Dar es Salaam. Wanasiasa wakongwe nchini wameshauri kuwapo maridhiano kwa vyama vya siasa kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu Oktoba, 2025.
Wakongwe hao, Waziri Mkuu wa zamani, Jaji Joseph Warioba na Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku wameeleza hayo, wakishauri Rais Samia Suluhu Hassan kuweka meza ya mazungumzo kati ya Serikali, Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ili kumaliza tofauti kabla ya uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu.
Jaji Warioba amesema endapo hilo halitafanyika nchi itaingia katika uchaguzi ikiwa katika mgawanyiko kuanzia viongoni na wananchi. Hivyo, amesema dawa pekee ipo katika mazungumzo na si mapambano ya lugha zinazogawa Taifa.

Ametoa kauli hiyo leo Mei 3, 2025 alipozungumza kwenye Kongamano la Uchaguzi Mkuu 2025 lililoandaliwa na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) lililofanyika jijini Dar es Salaam.
Wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu kumekuwapo kauli zinazoashiria mvutano kati ya Chadema, Serikali na CCM. Chadema kimeweka wazi kwamba, pasipo mabadiliko hakuna uchaguzi kupitia ajenda ya No reforms, No election.
Jaji Warioba amesema yeye na Mzee Butiku walikuwa wamefikiria kuwashauri viongozi wa nchi waone uzito wa yale yanayoendelea na wachukue hatua, kwani muda bado upo wa kuweza kuzungumza na mwafaka kupatikana.
Amesema bado shughuli za uchaguzi hazijaanza hadi Bunge litakapovunjwa, hivyo kwa kipindi hiki ipo nafasi ya kuzungumza na kufikia mwafaka.
“Na haya mambo sisi tulikuwa tunasema kama ni kurekebisha dosari zilizotokea katika uchaguzi wa mwaka 2019, mwaka 2020 na mwaka 2024 tunao muda kwa sababu ni mambo ya kanuni. Kanuni hazihitajiki kwenda bungeni, tukikubaliana kanuni zinaweza kubadilishwa, tufikie makubaliano, tusiende kwa mapambano,” amesema.
Vyama 18 vya siasa vyenye usajili wa kudumu, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na Serikali vimesaini Kanuni za Maadili ya Uchaguzi zitakazotumika katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2025 isipokuwa Chadema.
Jaji Warioba amesema ni vyema Rais Samia achukue jukumu la kuandaa meza ya mazungumzo akieleza alipoingia madarakani alichukua hatua kama hizo.
“Shughuli za kisiasa zilifungiwa, uhuru wa maoni ulizuiwa, akachukua hatua. Akakutanisha vyama vya siasa vikazungumza, nchi ilikuwa imetulia sasa yanazuka haya, bado anaweza kwa kuona uzito wa jambo hili na kwamba maridhiano ni muhimu, anaweza akawaita hasa wanaohusika, Serikali, CCM, Chadema wakae tofauti zao kila upande ukubali kwamba waache msimamo wao kwa kiwango,” amesema.
Amesema kufanya hivyo kutasaidia pande zote kufikia mwafaka na kujua namna ambavyo watakwenda katika uchaguzi bila matatizo.
“Kuna watu wanaodai wameumizwa kwa sababu ya siasa, tukiendelea hivi tukifika muda wa kampeni kuanza Serikali itasema Polisi wasimamie amani washughulike na yeyote anayetaka kuvuruga amani.
“Chadema wataendelea kusema No reforms, No election, katika kampeni ya aina hiyo kutakuwa na migongano. Migongano hiyo inaweza kuleta madhara kwa wananchi, ni muhimu kama Taifa kukaa pamoja kuona namna ambavyo tunaweza kujiepusha,” amesema.

Amesema hadi shughuli za uchaguzi zitakapoanza upo muda wa kutosha na endapo kutakuwa na utashi wa kisiasa suluhisho litapatikana.
Mwanazuoni na mchambuzi wa masuala ya siasa, Deus Kibamba amesema kupitia Katiba ya Tanzania, Zanzibar na sheria ya uchaguzi wa Rais wabunge na madiwani, Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi amebaini kuwapo mambo 97 yanayopaswa kushughulikiwa kabla ya uchaguzi.
Amesema mambo 50 kati ya hayo yanayopaswa kushughulikiwa hayahitaji mabadiliko ya sheria wala Katiba bali vitu, utaratibu, utamaduni ambao upo kwa baadhi ya watu ambao haujaandikwa sehemu yoyote.
“Yale mengine yanahitaji uguse sheria au Katiba,” amesema Kibamba.
Amesema kitendo cha mmoja wa Makamishna wa INEC kuwa na historia ya kuwa kiongozi mwandamizi wa chama cha siasa kunaweza kuwaondolea wananchi imani juu ya usimamiaji haki kwenye uchaguzi.