Waridi wa BBC: Mwanangu mwenye jinsi tata aliniambia ‘ninaweza kujitoa uhai’

.

Chanzo cha picha, Babi

Maelezo ya picha, Babi na mama yake

  • Author, Martha saranga
  • Nafasi, BBC Swahili
  • Akiripoti kutoka Tanzania

Anavuta kumbukumbu hadi Juni 3, 1994, zilipotimia siku za kujifungua ikiwa ni uzazi wake wa sita watoto wanne wakiwa hai na uzao wa kwanza kufariki miaka mingi iliyopita.

Bi Sofia anasema alipojisikia tu dalili za uchungu wa kujifungua alianza safari hadi hospitali ya Amana jijini Dar es Salaam akisindikizwa na mumewe.

Walipowasili hospitalini hapo tayari alianza kuhisi damu inavuja na mara alipokewa hadi katika chumba cha ukaguzi na baada ya muda mfupi aliandaliwa kwa ajili ya kujifungua.

Sofia Yusuph Masiana ni mwanamke mjasiriamali mkazi wa Dar es Salaam Tanzania, mama wa watoto watano akiwemo wa mwisho Babi John Musamba ambaye alibadili historia yake baada ya kuzaliwa bila maumbile ya kumtambulisha jinsi ya kiume au ya kike.

Anakumbuka kuwa haikuchukua muda mrefu alijifungua mtoto salama, muuguzi akamtoa na kumlaza pembeni akisubiri kondo la uzazi kutoka.

”Umejifungua mtoto wa kike” hawakumweka kwangu, walimweka pale … baadaye muuguzi mwingine akapita akasema si wa kike ni wa kiume…

Ndipo akajikuta katika lindi la mawazo kwa kushindwa kuwaelewa wauguzi hakujua ashike la muuguzi yupi, ndipo akaomba kumuona mtoto ili amkague mwenyewe.

”Nilipomshika kumfunua kwenye kike hayupo, kiumeni hayupo, ni mtoto wa jinsia gani huyu? akajiuliza na kujijibu basi Mungu atajua tu akamrudisha kumlaza alipokuwa.

Baada ya saa kadhaa anasema mume wake alifika hospitali kuleta chakula. Mume alipofika na kusikia kuwa tayari amejifungua salama aliingia kwa bashasha kumuona mkewe, na swali la kwanza anakumbuka lilikuwa ”tumepata mtoto gani? akamjibu ”mimi mwenyewe sielewi”

Tumpe jina gani?

Wazazi walichanganyikiwa na hawakujua jina stahiki la kumpatia mtoto wao. Ni wakati mwingine ambao Bi Sofia kama mama hakuacha kugubikwa na wimbi la mawazo juu ya namna gani wangemlea mtoto huyu? je wangempa jina gani? wangemlea kama binti au kijana? miongoni mwa maswali alijiuliza huyu mtoto namlea mwishowe atakuwa nani? anasema anamshukuru Mungu kwa ajili ya mume wake ambaye mara zote alisimama kidete kuhakikisha hakuna kinachoharibika si tu kwa mkewe hata kwa familia yote hasa watoto wake.

Mume wangu alisema atampa jina, akamuita Babi yaani akilenga huko mbeleni akijipambanua kama mvulana basi aendelee kuitwa Babu, au akijipambanua kama msichana basi tumwite Kibibi.

Familia na Jamii ilivyolichukulia suala hilo

Haikuwa rahisi kuikubali hali isiyoeleweka aliyoikuta kwa mwanae huyo aliyezaliwa na afya njema kabisa. Baada ya kuruhusiwa kurejea nyumbani, mumewe alipitiliza chumbani na mtoto wao mchanga ili kumkagua alipojiridhisha juu ya alichokiona kwa mwanae mchanga basi waliwajulisha wanandugu na familia juu ya mtoto.

Bi Sofia anasema ndugu walipokea vizuri anakumbuka aliulizwa’ vipi anaweza kujisaidia haja zote vizuri? basi huyo hana shida endeleeni na maisha, kauli iliyowatia moyo kwa muda tu.

Kama ilivyo kawaida watu wanapomtembelea mzazi aliyejifungua hawaachi kumuulizia jinsi yake naye hakusita kuwaambia ukweli kwamba huyu si msichana wala mvulana. “Sikuweza kuona mishangao kwa wakati huo lakini baadhi walitoka na kushangaa na hali hiyo ya mwanangu, na taratibu taarifa zikasambaa na kadri mtoto alivyoendelea kukua na kujichanganya na jamii nikagundua namna baadhi ya watu walivyotunyooshea vidole”.

”Huyu mtoto wake sijui yukoje”akipita sasa wanamsonda vidole”ona huyu mtoto si mwanamke wala mwanaume”

Wapo waliothubutu kumtamkia wazi kuwa hiyo ni laana, au amerogwa na kumshauri kutafuta ufumbuzi kwa waganga wa kienyeji uamuzi ambao hakuutilia maanani.

Kuna wakati baba mdogo alimwambia ameulizia kwa mganga mmoja wa jadi ambaye amemuhakikishia kuwa na tiba ya hali ya mtoto huyo hivyo akimtaka Bi Sofia kufunga safari hadi kwa mganga, ushauri ambao hakuuona kuwa na tija.

.

Chanzo cha picha, Babi

Safari za matibabu hospitalini

Baada ya muda walianza safari za kurudi hospitali moja hadi nyingine kujaribu kuchunguza zaidi kuhusu jinsia na utambulisho wa mtoto wao, anasema haikuwa safari rahisi kwani hapo mwanzo hakuwahi kupata majibu ya nini hasa kilisababisha mwanae kuzaliwa na upungufu huo.

Anakumbuka alipokutana na Dr. Simba wa hospitali ya taifa ya Muhimbili, ambaye alimfanyia vipimo kwa kuchukua mate ya mtoto huyo lakini baadaye majibu yalitoka wakishindwa kueleza ni jinsi gani, hakuwa na vichochoe vya kike wala kiume.

Walifanya kipimo cha Ultra sound wakamjibu wanaona maji tu tumboni.

Baada ya kuhangaika sana hospitali mbalimbali wakashauriwa kuendelea na vipimo kwa kadri anavyoendelea kukua.

”Tuliambiwa tumuache akue kidogo ndipo tumfanyie vipimo tena”anaeleza Sofia kwamba alipofikisha umri wa miaka saba walimpima tena na hakukuwa na taarifa ya tofauti.

Changamoto za malezi na makuzi

Bi Sofia alijipa moyo kwamba mwanae baada ya kukua huenda angeweza kubaini anajiskia kama mwanamke au mwanaume, lakini anakumbuka katika utoto wake alipendelea zaidi kumvalisha nguo za kiume, hadi siku moja Babi alipokuwa na umri wa miaka nane alipomwambia mama yake kuwa anatamani kuvaa gauni amechoka kuvalishwa suruali pekee.

”Mama nakuomba uninunulie gauni, we unanivalisha misuruali tu mimi…nikafurahi nikasema ah huyu mtoto kumbe anahomoni za kike..basi nikaendelea kumvalisha kama msichana.

Ukafika wakati Babi akaanza shule ya msingi ambapo alikutana na unyanyapaa hasa kutoka kwa watoto wenzake.”Nakumbuka kidato cha kwanza hadi cha nne, alisoma lakini kwa tabu, alirudi analia anasema wamenitukana, lakini nilijitahidi kumkumbatia na kumlida dhdi ya kejeli na kumtweza utu wake”

Fikira na mawazo yasiyokwisha

Nilipitia maumivu makali ya kihisia kwani nilijihoji maswali lukuki ambayo hayakuwa na majibu. Nilikosea wapi hata kuzaa mtoto akiwa hivi? Je ni vidonge vya majira nilivyotumia? nilitamani sana kujua nimechangia vipi mtoto wangu kuwa hivi? Nilikuwa naumia sana, nilikonda sana”

Faraja pekee ilikuwa ni mume wangu, na watoto wangu ambao hawakuchoka kututia moyo kuwa tusijali unyanyapaa wa baadhi ya watu.

”Baba alikuwa akipata safari za kikazi anamuombea ruhusa na kusafiri naye ili mradi tu Babi afurahi”

Nakumbuka kabla hajafariki dunia 2021 alisema angemuandika Babi kuwa mrithi wa mali zake zote kwa kuwa aliamini Babi ni mtoto wa ajabu ambaye aliweza kutuunganisha familia na kutufanya tuwe kitu kimoja na kupitia kwake kila mwanafamilia angenufaika na chochote ambacho baba angekiacha.

Na kweli alifanya hivyo na mwanangu ameweza kusimamia imani ambayo baba yake alimjenga kwayo.

Sofia anasema baadaye alipiga moyo konde ya kwamba huyu mtoto alimpata tu kutoka kwa Mungu basi hatajihangaisha tena kusononeka wala kujilaumu. Anasema polepole akaanza kuzoea hiyo hali lakini akijizatiti kumlinda mwanaye dhidi ya unyanyapaa.

Safari ya kumsaidia mtoto kujitambua haikuwa rahisi nayo….Sofia anasema walianza kuzungumza na Babi karibu kila mwezi alipoanza kukua na kuhoji maswali mengi hasa kwa nini yeye yuko hivyo.

”Tulimwambia Babi wewe si mwanaume wala mwanamke, lakini ni mipango ya Mungu tunaomba uikubali”anasema Babi aliikubali kwa muda mfupi tu zipo nyakati nikiwa jikoni napika nasikia anakuja na kuniuliza ”Mama hivi mimi ni nani? mimi sijaelewa…na kadri siku zilizozidi kwenda anazidi kujitambua na kuuliza maswali mengi sana. Aliwahi kutuuliza na baba yake hivi nasoma ili niwe nani? wenzangu wataolewa na kuoa, mimi ntakuwa mtu gani? aliwahi kuniambia ninaweza kujichinja mimi….lakini tuliita kaka zake na dada zake tukakaa kikao kwa ajili yake kumjenga na kumtia moyo…ilinisononesha japo nilijikaza.

Sitasahau siku moja kuna watu mtaani walifanya jaribio la kutaka kumvua nguo ili wamuone mwanangu, hii ni baada ya kuwa wanamtania kila mara kwa majina kama Jike dume. Niliripoti polisi wakaitwa na kuonywa.

Umuhimu wa kujikubali

.

Chanzo cha picha, Babi

Maelezo ya picha, Mama yake Babi bi Sophia

Bi Sofia anamkumbuka Daktari Wangwe, mtaalamu wa magonjwa ya wanawake kama mtu wa mwisho kumtia moyo baada ya kumueleza kuwa hali aliyo nayo Babi ni hali ya kimaumbile inatokea na kumuonya kuwaza vibaya kwa namna yoyote kwa sababu haya ni mambo ya maumbile tu na akamuelezea kiundani inakuwaje hata mwanae akawa hivyo, jambo analosema alijiskia ametua mzigo mkubwa kwa kutambua kuwa maumbile ni mambo ya Mungu na si yeye aliyesababisha mwanae kuwa wa jinsi tata.

Anakumbuka pia Babi alipata ushawishi kutoka kwa rafiki zake kwamba ajitokeze katika majukwaa ya kisiasa na kugombea kuwa kiongozi ili mradi apate nafasi kufanya kitu anachokipenda na kujieleza siri yake aliyokaa nayo kwa miaka mingi.

Julai 23, 2020 aliitangazia dunia kwamba yeye si mwanamke wala mwanaume.

Baba yake alimuunga mkono sana, alikwenda naye kwenye kampeni na hata kwenda huko kwenye uchaguzi.

Babi alionekana mwenye furaha sana na alibadilika na kupata nguvu sana tangu alipoanza kusema kuhusu ulemavu wake. Kama mama yake nilijisikia amani sana baada ya Babi kujitangaza, niliona namna ambavyo jamii ilipokea kwa hisia mseto.

Tulipokea simu nyingi sana kutoka kwa watu mbalimbali nchini Tanzania wakimpongeza na kumpa pole na kumuombea dua njema, lakini zaidi sana nilistaajabu kupokea simu za watu walio na hali kama ya Babi, ambao wamemtafuta wakimpongeza kwa uamuzi wa ujasiri kujitangaza. Wapo waliosema hawawezi kujitangaza kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo unyanyapaa na kutoeleweka na jamii.

Bi Sofia anasema wakati huo alijifunza kwamba kuna kundi la watu kwenye jamii linaishi maisha ya ukiwa na ya kujificha wakishindwa kujitokeza kulingana na mazingira kuwabana.

Hawana wa kumwambia, na huenda wanazo ndoto kubwa katika maisha yao lakini hawawezi kuthubutu kujitokeza kwa sababu wanaogopa kutengwa na kujikuta wanajitenga wenyewe.

Bi Sofia anasema kwa imani yake aliamini ipo siku ingefahamika kwamba Babi ana hisia za kike na ingewezekana kufanyiwa upasuaji na angekaa vizuri…ilikuwa tofauti ”Daktari alituambia bado haonekani kuwa na vichocheo vya kike au kiume,na vipimo vinaonesha hana viungo vya ndani vya uzazi ambavyo vingemsaidia kuja kupata mtoto siku za usoni.”ilikuwa taarifa nzito sana” anasema..

Uhusiano wa kimapenzi

Babi John

Chanzo cha picha, Babi John

Maelezo ya picha, Babi John Musamba mwanaharakati wa haki za binadamu masuala ya jinsia tata

Anasema ”Nimekwishapokea wachumba mimi…mmoja ndugu zake walimwambia, lakini hakuamini.

Ukikutana na Babi, ana mwonekano mzuri na haiba ya kike. Si rahisi sana kubaini kama ana kasoro yoyote mwilini kama hautaelezwa na kuthibitishiwa, ndivyo ilivyokuwa kwa wanaume wengi ambao Bi Sofia anasema wapo waliovutiwa na kutaka kuanzisha mahusiano na BaBi.

Anazungumza akitabasamu akikumbuka namna baadhi ya vijana waliofika nyumbani na kuzungumza na wazazi wa Babi Kuhusu utaratibu wa kumposa Babi kwa kufuata mila za watu wa Serengeti. Ni kitu kizuri lakini sikuona sababu za kuwadanganya, tuliwaeleza ukweli kuwa haiwezekani.

Lakini nilifurahia mno, nilijiskia kama mzazi mwingine anavyojiskia pale anapopata ugeni wa kuposa mtoto wao. Walau na mimi nimeonja hiyo furaha japo isingewezekana.

Akaja kijana mwingine ambaye alikuwa rafiki sana wa kaka yake Babi.

”Aggrey, kijana wa kichagga alikataa kabisa Babi alipomweleza kwamba yeye ”hayuko hivyo”asingeweza kuolewa. Kijana huyo alituhakikisha amempenda sana Babi na angependa tumruhusu amuoe. Tulizungumza naye alisikitika mno, aliondoka lakini hadi leo haachi kumuonesha upendo Babi.

“Mimi ninachojua Babi hunihakikishia kwamba hajiskii chochote,hajiskii hisia za kutamani kike au kiume, anasema Sophia.

Uwezo wa kustahimili changamoto

Bi Sofia anajivunia watoto wake wote watano ambao hawajawahi kuwa mzigo kwake.Anasema anamshukuru Mungu sana kwamba watoto wake wamekuwa sababu ya kuwa wamoja na kushikamana sana kama familia.

Hata baada ya kifo cha Mume wake, hajawahi kusononeka kwani watoto wake wamekuwa naye karibu na kumfariji. Anasema ”ukiwa na mtoto kama huyu umemficha maana yake umempoteza”…anasema anatamani sana nchini Tanzania jamii ingewatambua watu wa jinsi tata wakati wa sensa ya watu na makazi.

”Anasema kipindi cha sensa maafisa walifika nyumbani na walitukuta Babi alijieleza mwenyewe nao wakaandika,walimtambua kama mwanamke lakini wakachukua maelezo ya jinsi tata.”

Anasema ameona namna anavyoitwa na watu mbalimbalimbali wa ndani na nje ya Tanzania.

”Eti anaitwa kuhudhuria mikutano Kenya,Uganda na hata Ulaya huko yaani ninashangaa kabisa ninajiskia vizuri.Kitendo cha kujitambulisha kimenipa uhuru,ninajiskia vizuri.

”Sikutarajia huyu mtoto anapigiwa simu kutoka Canada, Afrika Kusini,na hata Shelisheli yaani wanamuita kama nani? ninamshangaa Mungu”.

Kutokana na Babi kutumia mitandao ya kijamii, Bi Sofia amekuwa akikutana na watu wanaotumia mitandao na kumuona katika kurasa za Babi anasema hajiskii vibaya tena kuwaeleza kuwa ni mwanae na anajivunia alivyo ndivyo Mungu alivyomuumba. Pia anashauri wazazi kutoficha watoto wenye ulemavu.

Anasema anaona nuru mbele na matumaini kwamba ipo siku jamii itawaelewa watu wa jinsi tata na kuwa msaada kwao. Anaomba serikali Iweke sheria zinazowatambua watu kama mwanae.

.

Chanzo cha picha, Babi

Maelezo ya picha, Wazazi wake Babi

Daktari aeleza sababu za hali kama hii

Miaka kadhaa iliyopita BBC ilizungumza na daktari wa afya ya uzazi wa wanawake nchini Tanzania Dkt Berno Mwambe, ambaye aliielezea hali hii kwa Kiingereza hufahamika kama Disorder of Sex Development (DSD). Hii ni hali ya viungo vya uzazi kukosa kukomaa.

Anasema kuna aina nyingine ya ugonjwa unaojulikana kama Mayer-Rokitansky-Kuster-Hauser (MRKH) syndrome, ambao unahusu mwanamke kukosa viungo vyote vya sehemu za uzazi.

Daktari anaongeza kuwa hali hii inatokea mara chache sana kwa watoto wa kike, kwa wastani mtoto 1 Kati ya 4,500 wanaozaliwa.

Hali hii inasababishwa na mabadiliko katika vinasaba vinavyohusika katika ukuaji wa viungo vya mwanamke.

Na je marekebisho yanaweza kufanywa? Dkt Berno anasema kuwa inategemea usugu wa hali yenyewe.

Kwa mtu ambaye viungo vyake vya uzazi havijakua vizuri, basi mtu anaweza kufanyiwa upasuaji wa kurekebisha.

Kwa mtu ambaye hana kabisa kwa mfano Bi Musamba, matibabu yake yanakuwa magumu hususan kwenye muundo na tamaduni za jamii za kiafrika zilivyo.

Aidha daktari anasema nchi za ng’ambo hufanya marekebisho na hata kumpandikiza mwanamke mji wa uzazi wa mtu mwingine na hata kutengeneza uke. Mwathirika anaweza kufanikiwa hata kushika na kuubeba ujauzito baada ya upasuaji na tiba ya homoni.

Imeandikwa na Martha Saranga na kuhaririwa na Florian Kaijage