Wapishi, walimu wanolewa matumizi ya nishati safi

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikilenga kuhakikisha Watanzania wanne kati ya watano wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034, elimu kuhusu matumizi ya nishati hiyo kwa walimu wa shule na wapishi inaendelea kutolewa.

Katika juhudi hizo, walimu na wapishi kutoka shule mbalimbali za msingi katika Manispaa ya Temeke, jijini Dar es Salaam, wamepatiwa mafunzo ya siku moja yanayolenga kuwawezesha kuachana na matumizi ya nishati chafu shuleni.

Mafunzo hayo yameandaliwa na Shirika la Chakula Duniani (WFP) kwa lengo la kuboresha afya za wanafunzi katika shule zenye utaratibu wa lishe shuleni.

Akizungumza leo Alhamisi, Machi 27, 2025, wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo, Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Marianne Young amesema kuwa ubalozi huo utashirikiana na mashirika mbalimbali nchini kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala.

“Kupitia ubalozi wa Uingereza hapa nchini, tunataka kuona watu wanaishi kwenye mazingira salama. Inawezekana kufanikisha hilo endapo tutapunguza matumizi ya kuni na mkaa. Hii pia itachangia kuboresha lishe za watoto wetu shuleni,” amesema Balozi Young.

Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa WFP, Ronald Tran Bahuy amesema wameona jitihada za Serikali ya Tanzania katika kuhamasisha wananchi kuachana na matumizi ya nishati chafu na kutumia nishati safi.

“Tumeanzisha mradi wa kusapoti matumizi ya nishati safi ya kupikia shuleni, ambapo tutaanza na shule 50 kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Kigoma, Dodoma na Tabora. Mradi utaanzia Dar es Salaam katika Shule ya Msingi Kibasila,” amesema Bahuy.

Ameongeza kuwa jitihada hizo zinalenga pia kuboresha lishe shuleni, kwani tangu kuanzishwa kwa utaratibu wa lishe shuleni, kumekuwa na ongezeko la wanafunzi wanaojiandikisha, kuboreka kwa ufaulu na kupungua kwa utoro.

Ofisa Elimu Taaluma wa Mkoa wa Dar es Salaam, Geofrey Kituye,amesema mafunzo hayo ni muhimu, kwani Serikali pekee haiwezi kufanikisha kampeni ya matumizi ya nishati safi bila ushirikiano wa wadau mbalimbali.

“Sisi kama mkoa tumeanza kuunga mkono juhudi hizi tangu mwaka jana kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali. Kinachotufanya kuwa hapa leo ni sehemu ya utekelezaji wa mikakati ambayo Serikali tayari imeshaweka kuhusu matumizi ya nishati safi,” amesema Kituye.

Hata hivyo, amesema kuwa bado kuna mwitikio mdogo wa matumizi ya nishati safi, huku akitoa takwimu za shule 610 za Serikali jijini Dar es Salaam kuwa kati ya hizo, 37 tu sawa na asilimia 12 zinatumia nishati safi, 22 (asilimia 8) zinatumia gesi na kuni, huku shule 147 (asilimia 42) bado zinatumia kuni na mkaa.

Akizungumza kwa niaba ya walimu wenzake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Likwati, Innocent Balasi amesema mafunzo hayo yamewapa mwanga mpya kuhusu matumizi ya nishati safi katika kupikia shuleni.

“Nimejifunza umuhimu wa kuhama kutoka matumizi ya kuni na mkaa kwenda kwenye nishati mbadala. Faida zake ni nyingi, ikiwemo kuokoa muda, kutunza afya na kuboresha upatikanaji wa lishe shuleni,” amesema Balasi.

Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Umoja, Matrina Daudi, amepongeza mafunzo hayo, huku akivutiwa zaidi na majiko yanayotumia nishati ya umeme yaliyooneshwa katika mafunzo hayo.

“Majiko haya yanapika kwa haraka na ni salama zaidi, hivyo yatasaidia sana kupunguza changamoto zinazotokana na matumizi ya kuni na mkaa,” amesema Matrina.

Mafunzo hayo yanatarajiwa kusaidia kuongeza uelewa wa matumizi ya nishati safi katika shule mbalimbali nchini, huku Serikali ikiendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha azma ya matumizi ya nishati safi inatimia ifikapo mwaka 2034.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *