Dodoma. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira amesema Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, imeleta mageuzi makubwa katika eneo la utawala, huku akisisitiza kuwa mchakato wa mageuzi (‘reform’) ni endelevu na si wa muda mfupi.
Akizungumza na wanachama wa CCM jana jioni, Aprili 23, 2025, akiwa katika Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, Wasira alisema hakuna sheria itakayotungwa na kukubalika na watu wote kwa wakati mmoja.
Hivyo amesisitiza kuwa mabadiliko ni jambo la kawaida na la lazima katika jamii yoyote ile huku akisema hakuna ‘reform’ inayokataliwa kabisa, hata yale yaliyokwishafanyika yanaweza kubadilika kadri muda unavyosonga.
Kuhusu hoja ya baadhi ya watu wanaotaka uchaguzi uahirishwe hadi mabadiliko yafanyike, Wasira amesema Katiba iko wazi na inasema; uchaguzi hauwezi kuahirishwa isipokuwa kama nchi itakuwa imekumbwa na vita.
Wasira amesema kwa sasa hakuna vita na kuongeza;
“Hivyo uchaguzi utaendelea. Sio kwamba tunapuuza mawazo ya watu, tutazidi kujadiliana kuhusu mambo muhimu ya taifa letu. Tunashukuru sana nchi ipo katika hali ya utulivu, viongozi wetu wa kiroho wametushauri vizuri na wametutia moyo. Wametuhimiza uchaguzi uendelee lakini kwa amani,” amesema Wasira.

Makamu Mwenyekiti huyo amesema CCM ni chama kinachojali amani, jambo linalochangia kuwepo kwa utulivu wa taifa kwa zaidi ya miaka 60 sasa.
Hali hiyo inawapa fahari kwa sababu wana ushahidi wa uwezo wao wa kudumisha amani.
Amefafanua kuwa baadhi ya watu hudhani haki haipatikani ndani ya amani, lakini ukweli ni kwamba haki hujengwa na kulindwa kupitia mazingira ya amani.
Amesema amani ikitoweka, haki za watu hasa wanyonge kama wanawake, watoto na watu wenye ulemavu, huwa hatarini zaidi.
“Amani ni lazima. Wapo wanaosema wanataka haki, lakini sisi tunasema ndani ya amani ndiko haki ilipo. Ukiiondoa amani, watu wengi wataathirika – si mtu mmoja. Ushahidi upo, kwani tumepokea maelfu ya wakimbizi kutoka nchi jirani ambako amani ilivurugika,” amesema.
Kuhusu uzalishaji
Wasira pia aligusia suala la uzalishaji wa chakula, akibainisha kuwa baada ya uchaguzi na kuanzishwa kwa ilani mpya, kipaumbele kitaelekezwa kwa wakulima wa vijijini ili kupambana na umasikini.
“Umasikini unaweza kuondoshwa kwa kusaidia watu wa vijijini kupata fursa za uwekezaji. Programu ya Building a Better Tomorrow (BBT), iwapo itafika kila mkoa na kuwanufaisha wananchi wote, itabadilisha maisha yao,” alisema.
Aliipongeza Serikali kwa juhudi katika sekta ya umwagiliaji huku akisema changamoto kubwa ilikuwa ukosefu wa mfumo wa kudumu wa kusimamia umwagiliaji.

“Nchi kama Vietnam imekuwa kinara wa uzalishaji wa mazao kwa sababu ya mfumo mzuri wa umwagiliaji. Tukisambaza umwagiliaji Dodoma, kwa mfano, italeta mapinduzi kwa sababu mvua hapa si za kutegemewa. Tukitumia maji ya mvua kujenga mabwawa na kutumia matrekta badala ya jembe la mkono ambalo ni chanzo cha umasikini, tutaona mafanikio makubwa,” alisema.
Aliongeza kuwa vijana wengi siku hizi hawawezi tena kutegemewa kulima kwa kutumia jembe la mkono, hivyo katika ilani ijayo ya CCM, wataangalia namna ya kuweka mfumo wa matumizi ya matrekta ambayo ni mbadala wa jembe la mkono.
Akizungumza awali, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Adam Kimbisa alimwahakikishia Wasira kuwa chama hicho kimejipanga vyema kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025.
“Tunataka kukuhakikishia kuwa wananchi bado wanakiunga mkono Chama chetu. Kwa hiyo, kama uongozi wa mkoa tumejipanga kuhakikisha tunapata ushindi mkubwa kuanzia nafasi ya urais, ubunge hadi udiwani,” alisema Kimbisa.