Kishapu. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira amewavaa wabunge wa viti maalumu akiwataka waache kuwahonga wanawake kwa kuwagawia majiko ya gesi na vitenge ili wapate uongozi.
Amesisitiza kwamba chama hicho kimedhamiria kujenga maadili katika kupata viongozi watakaokwenda kuwatumikia wananchi.
Wasira amebainisha hayo leo Machi 27, 2025 wakati akizungumza kwenye mkutano wa ndani na wanachama wa chama hicho Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa ilani ya chama hicho.
Amesema anajua wabunge hao wanachaguliwa na watu wachache lakini lazima wajue rushwa ni adui wa haki na amesisitiza kwamba wanataka wananchi wawe na mamlaka na Bunge.

“Akina mama wa viti maalumu muache kugawa mitungi ya gesi na vitenge, mitungi yenyewe mnawapa akina mama gesi, ikiisha inageuzwa kuwa ‘furniture’, wanakalia, maana hata hela ya kununulia gesi hawana, haya ndiyo mambo yanayoitwa maadili?
“Sasa wapigakura wameongezeka, vitenge hivyo mtanunua hadi vitaisha madukani, acha mambo ya vitenge, acha mambo ya majiko nendeni kwa kina mama hawa, watendeeni haki,” amesema Wasira na kuongeza:
“Wabunge wa viti maalumu, acha niwaambie ukweli, sificha mambo kwa sababu mnachaguliwa na watu wachache kwa muda wa miaka mitano, kazi yenu kushughulika na wajumbe, hamuendi kwa kina mama wenyewe walioko chini. Kila siku mnacheza na wajumbe tu…mkija wilayani wajumbe, wajumbe walikuchagua ili utumikie wote,” amesema.
Akijenga hoja hiyo huku akishangiliwa na wanachama wa chama hicho, Wasira amesema kuna mtu mmoja ambaye hakumtaja jina, aliwahi kuwapeleka wajumbe Zanzibar baada ya kubaini gharama ilikuwa kubwa, akawarudisha.
“Tunataka viongozi ambao kweli wakienda bungeni, wawe wametumwa na wananchi na watasema mambo waliyowatuma, tunataka wananchi wawe na mamlaka na Bunge kwamba tumepeleka mtu kwa hiyari yetu akina mama viti maalumu acheni kugawa gesi na vitenge,” amesema Wasira.
Wasira amesema rushwa inapofusha wajumbe, chama kinataka kamati za siasa kuleta wagombea wenye sifa na wasibabaike kuwawajibika makada wenye kutaka kugawa fedha ili wachaguliwe kuwa viongozi.
“Tumesema katika ahadi yetu tutasema ukweli daima, rushwa ni adui ya haki na mkono unanyoosha juu, sitapokea wala kutoa, ukishusha tu unapokea ahadi yako inakomea hewani maana yake unaachana na Mungu unapokea rushwa,” amesema.
Awali, akizungumza kwenye mkutano huo, Mbunge wa Kishapu (CCM), Boniphace Butondo amewasilisha kilio kwa Wasira baadhi ya vijiji katika jimbo hilo vinakabiliwa na uhaba wa maji licha ya kupitiwa na bomba linalosafirisha maji kutoka Ziwa Victoria.
Akijibu kilio hicho katika mkutano huo uliofanyika Kishapu, eneo la Maganzo, Wasira ameanza kusema kwa kudai wakati mradi huo wa kusafirisha maji unaanza, walikubaliana kila kijiji kinachopitiwa lazima waachiwe maji.
“Kwa kuwa kuna malalamiko haya kutoka kwa wananchi, namuachia Mkuu wa Mkoa kufuatilia changamoto hii na kuipatia ufumbuzi ili wananchi wapate maji kama tulivyokubaliana,” amesema Wasira.
Katika mkutano huo, mkazi wa eneo hilo, Mussa Charles aliuliza swali kuhusu hatima ya ubovu wa barabara inayotoka Kolandoto hadi makao makuu ya wilaya hiyo.

Akijibu swali hilo, Wasira amesema makao makuu ya wilaya lazima yafikike kirahisi hasa wananchi wanapohitaji kwenda kufanya shughuli mbalimbali.
“Kutokana na umuhimu wake, barabara hii tunaenda kuiweka kwenye ilani ya uchaguzi na kwa kuwa mwenyewe ni mjumbe wa kamati ya kuandaa ilani, nimelichukua nitalifanyia kazi ili ijengwe kwa kiwango cha lami,” amesema.
Mwananchi huyo amesema barabara hiyo imekuwa kero kwa wananchi hususani wanapokuwa na wagonjwa kuwapeleka hospitali ya Wilaya.
“Barabara ina mashimo mengi kiasi kwamba hadi unafika hospitali mgonjwa tatizo lake linakuwa limeongezeka. Mgeni akija mwenyeji anapona sasa umekuja tunaomba msaada wako kuipatia ufumbuzi barabara hii,” amesema Mussa.