Wapalestina 55 wauawa katika mashambulizi mapya ya Israel huko Gaza

Mashambulizi ya mara kwa mara ya Israel dhidi ya Gaza, ikiwemo Jabalia kaskazini mwa Gaza, yamesababisha vifo vya Wapalestina 55 zaidi.

Wizara ya Afya ya Gaza ilisema Jumanne kwamba zaidi ya Wapalestina 300 pia wamejeruhiwa katika saa 24 zilizopita.

Katika moja ya mashambulio mabaya zaidi ya utawala wa Israel huko Gaza, familia nzima iliuawa katika shambulio la bomu dhidi ya nyumba yao karibu na mji wa kusini wa Khan Yunis.

Takriban Wapalestina 12 wameuawa na ndege za kivita za utawala huo karibu na kambi ya wakimbizi ya Jabalia.

Helikopta za Israel zimeshambulia ardhi ya Wapalestina ya kilimo kusini mwa eneo la Maghazi katikati mwa Gaza.

Hapo awali, shirika la habari la Palestina Wafa liliripoti kuwa Wapalestina wanane waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika shambulio la anga la Israel lililolenga kundi la raia katika mji wa Gaza na mahema mawili ya waliokimbia makazi yao huko Khan Yunis.

Mtandao wa televisheni ya Lebanon al-Mayadeen umeripoti kuwa wanajeshi wa Israel wamefanya mashambulizi ya anga kwenye kambi ya Nuseirat katikati mwa Gaza.

Kwa mwaka moja sasa jeshi katili la Israel linasonga mbele na mashambulizi yake ya mara kwa mara katika Ukanda wa Gaza uliozingirwa sasa zaidi ya mwaka mmoja katika vita vya mauaji ya kimbari.

Mashambulizi ya utawala dhalimu wa Israel dhidi ya Gaza yalianza Oktoba mwaka jana, na hadi sasa utawala huo umeua karibu Wapalestina 43,000. Zaidi ya wengine 98,000 pia wamejeruhiwa tangu wakati huo.