
Wapiganaji wa harakati ya Muqawama ya Hizbullah ya Lebanon wametangaza utiifu wao kwa kiongozi mpya wa harakati hiyo huku wakisisitiza kuwa maadui wana hofu kubwa kutokana na ushujaa wa wapiganaji wa harakati hiyo na sialaha zao.
Katika ujumbe wao kwa Katibu Mkuu mpya wa Hizbullah, Sheikh Naim Qassem, siku ya Jumamosi, wapiganaji wa Hizbullah walisema: “Tunatangaza, kwa niaba ya makundi yetu yote ya Jihadi na kutoka moyoni mwa kila mpiganaji wa Muqawama wa Kiislamu, utiifu wetu kwako.”
Wapiganaji hao wameapa kuendelea kufuata njia ya kiongozi wa zamani wa harakati hiyo, Shahidi Sayyed Hassan Nasrullah, ambaye aliuawa shahidi katika mashambulizi ya anga ya utawala wa kigaidi wa Israel dhidi ya mji mkuu wa Lebanon, Beirut, mwishoni mwa Septemba mwaka huu.
Wameahidi kuendeleza jitihada za kutimiza malengo ya Shahidi Nasrullah katika “kuwasaidia watu wanaodhulumiwa na kulinda wosia wake wa kuwa ngao inayolinda watu wetu na Umma pendwa, kulinda mafanikio ya damu ya mashahidi na kusonga mbele kwa busara katika njia ya Muqawama, ukombozi wa nchi na kufukuzwa kwa wavamizi.”
Aidha wapiganaji wa Hizbullah wamesema, hivi sasa wana nguvu za kutosha kukabiliana na maadui wa Muqawama.
Kauli hiyo imekuja huku utawala vamizi wa Israel ukiendeleza vita dhidi ya Lebanon ambapo hadi sasa umeua zaidi ya watu 3,100 tangu Oktoba mwaka jana.
Hizbullah imekuwa ikilipiza kisasi dhidi ya uchokozi huo kwa kufanya mamia ya operesheni zilizofanikiwa dhidi ya ardhi ya Israel huku wanajeshi wa utawala huo ghasibu wakijaribu kusonga mbele katika maeneo ya kusini mwa Lebanon bila mafanikio.