Wasanii na wasomi wa Uhispania, watoa wito kwa Madrid kusitisha biashara ya silaha na Israel

Mamia ya wasomi na wasanii wa Uhispania wameandika barua kwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Pedro Sanchez, wakitaka kuwekwa vikwazo vya silaha dhidi ya Israel kutokana na ukatili unaoendelea kufanywa na utawala huo huko Gaza na Lebanon.

Zaidi ya shakhsia 300 mashuhuri wa tasnia ya habari na burudani, pamoja na duru za wasomi, wameelezea wasiwasi wao juu ya biashara inayoendelea ya silaha na zana za kijeshi baina ya Uhispania na Israel.

Shakshia hao wameitaka serikali ya Uhispania kusitisha kabisa aina zote za biashara ya silaha na zana za kijeshi na Israel, na wameeleza wasiwasi wao mkubwa juu ya uhusiano wa kijeshi unaoendelea baina ya pande hizo mbili.

Miongoni mwa watu hao muhimu ni pamoja na wakurugenzi wa filamu Pedro Almodovar na Isabel Coixet, wanamuziki Rozalen na Mikel Izar, waigizaji Aitana Sanchez Gijon na Alba Flores, na mchekeshaji Andreu Buenafuente.

“Maadamu Uhispania inaendeleza uhusiano wa kijeshi na Israel, itaendelea kushiriki katika mauaji haya,” imesema barua hiyo, ikitaka hatua za haraka zichukuliwe.

Vilevile wametoa wito kwa utawala wa Sanchez kufanya juhudi zaidi za kuwalinda raia katika mauaji ya kimbari ya Israel.

Maelfu ya raia wameuawa katika mashambulizi ya Israel Ukanda wa Gaza

Oktoba mwaka jana Uhispania ilitangaza kuwa imesitisha biashara ya silaha na Israel kutokana na mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala huo huko Gaza.

Hata hivyo, uchunguzi mpya unaonyesha kuwa Madrid imeendeleza uhawilishaji wa silaha kwa utawala huuo katili.