Waongoza watalii mguu sawa kuelekea msimu mpya wa utalii 

Arusha. Wanachama wa umoja wa waongoza watalii nchini (TTGA), wamekutana jijini Arusha kujadili namna ya kuuanza msimu mpya wa utalii unaotarajia kuanza Juni mwaka huu.

Wanachama hao ambao wamekutana leo Jumapili Mei 11, 2025, miongoni mwa mambo waliyojadili ni pamoja na changamoto za msimu uliopita na wamewasilisha changamoto zao kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Pindi Chana na kuomba utatuzi.

Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na ukosefu wa bima za afya sambamba na ubovu wa miundombinu ya ndani ya hifadhi hasa barabara zilizoharibiwa na mvua za masika.

Akizungumza katika mkutano huo, Katibu wa waongoza watalii Robert Max ameiomba serikali kuwarudishia mpango wa bima za afya zilizositishwa hivi karibuni.

“Tuaomba serikali kurudisha mpango wetu wa bima za afya, hali imekuwa ngumu ya kupata matibabu hii inahatarisha maisha yetu kutokana na mazingira ya kazi kuwa magumu,” amesema.

Amesema Serikali ni vema Serikali ikahakikisha kabla ya msimu wa utalii kuanza, inaboresha pia miundo mbinu hasa ya barabara za ndani ya hifadhi, nyingi zimekuwa mbovu.

Naye mwekezaji wa utalii na muongoza watalii Wilbard Chambulo amesema waongoza watalii wengi hawajaenda shule kusomea taaluma hiyo bali wamejifunza kutoka kwa wengine, hivyo ameiomba serikali kuona namna ya kuingiza mtalaa huo katika vyuo vikuu nchini.

“Hakuna muongoza watalii amesomea hapa akapata shahada au hata stashahada popote, wengi wanafanya kutokana na uzoefu wa wengine waliowaiga na kitendo hicho kimewakosesha hata nafasi kubwa za kazi zenye uhitaji wa taaluma kwanza,” amesema.

Kutoka na hilo, ameiomba serikali iwatambue kisheria watutungiwe sheria, kanuni na taratibu kwa lengo la kuboresha utendaji kazi wao.

Akifungua kongamano hilo akimwakilisha Waziri wa Maliasili na Utalii, Mkurugenzi wa wanyamapori Tanzania,  Alex Lobora amesema waongoza watalii ni wadau muhimu katika sekta hiyo na wanawategemea katika kufanikisha malengo ya kuongeza idadi ya watalii na mapato zaidi.

“Lakini pia mjue sekta ya utalii ni nyeti, inahitaji watu wenye taaluma, weledi na maadili kutokana na nafasi yao ya kukutana moja kwa moja na watalii na kuwahudumia, hivyo tunategemea muwe wazalendo zaidi katika utekelezaji wa majukumu yenu,” amesema Lobora.

Amesema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya utendaji kazi wa waongoza watalii nchini na kutengeneza fursa za kiuchumi ili waweze kunufaika na sekta hiyo zaidi lakini pia kuongeza pato la Taifa kutoka Asilimia 17 iliyopo sasa hadi kufikia asilimia 20 miaka ijayo.

Kwa upande wake, Meneja wa NMB Kanda ya kaskazini, Baraka Ladislaus amesema taasisi yao imejipanga kuwasaidia wadau wote wa utalii kutatua changamoto za kifedha kwa ajili ya kusaidia biashara zao za kiutalii ikiwemo mikopo yenye riba nafuu.

Baraka amesema wadau wanaofanya kazi za kupokea na kuhudumia watalii wanakumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo ya uhaba wa fedha na kushindwa kutoa huduma bora.
Hivyo, amesema wamejipanga kuhakikisha wanawasaidia kukidhi mahitaji ya kifedha ya kila siku sambamba na kurahisisha miamala ya kibenki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *