Wasomi waibua mpya Dk Slaa kurejea Chadema

Dar/Mbeya. Wakati Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kikitangaza kurejea kwa kada wake wa zamani, Dk Willibrod Slaa, wachambuzi wa siasa wameeleza kwamba msimamo na harakati za Dk Slaa zinaendana na uongozi wa sasa, hivyo watashirikiana kwa karibu kusukuma ajenda ya chama.

Dk Slaa ametangazwa kurejea Chadema leo Jumapili, Machi 23, 2025, wakati wa uzinduzi wa ziara ya chama hicho ya siku 48 jijini Mbeya, inayolenga kuelimisha umma kuhusu kaulimbiu ya “No Reform, No Election” (Bila Mabadiliko, Hakuna Uchaguzi).

Katika mkutano huo, uliohudhuriwa na viongozi waandamizi wa Chadema wakiongozwa na Mwenyekiti, Tundu Lissu, wameitambulisha kaulimbiu yao sambamba na kumpokea Dk Slaa, aliyewahi kuwa Katibu Mkuu na mgombea urais wa chama hicho kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Dk Slaa alijiondoa Chadema mwaka 2015 kwa kutokubaliana na uamuzi wa chama chake kilichoshirikiana na vyama vingine vilivyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kumsimamisha Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kama mgombea urais.

Kiongozi huyo alieleza kwamba anasimamia ukweli na dhamira yake ilimfanya ashindwe kumuunga mkono Lowassa, ambaye alikuwa akimtuhumu kwenye majukwaa kwa ufisadi.

Septemba 2015, aliondoka nchini kuelekea Marekani na baadaye Canada, alikokuwa akiishi na familia yake. Akiwa Canada, Novemba 17, 2017, Rais wa awamu ya tano, hayati John Magufuli, alimteua kuwa Balozi, akiiwakilisha Tanzania nchini Sweden.

Baada ya kumaliza muda wake wa miaka mitatu kama Balozi wa Sweden, mwaka 2021, Dk Slaa alirejea nchini. Hata hivyo, Septemba mosi, 2023, Rais Samia Suluhu Hassan alimvua hadhi ya ubalozi kutokana na kauli zake za kuikosoa Serikali hadharani.

Tangu alipoanza kuishi nchini, amekuwa mkosoaji mkubwa wa Serikali, akiungana na wanaharakati wengine, hususan katika sakata la mkataba wa uwekezaji katika Bandari ya Dar es Salaam kati ya Serikali na kampuni ya DP World, akishirikiana na Wakili Boniface Mwabukusi.

Wakati wote huo, Dk Slaa hakuwa na uhusiano wowote na viongozi wa Chadema, hasa mwenyekiti wa zamani, Freeman Mbowe, ambaye wakati wa kesi yake ya ugaidi, Dk Slaa alidai kuwa Mbowe ni gaidi na akashangaa kwa nini hajafungwa.

Vilevile, wakati wa kampeni za uchaguzi wa Chadema uliofanyika Januari 2025, Dk Slaa aliweka wazi kumuunga mkono Tundu Lissu, huku akieleza katika kipande cha sauti kilichosambaa mitandaoni kwamba kulikuwa na mpango wa Rais Samia Suluhu Hassan kumsaidia Mbowe kwenye uchaguzi huo, jambo lililosababisha akamatwe na kufikishwa mahakamani.

Wachambua kurejea kwake

Akizungumzia kurejea kwa Dk Slaa Chadema, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Conrad Masabo, amesema hakuondoka rasmi kwa sababu hakuwahi kujiunga na chama kingine.

Amesema kwa mujibu wa Dk Slaa, kilichomtoa ni ujio wa hayati Lowassa aliyeletwa na uongozi wa Chadema uliopita, na kwa sasa kuna uongozi mwingine, hivyo huenda mabadiliko hayo yanaendana na kiwango kikubwa cha siasa anazozitaka.

“Huyu hajarejea, bali amekuwa kama mwanachama ambaye hakuwa active, sikuwahi kusikia kama amejiunga na chama kingine. Kwa hiyo, huwezi kurejea kama hujaenda chama kingine,” amesema.

Dk Masabo amesema kwa muda mrefu, Dk Slaa amekuwa akifanya harakati ambazo kwa sasa zinafanana na mtazamo na mwelekeo mpya wa Chadema.

“Kadhia alizozipata, ikiwemo kunyang’anywa hadi pasipoti ya ubalozi, kukamatwa kwa tuhuma za uhaini na kuwekwa ndani kwa muda mrefu kwa mashtaka ambayo kisheria yanahitaji dhamana lakini akanyimwa.

“Kwa mtazamo wangu, ndiyo maana ameona ni wakati sahihi wa kuungana na wenzake wenye mrengo unaofanana kufanya siasa kutafuta mabadiliko,” amesema.

Akizungumzia ushawishi wake, amesema kwa kuwa ameshaingia, chama kinakuwa kimepata nguvu kazi na mshauri kwa kuwa ana uelewa wa muda mrefu.

Dk Slaa ni mzuri katika kupanga hoja na mikakati, hivyo ni mchango mkubwa kwenye chama na kitapata faida, na yeye atapata uwanja wa kufanyia siasa,” amesema Masabo.

Mchambuzi wa masuala ya siasa, Kiama Mwaimu, amesema Dk Slaa bado anakereketwa na suala la kutaka mabadiliko, ndiyo maana baada ya kuondoka kwa uongozi wa Chadema uliopita, ameamua kurejea

Amesema mchango wake mkubwa kwa sasa Chadema ni kuwa mshauri na hatarajii kuwa mgombea, bali atashauri nani agombee urais na mikakati itakuwaje katika kupambana na chama tawala kwa kuwa ana uzoefu wa muda mrefu.

“Atakuwa mshauri mkuu hasa kwenye kampeni na maneno yake siyo ya vurugu kwa kuwa ni mtu mzima na atapunguza hata makali ya baadhi ya maneno, atakuwa mshauri mkuu,” amesema.

Kwa upande wake, Mhadhiri Mwandamizi Mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Dk Azaveri Lwaitama, amesema kurejea kwake si jambo jipya kwani watu wanaoingia na kutoka kwenye chama ni jambo la kawaida. Hata hivyo, amesema kikubwa ni ajenda ya sasa ya Chadema.

“Ujumbe wa chama wa ‘No Reform, No Election’ ndiyo unaomvutia, ambao unataka mabadiliko kuelekea kwenye uchaguzi mkuu,” amesema.

Dk Lwaitama amesema kilichomuondoa Chadema kilikuwa ujio wa Lowassa, na sasa ameona ujio wa sera za Chadema ndiyo zimemrejesha.

Hakuwahi kurejesha kadi

Akizungumza wakati akimtambulisha Dk Slaa kwenye mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), Amani Golugwa, amesema Dk Slaa hakuwahi kurejesha kadi yake, licha ya mfarakano kati yake na chama wakati huo.

“Wakati anaondoka, kumbe hakuwahi kurejesha kadi yake. Kuna maneno-maneno tulikwazana, sasa wakati wa kurudi ilibidi tuitane ndani kuzungumza yale tuliyokwazana na sisi viongozi tumeyamaliza naye

“Tukasema tuihakiki kadi yake, tuiangalie, na tulipoikagua tukagundua kumbe kweli hakuirudisha, huyu mwanachama aitwaye Dk Wilbroad Slaa. Alitueleza anataka kurejea ili aihuishe.

“Kwa sababu tumemalizana naye na wakati anaondoka aliondoka mbele za watu, basi itabidi arudi hivyohivyo ili watu wamuone,” amesema Golugwa.

Lissu amwelezea Dk Slaa

Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, amesema Dk Slaa ndiye aliyempa kadi ya Chadema mwaka 2004.

Amesema katika kipindi chake wakati Lissu anaingia, Chadema ilikuwa na wabunge wachache lakini wakapanda hadi kufikia wabunge 117 wa Ukawa.

“Alikuwa katibu mkuu kwa muda mrefu kuliko mwingine yeyote wa chama chetu. Kipindi chake kilikuwa na mafanikio makubwa na aliondoka mwenyewe. Utaratibu wake kikatiba ni rahisi sana; angeweza kwenda kwenye mtandao akapata kadi na tusingesema ameingiaje, lakini ameona arejee kwa namna hii,” amesema Lissu.

Dk Slaa aomba radhi

Katika mkutano huo, baada ya kupanda jukwaani kuzungumza, Dk Slaa ametumia nafasi hiyo kuwaomba radhi wanachama wa chama hicho, huku akishukuru kurejea.

Amesema kama kulikuwa na mfarakano baina yake na chama, kwa sasa umeisha rasmi na ameomba kurejea upya kuanza mapambano ya kudai mabadiliko.

“Naomba msamaha na radhi kwa wanachama, mfarakano uliotokea kwa sasa umeisha rasmi. Nakuja kuanza upya mapambano, niko tayari kwa mabadiliko ambayo wengine hawataki,” amesema Dk Slaa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *