Dar es Salaam. Miongoni mwa mbinu za ukuaji endelevu wa biashara kwa wafanyabiashara na wawekezaji ni maarifa ya kifedha yanayochochea ukuaji huo.
Ili kutekeleza hilo, Benki ya Absa Tanzania imekuja na mkutano maalumu wa asubuhi kwa ajili ya uwekezaji wenye lengo la kuwawezesha wateja wa kampuni na taasisi za kifedha kupata maarifa na suluhisho za kifedha.
Mkutano huo uliofanyika leo Alhamisi Mei 8, 2025 jijini Dar es Salaam ambapo umehudhuriwa na zaidi ya wateja 100 wa kibiashara kutoka sekta mbalimbali nchini, ambapo wataalamu waandamizi wa masuala ya uwekezaji kutoka Benki ya Absa Tanzania na Absa Group wamewasilisha mada zinazogusa masuala ya soko la mitaji kwa njia ya mikopo, ubia wa kimkakati na fursa za ununuzi na muunganisho wa kampuni ukanda wa Afrika Mashariki.
Akizungumza wakati wa ufunguzi, Mkurugenzi Mtendaji wa Absa Tanzania, Obedi Laiser amesema benki imejikita katika kusaidia wateja wake kuwa na uelewa mpana wa mazingira ya uchumi yanayobadilika kwa kasi.

“Lengo letu ni kuiwezesha Afrika ya kesho, pamoja, stori moja baada ya nyingine amesisitiza kuwa huduma za uwekezaji za Absa zinalingana na mazingira ya ndani huku zikinufaika na mtandao mpana wa benki hii barani Afrika, bila kusahau kaulimbiu yetu ni ‘Stori yako ina thamani‘
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kitengo cha Wateja wa Mashirika wa Absa Tanzania, Nellyana Mmanyi amesema benki hiyo ina uwezo mpana wa kutoa huduma zinazokidhi mahitaji ya wateja kwa wakati husika.

“Huduma zetu zinaanzia katika ushauri wa kifedha, ufadhili wa miradi na mali, hadi katika masoko ya mitaji. Tunachokitoa si bidhaa tu, bali ni ushirikiano wa kimkakati unaozingatia hali halisi ya kufanya biashara Tanzania na Afrika kwa ujumla,” amesema.