WASIRA- CCM HAITAKUWA NA NAMNA YA KUWASAIDIA WABUNGE WALIOSHINDWA KUFANYA VIZURI KATIKA MAJIMBO YAO

 

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Stephen Wasira, akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa CCM Mjini Tabora, akiwa katika ziara ya kukagua uhai wa Chama, utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi na kusikiliza kero za wananchi. 

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Stephen Wasira, akizungumza na viongozi wa vyama vya ushirika vya mkoa wa Tabora kusikiliza changamoto za wakulima hususan wa tumbaku wa mkoa huo, akiwa katika ziara ya kukagua uhai wa Chama, utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi na kusikiliza kero za wananchi. 

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Stephen Wasira, akizungumza jana na wananchi katika eneo ambalo ulifanyika mkutano wa hadhara mwaka 1958 ulioongozwa na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere baada ya kupitisha azimio la TANU kushiriki uchaguzi wa kura tatu ambao ulikuwa hatua muhimu iliyofanikisha Uhuru wa Tanganyika (Tanzania Bara) mwaka 1961. Wasira amehitimisha ziara ya kukagua uhai wa Chama, utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi na kusikiliza kero za wananchi mkoani Tabora,

Na Mwandishi Wetu, Tabora

 
WAKATI Bunge likitarajiwa kuvunjwa Juni 27, mwaka huu, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema wabunge ambao hawakufanya vizuri katika majimbo yao wala kurudi kwa wananchi watambue Chama hakitakuwa na namna ya kuwasaidia kwa sababu walipewa nafasi wakashindwa kuzitumia.
 
Kimesisitiza katika kuhakikisha CCM inapata wagombea ubunge na udiwani wanaokubalika kwa wananchi kimeamua kubadilisha utaratibu wake wa kupata wagombea katika nafasi hizo ili kuhakikisha wananchi wanawapiga kura Chama hicho na hatimaye kushinda Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba mwaka huu.
 
Akizungumza jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Tabora alipokuwa akihitimisha ziara yake katika Mkoa huo, Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Stephen Wasira alisema Chama kimebadilisha mfumo katika kupata wagombea udiwani na ubunge kwa kupanua wigo wa demokrasia kwa kuongeza idadi ya wapiga kura.
 
“Tunataka kazi yetu iwe rahisi maana tunataka mgombea ubunge mwenzetu ambaye pia akienda kwa wananchi ni mwenzao kwa sababu hawezi kusahau kurudi kwa wenzake.
 
“Kwa hiyo kama mtu ulifanya vizuri huwezi kuwaambia wananchi ulikuwepo. Ulikuwepo sawa lakini kama maoni hayaendi sawa utatusamehe maana tunataka yule ambaye alifanya vizuri, kama hukufanya vizuri sasa tutakusaidiaje?.
 
“Maana CCM tulikupeleka na kuchaguliwa lakini baada ya kuchaguliwa ukapotea. Umefika wakati wa uchaguzi unasema nimerudi nyumbani, ulikuwa umeenda wapi? Na kama kweli ulisafiri kwa nini hukuwaaga waajiri wako,” amesema Wasira.
 
Akieleza zaidi Wasira amesema ukweli ni kwamba uchaguzi wa wabunge utakuwepo na umeshafika na mkutano Mkuu Maalum wa CCM uliweka utaratibu wa kupata wagombea kwa sababu Chama lazıma kiwe kinafanya mabadiliko kulingana na wakati.
 
Amesema wamefanya mabadiliko katika uteuzi na kwamba itakapofika Juni 28, na Julai 5 mwaka huu watakuwa wameshajua nani anagombea na kuongeza wanajua sasa kuna watu wanajipitisha kaika majimbo na kata.
 
“Sasa hivi tunajua wako wanapita pita tunawafahamu na tunawafuatilia mwenendo wao na hatufuatilii waliopo bali hata wa zamanı maana kuna mambo hatuyapendi sana lakini itakapofika wakati huo tutajua.
 
“Siku hizi hakuna kupita bila kupingwa sheria imekataa, kwa hiyo hata ukifanya kuzuia wengine unapoteza muda acha waje kama ni 10 au 20. Sio kwamba tunamkoa mtu hata kidogo.
 
“Tunataka watu wengi wapige kura ya maoni watuambie kwa maoni yao nani anafaa kuwa wa kwanza, wa pili na wa tatu maana huwezi kununua watu 13,000 na ukiwanunua utakufa kabla hujawalipa wote, hutaweza maana zamanı walikuwa wako wachache,” amesema Wasira.
 
