Wasanii hawa walivyo kizungumkuti kulipa madeni

Dar es Salaam. Dawa ya deni kulipa” hivi ndivyo walivyosema Wahenga. Lakini msemo huu unaonekana kupewa kisogo na baadhi ya wasanii nchini ambao walikopa fedha kupitia Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania. 

Mfuko uliopewa hati ya usajili Septemba 2020, ukiwa na lengo la kuinua ubora wa kazi za utamaduni na sanaa ili ziweze kujiendesha kibiashara, kutengeneza ajira nchini pamoja na pato la taifa.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Sanaa na Utamaduni Tanzania, Nyakaho Mahemba anasema licha ya kutoa mikopo kwa wasanii kwa lengo la kuwasaidia kujiendesha kiuchumi lakini baadhi yao wanatumia pesa hizo nje ya malengo na wengine wanakimbia madeni.

“Kuna baadhi ya wasanii, ambao wao wanatabia ya   kutolipa madeni. Hasa wanaofanya vibaya ni baadhi ya wasanii wa muziki wa nyimbo za injili. Wao wanasuasua katika marejesho, hawafanyi vizuri kwenye kulipa, tena ni wasanii wakubwa,” amesema

Amesema mbali na kusumbuliwa na baadhi ya wasanii wa nyimbo za injili, wapo wengine waliokopa na kukimbia nchini.

“Hawa wasanii wasiolipa kuna hatua ambazo  tunazichukua kwa ajili yao. Hatupo tayari kufanya kazi na msanii ambaye tumempa pesa inayotokana na kodi za Watanzania halafu anaitumia kwa manufaa yake.

“Tunafahamu ya kwamba mkono wa serikali ni mrefu. Hata hao ambao wamekimbilia nchi za nje, tumeongea na balozi katika nchi husika tunawatafuta. Hii ni kodi ya watu hatuwezi kumuacha mtu katika hili,”amesema Nyakaho na kuongezea. 

“Kwa sasa mfuko unatoa mikopo kwa kushirikiana na Benki kadhaa. Lengo la ushirikiano huu ni kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma, kutumia utaalamu na uzoefu wao katika eneo la utoaji wa mikopo, usimamizi wa marejesho pamoja na ufuatiliaji wa miradi,”amesema.

Alisema changamoto nyingine ya wasanii ni kupenda kufanya kazi kiholela.

“Baadhi ya wasanii wanafanya kazi katika mifumo isiyo  rasmi. Yaani unakutana na msanii mkubwa lakini hana akaunti ya benki, namba ya NIDA, email. Sasa hiyo haifai kwa sababu kufanya kazi na benki lazima uwe na vitu vilivyo katika mfumo rasmi,”alisema.  

Aidha amekanusha tetesi za baadhi ya watu zinazodai kuna upendeleo katika utolewaji wa mikopo hiyo.

“Fuateni taratibu, pesa zinatoka kwa watu wenye sifa. Lakini pia tunaendelea kuwajengea uwezo wachangamkie fursa. Huu ni mfuko wao wasanii, fedha ni zao wachangamkie fursa wakope.

“Lakini wakiwezeshwa waingize hela katika miradi waliyoombea. Wasitumie kinyume na malengo, wasimamie miradi yao vizuri. Baada ya hapo walipe mikopo kwa wakati ili wengine waweze kuwezeshwa,” amesema.

Hata hivyo, akizungumzia madai ya wasanii wa muziki wa injili kugeuka kikwazo katika mfuko huo. Rais wa Shirikisho la Muziki Tanzania Addo November, anasema madai hayo ni ya ukweli ingawa wapo baadhi wanaolipa vizuri.

“Ni kweli baadhi ya wasanii wanasumbua kwenye malipo ya mkopo wakiwemo wasanii wa injili. Nilishaongea nao wanapaswa kulipa haraka iwezekanavyo na kama hawajafanya hivyo nilishawaambia majina yao nitayaanika kwa wasanii wenzao,” amesema November.

Sambamba na hayo amewatahadharisha wasanii kwa kusema hakuna fedha yoyote itakayabaki mfukoni kwa mtu.

“Njia ni moja kulipa. Mkono wa serikali ni mrefu kwa yeyote atakayejaribu kukimbia mkopo huo, atakamatwa. Serikali isikatishwe tamaa na wasanii wachache wanaokwepa kulipa mikopo,”amesema.

Hadi sasa mfuko huo umefanikiwa kutoa mikopo yenye thamani ya Sh 5,250,070,500.89 kwa miradi 359 ya sanaa iliyozalisha jumla ya ajira 497,213 ikiwemo miradi ya muziki 78, filamu 90, maonesho 65, ufundi 103 na lugha na fasihi 23.

Huku mikoa 18 ikiwa imenufaika na mikopo hiyo. Kati yake ni  Dar es Salaam, Arusha, Morogoro, Pwani, Geita, Mwanza, Mbeya, Dodoma, Kagera, Mara, Shinyanga, Tabora, Singida, Manyara, Kilimanjaro, Simiyu, Kigoma na Katavi.

“Kupitia uwezeshaji wa mikopo kisekta. Sekta ya muziki imepata mikopo yenye thamani ya Sh 1,246,215,189 kwa miradi 78, filamu Sh 1,329,007,342.00 kwa miradi 90, sekta ya sanaa za ufundi Sh 1,550,060,050.00 kwa miradi 103 na sanaa za maonesho imepata mikopo ya Sh 759,087,719.00 kwa miradi 65,”alisema Nyakaho.
 
Alisema katika mikopo hiyo yenye thamani ya Sh 5,250,070,501.89 iliyotolewa kwa miradi 359. Sh 1,470,019,740 zilikopeshwa kwa makampuni 54, Sh 525,007,050 zilikopeshwa kwa vikundi/bendi 31, Sh 1,312,517,625 zilikopeshwa kwa miradi 109 inayomilikiwa na wanawake na Sh 1,942,526,085. 89 kwa miradi 165 inayomilikiwa na wanaume.

Ikumbukwe mikopo hiyo inatolewa katika aina mbalimbali za sanaa kama vile sanaa za muziki, filamu, sanaa za maonesho, sanaa za ufundi,  lugha na fasihi.  Huku kiwango cha mkopo kikianzia Sh 200,000 hadi Sh 100,000,000.

Mkopo unaanza kurejeshwa baada ya miezi mitatu ndani ya miezi ishirini na nne. Huku riba ikiwa ni asilimia tisa tu.

Nyakaho ameongezea kuwa kwa msanii anayetaka kukopa anatakiwa kufuata vigezo hivi,

>> Barua ya maombi ya mkopo

>> Barua ya utambulisho wa makazina eneo la biashara kutroka kwa Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa\Kijiji

>> Picha mbili za mwombaji na mwenza wake kama yupo

>> Kitambulisho cha taifa,hati ta kusafiria au leseni ya udereva

>> Cheti cha usajili\Utambulisho\kibali kutoka taasisi inayosimamia kazi ya Utamaduni na Sanaa

>> Utambulisho wamwombaji kuwa ni mwanachama  wa umoja wowote.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *