Wasira: CCM haina namna ya kuwasaidia wabunge wazembe

Tabora. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimesema hakitakuwa na namna ya kuwasaidia wabunge wake waliopewa nafasi ya kuwawakilisha wananchi, lakini wakashindwa kuitendea haki.

Kimesema msimamo wake kwa sasa ni kupata wagombea wanaokubalika na wananchi, ndiyo maana kimebadili utaratibu wa kura za maoni na mchujo.

Katika mchakato wa kura za maoni, chama hicho kwa sasa kimeongeza wajumbe watakaoshiriki kupiga kura hizo, huku kikiweka utaratibu wa mchujo wa wagombea.

Kupitia utaratibu huo mpya, si kila mgombea atafika mbele ya wajumbe kupigiwa kura za maoni, bali watachujwa watatu na ndiyo watakaopigiwa kura hizo.

Hayo yameelezwa jana na Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira alipohutubia mkutano wa hadhara katika ziara yake mkoani Tabora.

“Tunataka kazi yetu iwe rahisi, tunataka mgombea ubunge mwenzetu ambaye pia akienda kwa wananchi ni mwenzao kwa sababu hawezi kusahau kurudi kwa wenzake,” amesema.

Amesema kama mbunge alifanya vizuri, hatakuwa na sababu ya kuwaaminisha wananchi kuwa alikuwepo kwenye nafasi hiyo kwa sababu watakuwa wanamjua.

“Mtu aliyefanya vizuri huwezi kuwaambia wananchi ulikuwepo. Ulikuwepo sawa, lakini kama maoni hayaendi sawa utatusamehe, maana tunataka yule ambaye alifanya vizuri. Kama hukufanya vizuri sasa tutakusaidiaje?

“Maana CCM tulikupeleka na kuchaguliwa, lakini baada ya kuchaguliwa ukapotea. Umefika wakati wa uchaguzi unasema ‘nimerudi nyumbani’, ulienda wapi? Na kama kweli ulisafiri kwa nini hukuwaaga waajiri wako?” amehoji Wasira.

Amesema wamefanya mabadiliko katika uteuzi na kwamba itakapofika Juni 28 hadi Julai 5 mwaka huu, watakuwa wameshajua nani anagombea.

“Sasa hivi tunajua wako wanapitapita, tunawafahamu na tunawafuatilia mwenendo wao. Hatufuatilii waliopo tu bali hata wa zamani, maana kuna mambo hatuyapendi sana lakini itakapofika wakati huo tutajua.

“Siku hizi hakuna kupita bila kupingwa, sheria imekataa. Kwa hiyo hata ukifanya kuzuia wengine unapoteza muda, acha waje kama ni 10 au 20. Sio kwamba tunamkataa mtu, hata kidogo,” amesema.

Amesema chama hicho kinataka watu wengi washiriki kupiga kura kwa kuwa haitawezekana kuwanunua zaidi ya watu 13,000.

“Ukiwanunua utakufa kabla hujawalipa wote, hutaweza maana zamani walikuwa wachache,” amesema.

Wasira amesisitiza kuwa wameamua watu wengi wapige kura ya maoni ili wakija katika uchaguzi wa mwisho, mmoja akipitishwa wananchi waridhike.

Katika hatua nyingine, amesema chama hicho kitaendelea kuhubiri amani na kuhakikisha inapatikana.

 “Sasa nikasema ngoja niende (Tabora), kwenye kitovu ambapo Mwalimu Julius Nyerere alitoa machozi kwa ajili ya amani, tuwasaidie kuelewa kwamba ukizungumza amani, ndani ya amani kuna haki.

“Amani ikikosekana, wanawake na watoto wao katika nchi jirani wanakimbilia Tabora…

Ukilinda amani unalinda haki, tena unalinda haki ya wanyonge, unalinda haki ya wasiokuwa na sauti,” amesema.

Amesema wapo wanaozungumzia haki wakimaanisha kubadili Katiba, wakiamini ndiyo itakayowapa nafasi ya kushinda wadhifa wa urais.

Amesema inapozungumzwa haki, isitazamwe inayodaiwa na mtu mmoja, bali yaangaliwe maslahi ya wengi.

“Unatuambia utakinukisha, unatuambia utaichoma Tanzania. Nani anakupa leseni ya kuichoma Tanzania? Kwa idhini ya nani?

Ndiyo maana tunawaambia wale wanaotaka kutumia nguvu, tutawaambia hiyo siyo njia halali. Unataka kuvunja haki ya wanyonge wa Watanzania,” amesema.

Amesema wanachosema hao wanaojiita wadai haki ni kutaka kuharibu amani na kusababisha uwekezaji wote uliofanywa nchini uharibike.

“Hatuwezi kuruhusu watu wachache au kikundi kinachotumwa na vibaraka na wakoloni mambo leo kuja kuvuruga amani ya nchi yetu. Hatutafanya hivyo. Narudia, kuna amani na ndani ya amani kuna haki,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *