Wasio na wapenzi leo siku yao, wajipende

Dar es Salaam. Endapo jana Februari 14 ulikosa raha kwa sababu wengi walisherehekea siku ya wapendanao kwa kupokea zawadi, ujumbe wa mahaba au kwenda matembezi na wenza wao, wakati wewe hauna mwenza, basi leo ndiyo siku yako.

Kama ambavyo jana dunia iliadhimisha siku ya wapendanao leo inaadhimishwa siku watu wasiokuwa na wenza, kwa maana nyingine inawezekana, wapo wanaowapenda lakini si wa uhusiano wa kimapenzi.

Siku hii inayofahamika kama Single Awareness Day (Siku ya kutambua upweke katika mahusiano) huadhimishwa Februari 15, siku moja baada ya kuadhimishwa Valentine.

Maadhimisho haya si kwamba yanahamasisha watu wawe wapweke, la hasha. Yanalenga kuwafanya wasio na wapenzi waelewe maana yake na wasijione kwamba kuwa katika hali hiyo ni mwisho wa maisha kwao.

 “Ni fursa kwa watu ambao hawako katika uhusiano wa kimapenzi kuwekeza nguvu kwenye kujipenda wenyewe na kujijali. Unatakiwa kufurahia uhuru wako kwa sababu kuna wengine wanatamani kupata nafasi hiyo, ameandika mwanasaikolojia Donald Kingstone wa Uingereza.

Ameongeza: “Badala ya kujisikia kutengwa au kuachwa nyuma, tumia siku hii kuponya moyo wako, jithamini kwa wema.”

Unaweza kujiuliza unasherehekeaje siku hii, kama msingi wake unavyojieleza ni siku ya kujali nafsi yako, kujipenda, na kukubali hali yako ya kuwa mpweke.

Kwa mujibu wa Kingstone unaweza kusherehekea siku hii kwa kujifanyia vitu ambavyo si mara nyingi unajifanyia, mfano kutoka kwa ajili ya mlo maalumu, inaweza kuwa mchana au usiku.

“Hapa lengo ni kujifurahisha, hivyo unaweza kufanya chochote ambacho unaona kitaipa furaha nafsi yako, inaweza kuwa kujitoa kwa ajili ya chakula kwenye mgahawa au hoteli tofauti na unapoenda mara kwa mara.

“Unaweza kuitumia siku hii kusoma kitabu, kwenda saluni, kusinga mwili, kuogelea au kufanya chochote kile kinachokupa furaha ukiwa mwenyewe na ukafurahia maisha yako ya ukapera,” amesema.

Kama huwezi kuwa mwenyewe basi unaweza kuadhimisha siku hii kwa kuungana na marafiki mkaangalia filamu au kucheza muziki kwa pamoja.

Muhimu zaidi ni kuitumia siku hii kujifunza kujipenda (self-love) huku ukitafakari kuhusu maisha yako binafsi na ustawi wake.

Kama huna mwenza leo, jiamini wala usiwe usiumize kichwa kwa hali unayopitia badala yake ongeza nguvu kwenye kujipenda na kujijali bila kusahau kuwa, hali hiyo inaweza kuwa sehemu yenye furaha na manufaa katika safari ya maisha yako.

Ukiwa ni mpenzi wa muziki zipo nyimbo kadhaa zinazoweza kukuburudisha ukiadhimisha siku hii kama Single (Harmonize), Nipo Single (Dayoo ft Ibra), Inatosha (Lavalava), Nitongoze (Rayvan ft Diamond), Lonely (Yammi ft Nandy) na nyingine nyingi zinazoweza kukupa burudani.