Wasiofahamika waiba nguzo 140, waya uwanja wa ndege Moshi

Moshi. Watu wasiofahamika wameiba nguzo zaidi ya 140 na waya wa uzio katika uwanja wa ndege wa Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Hayo yamesemwa jana Jumamosi, Machi 1, 2025 na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, wakati akizungumza katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani humo.

Lengo la kikao hicho kilichofanyika Moshi Mjini ni kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM kwa mwaka 2020/25.

Babu amesema Serikali imetoa Sh12.5 bilioni kwa ajili ya ukarabati wa uwanja wa ndege wa Moshi, na kati ya hizo, Sh4 bilioni ni kwa ajili ya uzio. Wakati mkandarasi akiwa hajakabidhi kazi, tayari zimeibiwa nguzo 140 na waya.

“Tunaufanyia ukarabati uwanja wa ndege wa Moshi na Serikali imetoa Sh12.5 bilioni, na katika fedha hizo, Sh4 bilioni ni kwa ajili ya ujenzi wa uzio wa uwanja huo. Mkandarasi hajakabidhi kazi, tayari kuna nguzo 140 zimeibiwa na waya ambao unafanya uzio ule umekatwa,” amesema Babu.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu  akizungumza kwenye kikao cha Halmashauri kuu ya CCM Mkoa wa Kilimanjaro

“Hao waliofanya kazi hiyo ni Watanzania wenzetu ambao hawana uchungu na fedha zinazotolewa na Serikali. Tayari nimetoa maelekezo nguzo zote 140 zilizoibiwa zirudi pale, na ule waya uliokatwa nataka urudishiwe uwe kama ulivyokuwa mwanzo wakati mkandarasi akifanya kazi,” amesema.

Aidha, Babu ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi mkoani humo amesema mpaka sasa hakuna aliyeakamatwa kuhusiana na tukio hilo na kueleza kuwa wanaendelea kufuatilia.

Katika hatua nyingine, Babu amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua kwa watumishi ambao watabainika kukwamisha utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM kwa kuendeleza rushwa na ubadhirifu wa mali za umma.

Naye Mkurugenzi wa kampuni ya Rocktronic Ltd, ambao ni wakandarasi katika uwanja wa ndege Moshi, Prajesh Chauhan, amesema tayari amesharipoti suala hilo polisi kwa ajili ya uchunguzi zaidi na taratibu nyingine.

Akizungumza kwenye kikao hicho cha Halmashauri Kuu, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), Seleman Mfinanga, ameipongeza Serikali kwa kazi kubwa ya utekelezaji wa miradi mbalimbali katika mkoa huo, hatua ambayo inakiweka chama hicho katika nafasi nzuri ya ushindi katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.

Mfinanga ambaye ndiye alikuwa Mwenyekiti wa kikao hicho, amesema pamoja na kazi kubwa ambayo imefanywa na Serikali, ipo miradi ambayo inaendelea na haijakamilika, na kuwaomba wasimamizi, ikiwemo wakurugenzi wa Halmashauri, kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati.

“Kuna miradi ambayo haijakamilika na mingine imebakia kidogo kukamilishwa. Niombe wabunge na wakurugenzi wasimamie miradi hiyo na kuhakikisha inakamilika kwa wakati. Niombe pia wakurugenzi kuna wakati mwingine fedha zinakuja kwa ajili ya miradi na baadaye zinarudishwa. Kama miradi ipo, tekelezeni, kwani kurudisha fedha kuziombea tena inakuwa ngumu,” amesema Mfinanga.