
Wizara ya Afya ya Palestina imetangaza kuwa watu 39 wameuawa shahidi na 123 wamejeruhiwa katika mashambulizi ya kinyama ya utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza katika muda wa saa 24 zilizopita.
Ukijumuisha na waliouawa shahidi siku iliyopita, idadi ya Mashahidi wa mashambulizi ya jeshi la utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza tangu tarehe 7 Oktoba 2023 imefikia watu 43,508 na idadi ya waliojeruhiwa imefikia watu 102, 684.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, raia wasiopungua watano wameuawa shahidi katika shambulio la utawala wa Kizayuni dhidi ya shule moja huko Gaza.
Wanajeshi hao wa utawala wa Kizayuni wamelenga pia shule ya Fahd al-Sabah, makazi ya wakimbizi wa Kipalestina huko mashariki mwa mji wa Gaza.
Wazayuni wameshambulia pia kwa mabomu eneo la Abu Hajir, kaskazini mwa kambi ya El Brij, katikati ya Ukanda wa Gaza.
Ndege za kijeshi za utawala wa Kizayuni zimeshambulia pia kwa mabomu mahema ya wakimbizi wa Kipalestina kusini mwa Ukanda wa Gaza na kusababisha vifo vya watu wasiopungua watatu na kuwajeruhi wengine watano.
Tangu tarehe 7 Oktoba 2023, na kwa uungaji mkono kamili wa nchi za Magharibi, utawala wa Kizayuni umekuwa ukifanya mauaji makubwa ya umati dhidi ya watu wasio na ulinzi na madhulumu wa Palestina katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Kimya cha jamii ya kimataifa na taasisi za kutetea haki za binadamu kwaa jinai za utawala ghasibu wa Israel, kimesababisha kuendelea mauaji ya wanawake na watoto wa Kipalestina yanayofanywa na mashine ya vita ya utawala haramu wa Kizayuni.
Katika kipindi hiki, asilimia 70 ya nyumba na miundomsingi ya Ukanda wa Gaza imeharibiwa vibaya, na mzingiro na hali mbaya ya kibinadamu, pamoja na njaa kali ambayo haijawahi kushuhudiwa, vinatishia maisha ya wakazi wa eneo hilo.