Washindi sita ‘Tembo Card Shwaa’ kutalii Serengeti

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Benki ya CRDB imetangaza washindi sita wa kampeni ya ‘Tembo Card Shwaa’ ambao watasafiri kwenda kutalii katika mbuga ya Serengeti mkoani Mara.

Washindi hao ambao watasafiri wakiwa na wenza wao wamepatikana kupitia droo iliyochezwa Aprili 3,2025 ikiwa ni awamu ya kwanza ya Kampeni ya ‘Tembo Card Shwaa’.

Meneja Mwandamizi Kitengo cha Kadi wa Benki ya CRDB, Karington Chahe, amesema kampeni hiyo inalenga kukuza matumizi ya kadi na ili kuweza kushinda mteja anatakiwa kuchanja na Tembo Kadi katika kila matumizi.

Amesema kupitia kampeni hiyo wanatarajia kupeleka washindi 24 mbuga ya Serengeti kutalii na kuunga mkono kaulimbiu ya Royal Tour.

“Tumewapata washindi wetu wa Serengeti awamu ya kwanza na kutakuwa na washindi wa awamu nyingine mbili. Tulipozindua kampeni hii ulikuwa wakati wa Valentine kwaiyo, washindi wetu tutawapeleka kutalii Serengeti wakiwa na wapendwa wao,” amesema Chahe.

Washindi hao ni Sanora Shoo, Mashaka Ndonde, Agnes Kanje, Brighton Materu ambao ni wakazi wa Dar es Salaam, Ponsiano Sawaka (Arusha) na Arnold Likiwike (Kilimanjaro).

Meneja huyo amesema pia kampeni hiyo itakuwa na washindi watano ambao watapelekwa Ulaya.

“Tunasema Tembo Kadi Shwaa kiulaya ulaya, washindi watalipiwa kila kitu na Benki ya CRDB na watatembelea zaidi ya nchi tano za Ulaya.

“Tumia Tembo kadi yako kufanya miamala na jinsi unavyozidi kutumia kadi yako ndivyo unaongeza nafasi ya kushinda kwenye zawadi hizi…Watanzania wahakikishe wanafungua akaunti za CRDB na kupata kadi za Tembo,” amesema.

Kampeni hiyo ilizinduliwa Februari 13,2025 na inatarajiwa kufikia tamati Juni mwaka huu ambapo mshindi wa jumla atajinyakulia gari mpya (kilomita sifuri) aina ya Ford Ranger.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *