
Wapiganaji wa harakati ya muqawama ya Hizbullah ya Lebanon wametangaza utiifu wao kwa kiongozi mpya wa harakati hiyo huku wakisisitiza kuwa maadui wana hofu kubwa kutokana na ushujaa wa wapiganaji wa muqawama na silaha zao.
Katika ujumbe kwa katibu mkuu mpya wa Hizbullah Sheikh Naim Qassem siku ya Jumamosi, wapiganaji wa Hizbullah wamesema: “Tunatangaza, kwa niaba ya makundi yetu yote ya jihadi na kutoka moyoni mwa kila mpiganaji wa muqawama wa Kiislamu, utiifu wetu mpya kwako.”
Wapiganaji hao waliapa kuendelea kufuata njia ya kiongozi wa zamani wa kundi hilo, Shahidi Sayyed Hassan Nasrallah, ambaye aliuawa shahidi wakati wa mashambulizi ya anga ya utawala wa kigaidi wa Israel dhidi ya mji mkuu wa Lebanon Beirut mwishoni mwa Septemba.
Wameahidi kuendelea kujitahidi ili kufikia malengo ya Shahidi Nasrallah katika “kusaidia waliodhulumiwa na kulinda wasia wake wa kuwa ngao inayolinda watu wetu na umma mpendwa, kulinda mafanikio ya damu ya mashahidi, na kusonga mbele kwa busara katika njia ya muqawama, ukombozi wa nchi, na kufukuzwa wavamizi.”
Aidha wapiganaji wa Hizbullah wamesema hivi sasa wanamiliki nguvu za kutosha kwa ajili ya kukabiliana na maadui wa muqawama. Kauli hiyo imekuja huku utawala vamizi wa Israel ukiendeleza vita dhidi ya Lebanon ambapo hadi sasa umeua zaidi ya watu 3,100 tangu Oktoba mwaka jana.
Hizbullah imekuwa ikilipiza kisasi dhidi ya uchokozi huo kwa kuanzisha mamia ya operesheni zilizofanikiwa dhidi ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na wanajeshi wa Israel wakijaribu bila mafanikio, kusonga mbele katika maeneo ya kusini mwa Lebanon.