Wasira ang’aka ataka watu wajadili hoja, wasimjadili yeye

Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira, amewasihi Watanzania kujikita katika kujadili hoja anazotoa anapotekeleza majukumu yake badala ya kuzungumzia masuala yake binafsi.

Ingawa hakufafanua kwa kina aina ya habari alizorejelea, kauli yake inaonekana kuwa huo ni ujumbe unaowalenga baadhi ya watu, wakiwamo viongozi wa vyama vya upinzani, wanaohoji uteuzi wake katika nafasi hiyo licha ya kuwa na umri mkubwa wa miaka 80.

Na baadhi yao wanahoji mchango wake mpya katika uongozi, huku wengine wakijadili muda wake mrefu katika nafasi za uwakilishi tangu Serikali ya Awamu ya Kwanza ya Rais Julius Nyerere, wakitaka apumzike na kutoa nafasi kwa vijana.

Wasira ambaye amewahi kuwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika katika Serikali ya Awamu ya Nne, ameyasema hayo leo Alhamisi Februari 13, 2025 katika mahojiano na kituo cha redio cha Clouds FM kwenye kipindi cha Power Breakfast.

Chimbuko la kauli za Wasira kilichochewa na swali kutoka kwa msikilizaji wa kipindi hicho, Sam Odera, ambaye alitaka kujua kama Wasira ana jipya kwa kuwa amekuwa katika siasa tangu enzi za TANU.

Swali hilo lilisomwa moja kwa moja na mtangazaji aliyekuwa akiendesha mahojiano hayo.

Katika ufafanuzi wake, Wasira amejibu kuwa; “Mimi sina jipya, labda yeye hana jipya. Nimekaa siku ngapi hajasikia jipya? Upya siyo kwamba kuna mambo yanayozuka ghafla kutoka hewani, bali ni jinsi mtu anavyojiweka na kutumia akili yake katika mazingira mapya.”

Ameendelea kusisitiza kuwa badala ya watu kumjadili yeye binafsi, wanapaswa kujadili hoja zake.

“Watu wajadili hoja ninazotoa, lakini sasa wengine badala ya kuzungumza hoja wananizungumzia mimi. Waache kuzungumzia habari zangu binafsi, wazungumzie hoja, waangalie ujumbe (message) na si mjumbe (messenger),” amesema Wasira.

Miongoni mwa waliomkosoa Wasira pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Bara, John Heche, ambaye anasema mbunge huyo wa zamani wa Bunda anapaswa kupumzika kutokana na umri wake alionao wa miaka 80.

Mwingine ni Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, katika mkutano wake na wanahabari jana Jumatano Februari 12, 2025, alisema Wasira hana jipya kwa kuwa amekaa madarakani kwa muda mrefu.

“Anataka mdahalo na mimi, nimesikia ana umri wa miaka 80. Mimi nilianza siasa nikiwa na miaka miwili, sasa nina miaka 57, lakini yeye bado yupo tu. Alikuwepo tangu enzi za chama kimoja cha Mwalimu Nyerere, akaja (Ally Hassan) Mwinyi, Kikwete (Jakaya), Magufuli (John), sasa tupo na Samia (Suluhu Hassan), naye bado yupo.

“Mzee wa miaka 80 ana kipi kipya cha mimi kufanya naye mdahalo? Ili iweje? Ili atuambie nini ambacho hatujakisikia katika hii miaka 55 aliyokuwemo?” alisema Lissu.

Aisifia CCM

Katika mahojiano hayo, Wasira amesema kila mwaka chama hicho tawala kimekuwa kikijitofautisha ili kuendana na mazingira, sambamba na kuendelea kuwapika viongozi wapya.

“CCM ni chama kikikubwa cha siasa cha Afrika, kinabadilika kulingana na wakati,”amesema Wasira aliyewahi pia kuwa mbunge kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi.