Dodoma. Watu wasiojua kusoma na kuandika wameruhusiwa kusaidiwa kupiga kura na ndugu zao wanaowaamini, huku wazee na watu wenye ulemavu wakipewa kipaumbele katika vituo kadhaa vya kupigia kura.
Leo, Jumatano Novemba 27, 2024, Mwananchi Digital imeshuhudia wananchi wengi wakijitokeza kupiga kura kwenye vituo vilivyopangwa katika mitaa yao, huku wakifika mapema kabla vituo havijafunguliwa.
Vaileth Nyamsogoro, mkazi wa Oysterbay jijini Dodoma, amepongeza maandalizi akisema wamepiga kura bila usumbufu.
Hata hivyo, amesema kwenye kituo alichopigia kura hakuna eneo la faragha la kupigia kura, hali iliyosababisha majirani kusaidia kwa kutoa viti na meza.
“Tulipofika hapakuwa na eneo la faragha, lakini tulipoomba msaada wa majirani walitusaidia na hilo liliimarisha usiri wa kupiga kura,” amesema.

Mkazi wa mtaa wa Msangalalee Magharibi Kata ya Dodoma Makulu Jijini Dodoma, Kennedy Chidama akionyesha kidole chake chenye wino baada ya kupiga kura kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa leo Novemba 27, 2024. Picha na Rachel Chibwete
Kennedy Chidama, mmoja wa wapiga kura, amesema aliingia na mwanaye ili amsaidie kupiga kura kwa sababu hajui kusoma wala kuandika.
“Utaratibu ulikuwa mzuri na mwanangu amenisaidia kusoma majina ya wagombea pamoja na kunionyesha nembo za vyama ninavyovifahamu. Nimepiga kura kwa amani na nina uhakika wa uamuzi wangu,” amesema.
Aidha, wazee, watu wenye ulemavu na wagonjwa wamepatiwa kipaumbele kwenye baadhi ya vituo ambako Mwananchi Digital imefika na kushuhudia huku hali ya utulivu ikiwa imetawala.
Polisi waliopo kwenye kila kituo wanahakikisha usalama na amani inazingatiwa wakati wote wa upigaji kura.
Endelea kufuatilia Mwananchi.