Wasomi na wanazuoni wa Afrika kujifungia Dar es Salaam kujadili uhuru wao wa kitaaluma

Dar es Salaam. Wasomi na wanazuoni takribani 200 kutoka nchi mbalimbali za Afrika wanatarajia kukutana kwa siku nne jijini Dar es Salaam kujadili uhuru wa wanataaluma na wanazuoni katika bara hilo.

Pia kuchambua na kutathmini umuhimu, umadhubuti, na uhalisia wa Azimio la Kampala 1991 na lile la Dar es Salaam mwaka 1990 yaliyolenga yaliyoweka  mfumo wa namna ya kulinda na kukuza haki na uhuru wa wanataaluma na wanazuoni wa Afrika, na Vyuo vya Elimu ya Juu.

Tathmini hiyo itajikita katika muktadha uliopo ambapo kumekuwa na mabadiliko kadha wa kadha tangu kupitishwa kwake.

Kongamano hilo ambalo limeandaliwa na Ndaki ya Sayansi za Jamii kwa ushirikiano na Kanseli ya Maedeleo ya Utafiti Katika Sayansi za Jamii (CODESRIA) litafanyika kuanzia Aprili 29, 2025 hadi Mei 02, 2025 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM)

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mhadhiri Mwandamizi wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM), Dk Ng’wanza Kamata amesema kongamano hilo ambalo linafanyika kwa mara ya tatu limekuja wakati ambao kumekuwa na mwelekeo wa kutishia, kubana, na kuminya uhuru wa wanataaluma, wanazuoni barani Afrika.

Aidha Uhuru wa vyuo vya elimu ya juu nao umekuwa ukiendelea kupungua.

“Hali hii inatokea ikiwa ni zaidi ya miongo mitatu tokea kupitishwa kwa Azimio la Dar es Salaam Juu ya Uhuru wa Wanataaluma na Wajibu wao Katika Jamii na Azimio la Kampala Juu ya Uhuru wa Wanazuoni na wajibu wao katika jamii ambayo “

“Kongamano hili linalenga kuchambua na kutathmini umuhimu, umadhubuti, na uhalisia wa Azimio la Kampala katika muktadha uliopo ambapo kumekuwa na mabadiriko kadha wa kadha tangu kupitishwa kwake”amesema.

Ameeleza  kuwa kutokana na tathmini hiyo mkutano utaangalia haja ya kuhuisha Azimio la Kampala kwa kulifanyia marekebisho kidogo, ili likidhi mahitaji ya sasa ya kutetea, kukuza, na kulinda, Uhuru wa Wanataaluma na Wanazuoni.

“Hiyo ni sehemu ya madai yanayoendelea kote barani Afrika ya kukuza haki na demokrasia kama nyenzo muhimu ya kuleta mabadiliko ya kisiasa, kijamii, na kiuchumi yenye masilahi kwa ustawi wa walio wengi”amesema.

Ameongeza kuwa wanataaluma 100 watakaohudhuria kongamano hilo watatoka Tanzania na 100 wengine watatoka katika mataifa mbalimbali ya Afrika.

Kwa upande wake Mhadhiri Mwandamizi wa Idara ya Sosholojia na Athropojia UDSM, Dk Richard Sambaiga amesema katika siku hizo nne kutakuwa na mijadala ya kitaaluma kujadili mada takribani 80 zitakazowasilishwa katika Vikao (Sessions) na Majopo (Panel).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *