Kwenye vituo mbali mbali vya kupigia kura, wananchi wamejitokeza mapema kushiriki zoezi la upigaji kura, wakifahamu ni uchaguzi unaowapa fursa ya kuwachagua viongozi watakaoleta maendeleo.
Apolonie Dusabe ni mpiga kura na anasema hakuna rabsha zilizoshuhudiwa katika shughuli hiyo ya Alhamisi ila Hussein Ntahombaye ni raia mwengine anayedai licha ya uchaguzi kuwa wenye utulivu, kinachohitajika ni matokeo ya uchaguzi kukubaliwa na pande zote, ili kuepuka vurugu.
Mkuu wa tume ya uchaguzi Prosper Ntahorwamiye licha ya kudai kwamba zoezi hilo limekwenda vyema, amekiri kulikuwa na dosari zilizoshuhudiwa pia.
Kwenye kituo cha Shule ya upili ya International waangalizi wa kimataifa walikataliwa kufuatilia uchaguzi. Mkuu wa Ceni Ntahorwamiye ameomba radhi na kusema watafanya uchunguzi kuhusiana na changamoto hizo zilizoripotiwa.
“Kwa jumla zowezi limekwenda vizuri lakini hakuna kinacho kusa na kasoro. Lakini ni makosa madogo ambao hayawezi kuathiri uchaguzi. Tumepata taarifa kuwa timu ya waangalizi wa Umoja wa Afrika ilokatariwa kufuatilia uchaguzi kwenye moja ya vituo vya hapa Bujumbura. Kama ni hakika kwa niaba ya tume ya kuanda uchaguzi Ceni tunaomba radhi kwa kosa hilo”, alisema Ntahorwamiye.
Utulivu huo ulioshuhudiwa katika vituo vya kupigia kura umetokana na idadi kubwa ya walinda usalama waliokuwa wameshika doria tayari kukabiliana na utovu wowote wa usalama utakaoshuhudiwa.
Upinzani haukushiriki uchaguzi
Mapungufu kadhaa yameshuhudiwa katika zoezi hilo huku baadhi ya wapiga kura wakilalamikia kutoshiriki kutokana na kutoonekana kwa majina yao katika madaftari ya wapiga kura.
Viongozi mbali mbali pia walikuwa miongoni mwa waliojitokeza kupiga kura zao. Katibu mkuu wa chama Cndd/Fdd amesema ana matumaini ya kushinda uchaguzi, na kwamba baada ya uchaguzi ni kujikita katika harakati za maendeleo.
Hata hivyo kutokana na hatua ya chama kikuu cha upinzani National Freedom Council NCL, kufungiwa kushiriki uchaguzi huo, baadhi wanahisi kwamba ni zoezi la chama tawala CNDD/FDD na washirika wake kuwachagua viongozi.
Mkoani Kirundo kumeripotiwa wapiga kura waliochanachana kadi zao za kupigia kura. Kesi yao tayari imefikishwa mahakamani.
Na mkoani Cibitoke kumeripotiwa afisa wa tume ya uchaguzi alomtandika raia mpiga kura kwa sababu zisizo tambulika.
Wakati huu ni kiripoti tayari vituo vya kupiga kura vimefungwa. Na matokeo ya muda yataanza kutangazwa saa 2 usiku.