
Gaza. Baada ya miezi 15 ya kukimbia makazi yao, wakazi wa Gaza nchini Palestina wameanza kurejea katika eneo lao kama sehemu ya utekelezaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Hamas na Jeshi la Israel (IDF).
Vita dhidi ya Hamas vimegharimu maisha ya Wapalestina 47,306 na kujeruhi 111,483 tangu Oktoba 7, 2023.
Leo asubuhi, Jumatatu Januari 27, 2025, misururu ya Wapalestina imeonekana wakitembea kwa miguu kuelekea Mji wa Gaza, huku wengi wao wakiwa wamebeba mabegi na mali zao, ikiwemo magodoro, kupitia Korido ya Netzarim iliyozinduliwa na vikosi vya IDF.
Awali, IDF ilitangaza kuwa Wapalestina walioyakimbia makazi yao wangeweza kupita Mtaa wa al-Rashid na Mtaa wa Salah al-Din kuanzia saa 11:00 asubuhi hadi 1:00 asubuhi. Mohammad Ahmed, mmoja wa Wapalestina waliorejea, amesema, “Nitaanza kuyajenga upya makazi yangu kwa kutumia matofali. Tutaanza kwa kuondoa vifusi na kuujenga upya mji wetu.”
Hani Mahmoud, mwandishi wa Al Jazeera, ameelezea furaha ya Wapalestina waliorejea kwa kusema, “Hatujawahi kuona furaha hii katika kipindi cha miezi 15,” na kuongeza kuwa kurejea kwao ilikuwa ni ushindi kwao na kwa Hamas.
Zaidi ya watu 50,000 wamepoteza maisha katika kipindi cha vita, na zaidi ya 110,000 wamejeruhiwa. Wapalestina wamesema kuwa kurejea kwao ni ushindi baada ya kupoteza makazi, hospitali, na miundombinu.
Kundi la Hamas liliuita uamuzi wa Israel kama ushindi, likisema ni ishara ya kushindwa kwa jaribio la kutwaa ardhi ya Wapalestina kwa mabavu. Tangu vita kuanza, zaidi ya milioni 2.3 walilazimika kuyakimbia makazi yao kutokana na uvamizi wa ardhini na vikosi vya IDF.
Jana, Jumapili, vikosi vya Israel vilikataa kuwaruhusu raia kusogelea au kupita katika Korido ya Netzarim kuingia eneo la Gaza, jambo lililosababisha vurugu na vifo vya watu wawili.
Uamuzi wa kuwazuia na kuwaua raia hao ulisababishwa na kitendo cha Hamas kugoma kumwachia mateka mmoja wa kike, Arbel Yehud, Jumamosi.
Hata hivyo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar imetoa taarifa kuwa baada ya kuingilia kati, Hamas ilikubali kumwachilia Yehud na mateka wenzake wawili.
Naibu Mkurugenzi Mstaafu wa Taasisi ya Wamarekani Uarabuni, Omar Baddar, amesema alikuwa na maswali kuhusu iwapo IDF ingewaruhusu raia kuingia kwenye makazi yao eneo la Gaza bila kuwaachia mateka hao. Hata hivyo, jambo hilo lilijidhihirisha baadaye baada ya Hamas kukubali kuwaachia huru.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.