Dar es Salaam. Wakati usiku wa leo Alhamisi, Februari 27, 2025 ni kilele cha sherehe za uzinduzi wa Kariakoo ya saa 24, wasanii zaidi ya 10 wanatarajiwa kukiwasha kwenye usiku huo.
Hilo limesemwa leo Alhamisi Februari 27, 2025 Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Toba Nguvila, alipokuwa anataja orodha ya wasanii watakaokuwapo kwenye uzinduzi huo unaofanyika jijini humo usiku huu.
Dk Nguvila amewataja wasanii hao kuwa ni Kinata Mc, Duly Sykes, Tundaman, Yamoto band, Jay Combat, Harmonize, Chino man na Man Fongo.

Ufanyaji biashara huo unalenga kuimarisha uchumi wa Mkoa wa Dar es Salaam, kuongeza mapato ya Serikali na kutoa fursa za ajira.
Uzinduzi wa ufanyaji biashara huo ulianza rasmi Februari 25, 2025 kwa kuwa na shughuli mbalimbali.
Moja ya shughuli hizo ni pamoja na ufanyaji usafi, kutolewa kwa semina na taasisi mbalimbali kuhusu masuala ya biashara ikiwemo mikopo na namna ya uanzishaji biashara na usajili wa kampuni.
Aidha leo kumekuwa na ufanyaji mazoezi ya kukimbia ulioanzia viwanja vya Mnazi Mmoja hadi Mtaa wa Mkunguni na Swahili Kariakoo kunapofanyikia shughuli hiyo ya uzinduzi ambapo Mkuu wa Mkoa huo, Albert Chalamila aliongoza mazoezi hayo.