
Dar es Salaam, Kuna kipindi iliaminika kuwa video kali za muziki zinapatikana kwa waongozaji wa nje ya nchi, hilo lilipelekea wasanii wengi hasa wale wa Bongo Fleva kutumia mamilioni ya fedha huko katika kuandaa kazi zao.
Hata hivyo, nyakati zimebadilika na kwa asilimia kubwa wasanii wanaonekana kubakisha fedha hizo kwa waongozaji wa nyumbani ambao wanawapatia picha nzuri na safi sawa na zile ambazo walilazimika kufunga safari kuzifuata.
Mathalani katika Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) 2023, katika kipengele cha Video Bora ya Mwaka, kati ya tano zilizotajwa kuwania, ni moja tu ndio imefanyika nje ya nchi tena kwa sababu maalamu.
Nayo ni Single Again Remix yake Harmonize, hii imefanyika Nigeria kwa sababu wimbo huo umemshirikisha msanii wa huko ambaye ni Ruger ila toleo la awali la wimbo huo video yake imefanyika hapa Tanzania.
Video nyingine katika kipengele hicho ambazo zimefanyika nchini ni Maokoto (Billnass), Sele (Mbosso), Nani Remix (Zuchu) na Achii (Diamond Platnumz) ambayo ndio ilishinda.
Akizungumza na gazeti hili, Director Ivan amesema wasanii wakubwa Bongo kuanza tena kufanya kazi na waongozaji wa video nchini baada ya kwenda nje kwa muda mrefu, ni katika kubadilisha upepo wa biashara yao.
“Wakati huu wanahitaji ladha nyingine mpya kabisa, huwezi kuwa kila siku unashuti na watu wale wale, pia hilo ni suala la kibiashara zaidi. Kikubwa ni kuweka juhudi na kufanya kazi vizuri ili uweze kuendelea kusalia katika nafasi yako” anasema Ivan.
Mwaka huu Ivan ameongoza video nyingi, moja wapo ni ya Harmonize, I Made It (2025) akimshirikisha Bobby Shmurda kutokea Marekani, hii imefanyika Tanzania na Marekani na kwa mujibu wa Ivan, imegharimu zaidi ya Sh100 milioni.
Baadhi ya wasanii au kupitia menejimenti zao waliwahi kuweka wazi gharama walizotumia katika kufanya video nje kama ifuatavyo, video ya Diamond, Nana (2015) iliyofanyika Afrika Kusini kwa Director Godfather iligharimu Dola40,000.
Video ya Alikiba, Aje (2016) ikiongozwa na Director Meji wa Afrika Kusini iligharimu Dola 32,000, Vanessa Mdee, Never Ever (2015) ikiongozwa na Director Justin Campos wa Afrika Kusini iligharimu Dola20,000.
Pia kuna Harmonize, Aiyola (2015) ilifanyika Afrika Kusini kwa Director Nick Roux na kugharimu Sh39 milioni, Shetta, Kerewa (2014) ilisimamiwa na Godfather kwa Dola 10,000, Joh Makini, Don’t Bother (2015) ilisimamiwa na Justin Compas kwa dola15,000.
Ukitazama kwa makini utabaini kuwa nchi ya Afrika Kusini ndio kimbilio la wasanii wengi, ukiachana na hao, wengine waliowahi kufanya video zao huko ni Mbosso, Lady Jaydee, Chege, Madee, Aslay, Billnass, Nikki wa Pili, Country Wizzy, G Nako, Lulu Diva.
Pia kuna Ommy Dimpoz, Mwana FA, AY, Fid Q, Rosa Ree, Jux, Shilole, Barnaba, Navy Kenzo, Dogo Janja, Mabantu, Zuchu, Rich Mavoko, Nandy, Marioo, Darassa, Mac Voice, Yamoto Band, Rayvanny, Young Lunya n.k.
Msanii Nahreel kutoka kundi la Navy Kenzo ambao video ya wimbo wao, Nisogelee (2021) ndio ilikuwa ya kwanza Bongo kufanyika katika daraja la juu Ubungo, Kijazi Interchange, amesema wasanii walikuwa wanaenda nje kufuata vitu kama hivyo.
“Tulikuwa tunaenda mbali kutafua location kama hizi, unaenda Afrika Kusini labda ili upate sehemu ina daraja lakini leo hii tunavyo hapa Tanzania, tuna mradi wa reli, ukienda kule Coco Beach kuna daraja la juu ya maji,” amesema.
“Kama sasa hivi tuna madaraja, kwanini tusifanye hapa?, kwa kifupi siku zinavyozidi kwenda tutakuwa na location nzuri na ni vitu ambavyo tunapaswa tujivunie kama wasanii,” amesema Nahreel ambaye pia ni Mtayarishaji Muziki kutoka studio ya The Industry.
Ikumbukwe video tatu za juu za Navy Kenzo ambazo zimetazamwa zaidi YouTube zimefanyika Afrika Kusini, nazo ni Katika (2018) imetazamwa (views) zaidi ya mara milioni 32, Kamatia (2016) milioni 17, Game (2015) milioni 4 na Feel Good (2016) milioni 4.
Hata hivyo, kwa muda sasa kumekuwepo na madai kuwa wasanii wengi Bongo wanawekeza fedha nyingi katika video huku wakifanya kwa kiwango cha chini sana upande wa muziki wenyewe (audio) kitu ambacho sio sawa.
“Hapa Tanzania kuna shida moja, wasanii wanazingatia sana ubora wa video kuliko audio (wimbo wenyewe) wakati wanapaswa kuipigania zaidi audio,” anasema Jabir Saleh, Mtangazaji vipindi vya burudani E FM Radio.
“Kuna mtu wa kimataifa aliniambia audio za Tanzania zina shida sana, yaani production ni mbovu mno!, unaweza kuvutia na video lakini audio unakuta hamna kitu, hivyo wanakosa nafasi sehemu nyingi za nje ambazo watu wanasikiliza muziki tu,” anasema Jabir.
Ili kutatua hilo au kuboresha muziki wao, baadhi ya wasanii kama Diamond na Marioo, wamekuwa wakisafiri sehemu mbalimbali wakiongozana na watayarishaji wao ambao ni S2kizzy na Abbah ili kupata utulivu na uzoefu kutoka kwa wenzao.
Mtayarishaji muziki, Abbah amesema kuwa muziki unakua hivyo kunatakiwa kuwepo na maudhui ya aina tofauti tofauti, kwa hiyo wasanii wanapotoka wanaenda kujifunza vitu vipya ambavyo wanaweza kuvitumia katika muziki wao.
“Ni maamuzi binafsi kama unahisi nikiwa Afrika Kusini naweza kutengeneza muziki mzuri sio vibaya kwenda, ni kama tu unavyoenda Dodoma, hivyo sio kama inaharibu chochote kile katika tasnia yetu,” amesema Abbah.
Kauli ya Abbah inakuja wakati baadhi ya wasanii akiwemo Alikiba wanasema fedha zinazowekezwa katika kuandaa video huwa zinachelewa kurudi au kupotea kabisa, hivyo utafika wakati watakuwa wanatoa audio pekee.
Hilo linaungwa mkono na Meneja Vipaji na Mtendaji wa Kibiashara katika Muziki, Sandra Brown ambaye anasema kutengeneza audio ni nafuu kuliko video, ila bado video ina umuhimu wake katika kuutangaza wimbo husika.
“Ikiwa utawekeza Sh20 milioni kwenye video, jua hiyo ni fedha ambayo inatoka, hairudi. Unafanya hivyo ili kuweza kuitangaza ile bidhaa ambayo ni audio, kwa hiyo video ya muziki ni sawa na tangazo la biashara, na audio ndio bidhaa yenyewe,” anasema.
“Audio ni bidhaa itaenda itatengeneza fedha kupitia mirabaha, kupitia kampuni za usambazaji, kwa hiyo tayari nina njia kama tatu au nne za kuweza kuingiza fedha kupitia sauti bila picha,” anasema Sandra, Meneja wa zamani wa Mbosso.
Ikumbukwe miongoni mwa wasanii wa mwanzo Bongo kuanza kwenda nje kwa ajili ya kufanya kazi ni AY, mathalani wimbo wake, Usijaribu (2007), audio na video vilifanyika Kenya kwa Ogopa Deejays/Video, na baadaye ilishinda tuzo za Kisi