Wasomi wataja mwarobaini malalamiko ya uchaguzi

Dodoma. Wachambuzi wa masuala ya siasa nchini wamesema malalamiko ya vyama vya upinzani kuchezewa rafu katika chaguzi za serikali za mitaa yataendelea kuwepo hadi pale kutakapokuwa na chombo cha uchaguzi chenye uwezo wa kusimamia ushindani.

Katika hatua ya kuteua wagombea, vyama vya upinzani vimelalamikia kuenguliwa kwa wagombea wake kinyume na kanuni za uchaguzi wa serikali za mitaa, ikiwemo wale waliojaza fomu za kuomba uteuzi kutaja shughuli za kujipatia kipato halali ni ujasiriamali.

Wengine walioenguliwa wanatajwa kuwa ni wale waliojaza fomu bila kuweka picha za wagombea, wakati kwenye kanuni hakuna kigezo hicho.

Wakati vyama vya upinzani vikitaja sababu hizo, wasimamizi wa uchaguzi wanasema wamewaengua wagombea kwa kusaini fomu zao wenyewe na wengine kutojiandikisha kwenye daftari la wapigakura.

Mbali na hilo, vyama hivyo vimelalamikia baadhi ya ofisi kufungwa walipokwenda kuwasilisha mapingamizi yao ya kutoteuliwa kugombea kwenye uchaguzi huo utakaofanyika Novemba 27, mwaka huu.

Hata hivyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa amewataka wagombea wenye malalamiko kufuata sheria, kanuni na miongozo kwa kuwasilisha mapingamizi yao mahali na kwa wakati husika.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu, Novemba 11,2024, Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Luisulie amesema malalamiko hayo yanaonyesha kutokuwepo kwa ushindani kutokana na kukosekana kwa chombo cha kusimamia ushindani,  kwa maana Tume ya Uchaguzi.

Amesema siku ambayo Tanzania itapata chombo ambacho hakiegemei upande wowote malalamiko hayo yatapungua ama yatakwisha.

“Kwa sasa hivi Serikali ndio inayosimamia uchaguzi, lakini sasa Serikali (kwa kuwa ni ya CCM) hiyo ndio inawagombea pia kwa vyovyote vile huwezi kutegemea kukawa na usawa.

“Haya mabishano yataendelea hadi hapo chombo cha kusimamia uchaguzi kitakapopatikana kutakuwepo na unafuu,” amesema.

Amesema hata wanavyokata rufaa ya kuenguliwa, wagombea wanapeleka malalamiko yao katika kamati za rufaa ambazo ni vile vile vyombo vilivyo chini ya Serikali ni tofauti na ubunge ambao kanuni na sheria zinatoa fursa kwa watu kwenda mahakamani wasiporidhika.

Hivi karibuni Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala ndogo ya Dar es Salaam imetupilia mbali shauri lililokuwa limefunguliwa na Watanzania watatu la kupinga Waziri wa Tamisemi kusimamia na kuratibu uchaguzi wa Serikali za mitaa 2024.

Alipoulizwa kuna chochote ambacho vyama vya upinzani vinatakiwa kujifunza, Dk Loisulie amesema wanachotakiwa kufanya ni kuendelea kupigania uwepo wa usawa kwa upande wa vyombo vya kusimamia uchaguzi na sheria.

“Kwa sababu inajulikana changamoto iko wapi. Sasa namna ya kutatua changamoto ndio wajifunze kuelekea kuitatua changamoto iliyopo (ya kutokuwa na chombo cha uchaguzi chenye usawa),” amesema Dk Loisulie.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT), Dk Ntuli Ponsian amesema hamna kitu kikubwa cha kufanyika ili kumaliza malalamiko ya kuenguliwa kwa wagombea, bali ni Watanzania kuamua kama wanataka kuijenga nchi ama kubomoa.

“… kuna vitu vingine vinatia aibu havihitaji watu waende shule, haihitaji watu wasome ni jambo la kawaida, kama tuliamua kuwa nchi ya vyama vingi, tutekeleze nchi tuliyoamua,” amesema.

Amesema kwa namna ambavyo mambo yanakwenda wanaweza kupanda chuki na kuwa itafika mahali watashindwa kuizima, hivyo kusababisha watu kushindwa kuishi pamoja.

Amesema kwa kufanya hivyo ni kitu ambacho watakuwa wamesababisha wenyewe kwa sababu uchaguzi wa serikali za mitaa ni uchaguzi wa watu wanaofahamiana wenyewe kwa kuwa wanaishi nao mitaani.

 “Hatuhitaji kutumia nguvu nyingi, nadhani hata watoto wa mitaani wanatushangaa watu hawa kwa umri wao wanaweza kufanya hivi. Hivi ni vitu vya aibu ambavyo haviwezi kufanywa na jamii ya kistaarabu ya leo,” amesema.

Amesema ukimweka kiongozi katika mtaa kwa kuwalazimisha watu (hawampendi) na utafanya kushindwa kuwaamrisha chochote watu anaowaongoza na hivyo ushiriki wa wananchi katika maendeleo ya jamii utakuwa ni mdogo.

“Jambo hili halina afya katika nchi yoyote, halimsaidii yeyote sanasana tunatengeneza jamii ambayo ni katili, isiyopendana wala kusaidiana, jamii itakayokuwa na chuki wasioweza kusaidiana,” amesema Dk Ponsian.