Wasira amesisitiza kuwa, wametaka watu wengi na hasa watu ambao wako karibu sana na wananchi ndio wapige kura ya maoni ili wakija katika uchaguzi wa mwisho mmoja akipitishwa wananchi waseme “kama ni huyo sawa sawa” sio Chama kikipeleka mgombea wananchi wahoji huyu wamemtoa) wapi.
 
CCM TUNAHUBIRI AMANI, HAKI
 
Akizungumza kuhusu amani ,Wasira amesema ni vema wananchi wakafahamu kuwa katika amani ndani yake kuna haki, hivyo Chama kitaendelea kuihubiri kuhakikisha inapatikana haki.
 
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Mjini Dodoma Wasira amesema kuna watu wanahoji CCM inazungumzia sana amani lakini haizungumzii haki, huku akibainisha kuwa wanaotoa madai hayo ni watu wazito.
 
“Sasa nikasema ngoja niende (Tabora) kwenye kitovu ambapo Mwalimu Julius Nyerere alitoa machozi kwa ajili ya amani, tuwasaidie kuelewa kwamba ukizungumza amani ndani ya amani kuna haki kwa sababu amani ikikosekana wenye uwezo mdogo wanaumia.
 
“Amani ikikosekana wanawake na watoto wao katika nchi jirani wanakilimbilia Tabora…ukilinda amani unalinda haki tena unalinda haki ya wanyonge, unalinda haki ya wasiokuwa na sauti.
 
“Unazungumza haki ya mtu anasema anataka kuwa Rais halafu anaambiwa eti tukibadili Katiba anakuwa Rais na haki inayosemwa ni mtu mmoja badala ya kuzungumza haki ya walio wengi. Tunauliza huyo anayesema hatuzungumzi haki tunazungumza amani sijui anadhani ndani ya amani hakuna haki.” Amesema Wasira.
 
Ameongeza kuwa kote ambako amani imekosekana haki ya wengi imepotea hususan nchi za jirani wananchi wake walikimbilia Tanzania, hivyo alihoji iwapo ikitokea amani iliyopo kukumbwa na dhoruba Watanzania watakimbilia wapi
 
“Wenyewe wamekimbia kwao na ninyi mnataka kukimbilia kwao mnapishana kama sisimizi. Hivyo tunasisitiza haki lakini haki iko ndani ya amani. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka vyombo na inasema kazi ya Bunge ni kutunga sheria, kazi ya Mahakama ni kutafsiri sheria na kuweka haki na haki hiyo ni haki ya kibinadamu, hatuzungumzi haki ya Mungu.
 
“Tumeweka mahakama kwamba ndio inayolinda haki za watu, sasa kama wewe unadhani hupewi haki uende kwenye mahakama ukadai hiyo haki yako usikilizwe ili ulete amani na upate haki yako kwa njia ya amani 
 
“Unatuambia utakinukisha, unatuambia utaichoma Tanzania nani anakupa leseni ya kuichoma Tanzania? Kwa idhini ya nani? Ndio maana tunawaambia wale wanaotaka kutumia nguvu tutawaambia hiyo sio njia halali unataka kuvunja haki ya wanyonge wa Watanzania
 
“Unataka kutengeneza matatizo yatakayofanya akinamama wakimbie kliniki na kliniki tulizowajengea zibomolewe kwa mabomu, hivyo hatuwezi kukubali hilo. Nawashangaa Watanzania ambao hawajaelewa na wakiwasikiliza wanawapigia makofi lakini hawajui gharama zake,” amesema Wasira.
 
Hivyo amewaambia wananchi kuwa ameamua kuwachochea Watanzania kupitia Tabora ambako ni chimbuko la amani iliyowekwa nchini kwa machozi ya Julius Nyerere kwamba amani hiyo lazima itadumu kwa gharama yoyote.
 
“Hatuwezi kuruhusu watu wachache au kikundi kinachotumwa na vibaraka na Wakoloni mambo leo kuja kuvuruga amani ya nchi yetu, hatutafanya hivyo. Narudia kuna amani na ndani ya amani kuna haki.

The post WASIRA- CCM HAITAKUWA NA NAMNA YA KUWASAIDIA WABUNGE WALIOSHINDWA KUFANYA VIZURI KATIKA MAJIMBO YAO appeared first on Mzalendo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *