
Dar es Salaam. Washiriki wa mbio za Kili Marathon wametakiwa kujiandikisha mapema kabla ya Desemba 12, 2024 ili kuepuka adha ya mrundikano wa dakika za mwisho.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na waandaji wa mbio hizo maarufu barani Afrika, Kilimanjaro Premium Lager International Marathon 2024, dirisha linalotoa unafuu wa punguzo la ada ya ushiriki bado liko wazi.
Pia, wamewakumbusha washiriki kuwa, wamebakiza siku chache ambazo ni chini ya mwezi mmoja za kunufaika na muda wa punguzo wa bei ya usajili iwapo watajiandikisha kabla ya Desemba 12, 2024.
“Kipindi cha washiriki kunufaika na punguzo maarufu kama ‘ndege alewahi’ kilianza Oktoba, 21 mwaka huu, kinatarajiwa kumalizika usiku wa Desemba 12, mwaka huu,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, baada ya hapo ada ya kujisajili itaongozeka kuanzia Desemba 13, 2024, hadi Februari 3, 2025, usiku.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa, usajili unapaswa kufungwa kabla ya Februari 23, 2025 na kwamba toleo la 23 la mbio hizo linatarajiwa kufanyika katika Uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), ili kuhakikisha tukio hilo linaambatana na kanuni rasmi za Shirikisho la Riadha la Kimataifa (IAAF) zinazohusiana na idadi ya washiriki ili kuhakikisha usalama wa washiriki wakati wa tukio hilo.
“Lengo la kuzingatia kanuni hizo za IAAF ni kuhakikisha washiriki wanafurahia muda wao wakati wa ushiriki wa mbio hizo kwa kuepuka msongamano mkubwa na wakati huohuo kuhakikisha huduma zingine kama vile za vituo vya maji na huduma za afya zinatayarishwa kulingana na idadi ya washiriki,” inaeleza taarifa hiyo.
Kilimanjaro Premium Lager ndio wadhamini wakuu wa mbio za marathon na imeshika nafasi hiyo ya udhamini tangu kuanzishwa kwa mbio hizo miaka 23 iliyopita.
Mbio za mwaka ujao zinatarajiwa kufanyika Jumapili ya Februari 23, 2025 na washiriki watapata fursa ya kushiriki mbio ambazo njia zitakazotumika zimepimwa kwa mujibu wa kanuni za IAAF na zitajumuisha washiriki wa mbio za kilomita 42 (Full Marathon), 21km (Tigo Half Marathon) na mbio za kilomita 5 (5km Fun run).