Dar es Salaam. Wakati Shirika la Viwango Tanzania (TBS) likisema bado lipo katika uchunguzi wa mafuta ya kula yanayodaiwa kuwaathiri wakazi zaidi ya 200 wa Yombo Dovya, jijini Dar es Salaam, wakazi hao wameendelea kuwa na wasiwasi kuhusu afya zao kwa kuwa baadhi yao bado wanaumwa hadi sasa.
Wananchi hao wanapaza sauti zao ikiwa zimepita siku 28 tangu TBS waingie katika uchunguzi wa mafuta hayo ili kubaini kama kweli ndio yaliyoleta athari kwa wananchi.
Taarifa zinaeleza kuwa wananchi hao walipata athari za kiafya baada ya kutumia chakula kilichoandaliwa kwa kutumia mafuta hayo, waliyodaia wameyanunua kwa mfanyabiashara wa duka mtaani kwao.

Alivyokuwa mmoja wa waathirika waliokula mafuta mwezi Januari, mwaka huu baada ya kuripotiwa kwa tukio hilo. Picha na Nasra Abdallah
Athari hizo zilianza kujitokeza siku nane baada ya kula mafuta hayo, ambapo wengi waliumwa tumbo, kuharisha, kuvimba uso, macho kuwasha na kuwa mekundu, kutokwa na vipele, na ngozi kubabuka.
Baadhi yao walikwenda vituo vya afya vya karibu kupata matibabu, na kadri idadi ya waathirika ilivyozidi kuongezeka, waliripoti suala hilo kwa ofisi ya serikali za mitaa, ambayo nayo iliwasiliana na mamlaka husika, zikiwemo halmashauri, TBS na Jeshi la Polisi, kwa ajili ya kuchukua sampuli za mafuta hayo kwa uchunguzi zaidi.
Januari 17, 2024, TBS katika taarifa yake kwa umma, iliyosainiwa na Kaimu Meneja Uhusiano na Masoko wa Shirika hilo, Deborah Haule, ilisema: “TBS imefanya ukaguzi ambapo shehena ya madumu ya mafuta yaliyokutwa kwa msambazaji wa bidhaa husika, iliondolewa mara moja na sampuli kuchukuliwa kwa ajili ya uchunguzi wa kina wa kimaabara kwa kushirikiana na mamlaka nyingine.”
Mwananchi Digital ilitaka kujua uchunguzi huo umefikia wapi hadi sasa baada ya kuwepo ukimya, ambapo Ofisa Habari wa TBS, Gladness Kaseka amesema bado haujakamilika, ukikamilika watautaarifu umma.

“Kwa sasa bado tunaendelea na uchunguzi, tunaomba wananchi wavute subira, kwani ukikamilika tutatoa hadharani tulichokibaini kama tulivyowataarifu wakati tunaingia katika uchunguzi,” amesema Gladness.
Wananchi wajawa hofu
Kwa upande wao, baadhi ya wananchi waliopata athari, akiwemo Mwakani Mgombeka, wamesema bado wanakabiliwa na matatizo ya kiafya.
“Kiukweli kuchelewa kutolewa kwa majibu ya uchunguzi wa Serikali kunatuogopesha kuwa huenda tukazidi kuathirika zaidi. Kichwa changu kilikuwa kinaniuma sana, sasa huniuma mara mojamoja nyakati za usiku, hivyo tunaomba wataalamu wetu waharakishe katika hili kabla hatujapata madhara makubwa zaidi,” amesema Mgombeka.
Naye Razaki Shafii, mwenye umri wa miaka 20, amesema bado anasikia maumivu ya macho hadi sasa, jambo linalomfanya kuwa na wasiwasi kwani hajui hasa nini kimemsababishia hali hiyo.

Alivyokuwa mmoja wa waathirika waliokula mafuta mwezi Januari, mwaka huu baada ya kuripotiwa kwa tukio hilo. Picha na Nasra Abdallah
“Hivi sasa ninaona kwa tabu sana, hasa jicho moja limepoteza uoni kabisa, na mbaya zaidi nilipata kutibiwa mara tatu Hospitali ya Temeke, lakini sasa hivi natakiwa kujigharamia baada ya kuambiwa muda wa kuhudumiwa bure umeisha. Nimeshindwa kwa kuwa mama yangu hana uwezo,” amesema Shafii.
Ameeleza kuwa baada ya kusitishiwa matibabu, alitakiwa kwenda kuomba barua kutoka kwa serikali ya mtaa ili kuendelea kupatiwa matibabu kwa njia ya msamaha, lakini tangu amwambie mwenyekiti wa mtaa hajaweza kupata majibu yoyote.
Mwenyekiti wa Mtaa huo, Denisi Moyo amekiri kupokea taarifa hiyo kupitia kwa mama yake Razaki, Niweje Said, na kuwa alizungumza na mtendaji ili kumpatia barua hiyo, lakini hajajua imekwama wapi na ameahidi kufuatilia.
“Ninakiri taarifa za Razaki ninazo, kwani wagonjwa wote waliotakiwa kupata matibabu tuliwaandikia barua za msamaha, na hata Razaki alipokuwa akipata usumbufu nilikuwa nikitumia njia ya kupiga simu hospitalini ili aweze kutibiwa,” amesema Moyo.
Hata hivyo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Temeke, Joseph Kimaro amesema hana taarifa ya mgonjwa huyo kushindwa kuendelea kupata huduma na kumtaka afike hospitalini hapo Jumatatu, Februari 16, 2025.
Kimaro, ambaye amekiri kuwa hospitali hiyo iliwapokea waathirika saba na kuwapatia matibabu, amesema hali zao zinaendelea vizuri, na ameahidi kufuatilia kujua kwa nini Razaki amesitishiwa matibabu, kwa kuwa lengo lao ni kutoa huduma bila kujali changamoto walizonazo wagonjwa.

Alivyokuwa mmoja wa waathirika waliokula mafuta mwezi Januari, mwaka huu baada ya kuripotiwa kwa tukio hilo. Picha na Nasra Abdallah
Hata hivyo, amesema barua ya serikali ya mtaa kuhusu msamaha wa matibabu ni muhimu kwa sababu wao wanatunza kumbukumbu kwa ajili ya ukaguzi wa mahesabu ya matumizi ya hospitali.
Mfanyabiashara wa mafuta aeleza
Mfanyabiashara wa mafuta ya jumla, Masoud Ally, ambaye mafuta yake yanadaiwa kununuliwa dukani kwake, amesema ameruhusiwa kuendelea na biashara, ingawa anatakiwa kuripoti kila wiki katika Kituo cha Polisi Chang’ombe.
Amesema ametakiwa kuwa makini na bidhaa hiyo kwa kuhifadhi nyaraka zote za manunuzi, na hata yeye ana hamu ya kuona ripoti ya uchunguzi huo inatolewa ili wateja wake waendelee kuwa na imani na bidhaa zao.
Masoud amekiri kuwa tukio hilo limemuathiri kibiashara, lakini anashukuru kuwa wao wamekuwa wakielewa wanapopewa ufafanuzi kuhusu hatua zinazochukuliwa na mamlaka husika.