Waraka wa TEC waibua changamoto saba za imani

Moshi. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), limetoa waraka wenye ujumbe wa Kwaresma kwa mwaka 2025, likitaja changamoto saba za imani iki-wamo mdororo wa kiuchumi, kuibuka kwa utanda-wazi na vikundi vya unabii mamboleo.

Mbali na masuala hayo,  waraka huo uliotolewa na maaskofu 40 wa kanisa hilo wakiongozwa na Rais wa TEC, Askofu Wolfgang Pisa, pia umegusia uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani utakaofanyika mwaka huu.

Kuhusu uchaguzi, maaskofu wametoa wito kwa wanasiasa na umma kujenga utamaduni wa uadilifu katika kuheshimu Katiba na sheria, wakitaka wanasiasa kutotumia njia za mkato kupata uongozi wa kisiasa.

Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) yamejiwekea utaratibu wa kutoa waraka wa kichungaji wakati wa Kwaresima na pale kunapokuwa na haja ya kufanya hivyo kama ilivyo-tokea mwaka 2018.

TEC limekuwa likitoa waraka wa ujumbe wa Kwaresma takribani kila mwaka, lakini pale in-apotokea haja ya kufanya hivyo nje ya masuala ya kiimani hufanya hivyo, kama ilivyofanyika mwaka 2023 wakati wa Mkataba wa DP World.

Kuhusu uchaguzi mkuu 2025

Maaskofu katika waraka wamewaalika waamini ku-shiriki katika kila jambo jema kama raia, kutii sheria zilizowekwa kihalali na mamlaka, kuishi maisha ya uadilifu na kushiriki katika shughuli za kisiasa kama wajibu wa kiimani.

“Lengo la ushiriki huu ni kusaidia kujenga jamii iliyo bora zaidi kwa sababu ili kuunda maisha ya kisiasa yaliyo ya kweli ya binadamu, hakuna lililo bora zaidi kuliko kustawisha ndani ya watu hisia za haki, upen-do na manufaa kwa wote,” umeeleza waraka huo.

“Mwaka huu 2025 Taifa letu litakuwa katika kipindi mahususi cha uchaguzi wa viongozi ambao watape-wa dhamana ya kulinda, kutetea na kusimamia ust-awi wa haki,” unaeleza waraka huo wa maaskofu wenye kurasa 44 ambao Mwananchi umeuona leo Ijumaa, Machi 7, 2025.

“Tunapenda kuwaalika Wakristo wote na watu wenye mapenzi mema kutekeleza zoezi hili kwa umakini na uadilifu mkubwa, tukitambua kila mwananchi mwenye haki ya kupiga kura, anatakiwa kufanya hivyo kwa kadri ya Katiba.

“Katika mazingira ya uchaguzi wa kisiasa, mara nyingi watu wengi hujikuta wapo katika changa-moto hata za kupoteza msimamo wao wa imani. Hupenda kutumia njia za mkato kama vile ushiriki-na, uongo na rushwa kupata uongozi,” wamesema maaskofu katika waraka huo na kuongeza:

“Wanasahau kuwa kila kiongozi hutoka kwa Mungu, maana sauti ya watu ni sauti ya Mungu. Hivyo wanatakiwa kutegemea nguvu za Mungu na kuwa tayari kuwasikiliza wananchi wote kwa manufaa ya nchi nzima ya Tanzania.”

TEC limesema: “Tunatoa ushauri kwa viongozi wa kisiasa tukisisitiza utoaji wa fursa ya kusikilizwa hata wale wachache wenye mawazo tofauti. Hii itatusaid-ia kukuza na kuheshimu utofauti wa kufikiri kwa manufaa ya nchi, kupinga chuki na kujenga umoja.

“Katika demokrasia, ushiriki wa umma katika siasa huleta maendeleo, kujenga na kustawisha umoja na mshikamano kwa njia ya mgawanyo sawa wa rasili-mali za Taifa. Ujenzi wa maisha bora na ustawi wa jamii ni jukumu letu sote.”

“Tunaalikwa kujenga utamaduni wa uadilifu katika kuheshimu Katiba na sheria zinazotuongoza,” unasisitiza waraka huo unaoongozwa na neno kuto-ka Wakorintho wa kwanza 16:13 unaosema: “Simameni imara katika imani.”

Changamoto dhidi ya imani

Waraka umezungumzia changamoto saba zi-nazoikabili imani ya Kikristo ambayo ni pamoja na kupungua kwa washiriki kunakosababishwa na mambo mbalimbali na kufanya taratibu kanisa kuwa ni la wazee zaidi.

“Kanisa taratibu linakuwa la wazee. Vizazi vichanga mara nyingi hutanguliza uhuru binafsi, ubinafsi na imani mchanganyiko. Kuenea kwa propaganda za upotoshaji imani na mitizamo tofauti kupitia mitandao ya kijamii huwaweka vijana kwenye safu nyingi za mitazamo ya ulimwengu na kuwafanya kuvutwa na njia mbadala za kiroho.

“Mabadiliko ya kiuchumi na maisha yanachangia kupungua kwa washiriki. Mahitaji ya maisha ya kis-asa hufanya iwe changamoto kwa watu binafsi kujit-olea kwa shughuli za kawaida za kanisa,” unaeleza waraka huo.

Pia unaeleza: “Kuenea kwa uchumba sugu na ndoa za dini tofauti husababisha umoja na muunganiko wa kanisa kupungua.”

Waraka umezungumzia upungufu wa mapadri na makasisi kuwa ni tatizo kubwa kwa kanisa hilo duni-ani kote na kwamba, upungufu wa mapadri una athari kubwa kwa kanisa kutimiza kazi zake kuu za kikuhani duniani.

“Mahitaji ya maisha ya kikasisi, ambayo ni pamoja na useja, kujitolea maisha yote yanaonekana kuwa ya kutisha na yasiyopendeza kwa baadhi ya watu. Changamoto hizi hukatisha tamaa vijana kujitoa kwa kuogopa uzito wa upadri kama njia ifaayo,” waraka wa TEC unaeleza.

Kashfa unyanyasaji watoto

Waraka umeelezea suala la kashfa za unyanyasaji wa kijinsia na dhidi ya watoto kuwa zimekuwa na athari kubwa na za kudumu kwa taasisi nyingi za kidini na familia, hivyo kusababisha kupoteza uaminifu na kutathimini jukumu la dini.

“Athari za muda mrefu za kashfa za unyanyasaji wa kijinsia zinaonekana si tu ndani ya jumuiya ya kikani-sa, lakini pia ndani ya jamii kwa ujumla. Kashfa hizi zinahitaji uwajibikaji na mageuzi katika jumuiya za kikanisa na familia,” linaeleza baraza hilo.

Mdodoro wa kiuchumi

Maaskofu wamesema mdodoro wa kiuchumi ni changamoto kubwa ambayo makanisa na mashirika ya kidini yamekuwa yakipambana nao katika miaka ya hivi karibuni nchini na duniani.

“Mdororo wa kiuchumi ni matokeo mchanganyiko wa mambo yanayoathiri uwezo wao wa kuendeleza shughuli, kudumisha miundombinu na kutimiza dhamira yao.

“Kupungua kwa usaidizi wa kifedha kunachangiwa na ukweli kwamba, vizazi vizee ambavyo vina mwelekeo wa kuchangia mara kwa mara vinapun-gua kwa idadi.

“Mdororo wa kiuchumi au kutokuwa na uhakika na kipato cha kiuchumi husababisha kupungua kwa mapato yanayoweza kutumika na kusababisha watu binafsi kupunguza utoaji wa misaada ikiwamo ni pamoja na taasisi za kidini.

“Taasisi za kidini zinakabiliwa na ushindani wa usaidizi wa hisani na mashirika mengine yasiyo ya kidini. Wafadhili wengine huja na shinikizo la kufu-ata mrengo usio wa kiimani,” inaelezwa katika waraka ambao gazeti hili limeuona.

Utandawazi, unabii mamboleo

Waraka pia umezungumzia kuibuka kwa watu na vikundi vya unabii mamboleo na mafundisho yao kuvutia watu kwa kuahidi mafanikio, ukieleza hiyo ni changamoto kubwa kwa imani ya kweli.

“Mafundisho ya Kanisa Katoliki kuhusu masuala ya kimaadili na kijamii yanatofautiana sana na yale ya imani nyingine,” unaeleza waraka.

TEC linaeleza utandawazi huleta maoni tofauti ku-husu kanisa, teolojia na huduma ya kichungaji na kwamba, kanisa halinakili tu mbinu na njia za mifu-mo mingine ya kijamii na falsafa, bali lina maisha ambayo ni zaidi ya hayo.

“Kanisa linakuwa la kidunia linaposhushwa hadhi na kuwa shirika la kijamii kama mashirika mengine mengi ambayo yapo katika jamii. Kanisa ni taasisi ta-katifu iliyoanzishwa na Roho Mtakatifu,” umaeleza waraka na kuongeza:

“Kwa bahati mbaya, baadhi ya watu leo wana-lichukulia kanisa kama shirika la lazima lenye man-ufaa kwa jamii tu, na jukumu lake linathaminiwa kulingana na manufaa ya kijamii pekee.”

Waraka unasema: “Kuna wengine pia ambao ha-waoni jukumu la kinabii na utakaso wa kanisa amba-lo linajumuisha utakaso wa mwanadamu na ulim-wengu wote. Badala yake, wanakubali tu kanisa ka-ma nyenzo ya mapato na mapambo.”

Kupoteza dhana ya dhambi

Waraka umegusia kile ilichosema ni kupoteza dhana ya dhambi ambako kunaleta kutokujali ukweli kwamba matendo ya uovu humchukiza Mungu, huharibu uhusiano pamoja naye na kuwa matokeo yenye uharibifu kwa jamii.

“Udhihirisho wa upotevu huu wa maana ya dhambi unaonekana katika kukataa ukweli wa maadili. Wa-kati maswali ya maadili mema na mabaya yanaon-ekana kwa uthabiti, ufahamu wa dhambi ya mtu na matokeo yake hupungua.

“Kutupiliwa mbali huku kwa sheria ya maadili, hatimaye kunaweka wokovu wa mtu binafsi hata-rini. Ni lazima tutambue uzito wa dhambi ikiwa kweli tunathamini zawadi ya Kristo ya msamaha na utapanisho,” unasisitiza waraka.