa.
Ushauri huo umetolewa na wastaafu hao wakati wakipata elimu juu ya mikopo na fursa za kifedha inayotolewa na benki hiyo kwenye ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Uuguzi na Ukunga cha Kisare Hospitali ya Nyerere DDH Mugumu Serengeti.
Ofisa Mikopo benki hiyo tawi la Musoma, Irene Gidion wa amesema wanatoa elimu ya mikopo na fursa mbalimbali za kibenki ambayo ni nafuu kwa wastaafu lengo ikiwa ni kuboresha maisha yao na kufafanua kuwa benki hiyo ni mali ya serikali na inatoa huduma kama benki nyingine wakishirikiana na mifuko ya jamii.

“ Azania Benki ni kama nyingine katika kutoa huduma za kifedha ni mali ya serikali ambayo ina zaidi ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwake na inawahusu wastaafu kufungua akaunti na kuchukua mikopo kwa riba nafuu kwani ina matawi mbalimbali hapa nchini,” amesema Irene.
Amesema benki hiyo kwa kuenzi michango ya watumishi wastaafu waliolitumikia taifa kwa uadilifu benki kwa kushirikiana na mifuko ya hifadhi ya jamii NSSF na PSSSF inatoa mikopo kwa asilimia 14 tofauti na benki nyingine kuanzia miezi nane hadi miaka tisa, kiwango cha mkopo ni kuanzi sh 15,000 hadi milioni 500 ambayo ina bima.
Amesema ili mteja aweze kupata mkopo huo ni lazima kufungua akaunti katika benki hiyo ambapo aliwatahadharisha wastaafu hao kuwa mtu haruhusiwi kuwa na mikopo katika benki mbili ni muhimu uwe na mkopo benki moja aidha unapokuwa na mkopo benki nyingine na anataka kukopa Azania wataununua mkopo huo.
Amefafanua kuwa Afisa mikopo wanatoa huduma za kifedha kutumia mawakala, ATM pia zipo huduma za mobile,WhatsApp ili kusaidia wateja wasitembee umbali mrefu kufuata huduma .

“ Tuna akaunti kwa mtu mmoja mmoja, vikundi, wakulima, wajasiriamali na akaunti ya mwanamke hodari ambayo huduma hii inawasaidia wanawake kukopa kwa asilimia 1 na fedha zinakuwa salama,” amesema.
Wakiuliza maswali na kujadili mada zilizowasilishwa kwao na wawezeshaji wastaafu waliomba asilimia 14 ya mkopo inayotozwa na benki ni kubwa kulingana kiwango cha pensheni, hivyo ipunguzwe angalau kufikia asilimia tisa.
Naye Nyamhanga ambaye ni Ofisa Mahusiano wa Azania tawi la Mugumu wilayani Serengeti amesema benki hiyo inatoa mikopo kwa wafugaji, wakulima pia mikopo ya vikundi ambapo alitaka wastaafu kujiunga na kufungua akaunti na muda wa kurejesha mkopo ni miezi 108.