Wasira: CCM haina chuki, visasi bali inaamini katika maridhiano

Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira amewahakikishia Watanzania kwamba chama hicho hakina chuki wala kısası na mtu, bali kinaamini katika kutekeleza sera ya maridhiano.

Wasira ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Aprili 17, 2025 wilayani Urambo mkoani Tabora, alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara. Wasira anaendelea na ziara yake ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi, kuzungumza na viongozi wa CCM na kusikiliza kero za wananchi.

Amesema CCM inaamini katika maridhiano ambayo pia ni sera ya Serikali inayoongozwa na  Rais Samia Suluhu Hassan, ndio maana hata waliokimbia nchi ni maridhiano ndiyo yaliwarudisha nchini.

“Niwasaidie tu kuwaelimisha kwamba, mkiwa na sera ya maridhiano haiwi mbadala wa sheria na wala huwezi kusema kwa sababu wewe ni mwenyekiti basi upo juu ya sheria.

“Wote tuko chini ya sheria hata mimi nikiamka sasa hivi nikakupiga kofi, Jeshi la Polisi watanikamata, hawawezi kusema wewe ni Makamu Mwenyekiti wa CCM maana umakamu haunipi uhuru wa kupiga watu makofi halafu nikaondoka salama,” amesema Wasira.

Amesisitiza; “CCM haina visasi na mtu, lakini atakayekosea hukamatwa na polisi kwa kuwa wamesomeshwa kukamata, vilevile wamesomeshwa kusema hili ni kosa, “sio kila anayekamatwa huwa polisi wametumwa, sio kweli.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *