Wanne Yanga waikosa Fountain Gate kesho

Yanga haitokuwa na wachezaji watano katika mechi yake ya Ligi Kuu dhidi ya Fountain Gate, kesho Jumatatu, Aprili 21 katika Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Babati, Manyara.

Wachezaji hao watakosekana kwa sababu ya majeraha waliyoyapata katika mechi zilizopita za mashindano tofauti.

Kocha wa Yanga, Miloud Hamdi amewataja wachezaji wanne watakaosekana kuwa ni Khalid Aucho, Kennedy Musonda, Pacome Zouzoua na Stephane Aziz Ki lakini licha ya kutomtaja Yao Attohoula, beki huyo atakosekana kwa vile naye ana majeraha.

“Ni kweli tuna baadhi ya wachezaji majeruhi kama Aucho, Pacome bado hajawa tayari, Musonda anahisi maumivu kidogo si makubwa lakini hatuwezi kumuhatarisha pamoja na Azizi Ki ana maumivu ya muda mrefu.

Nawaheshimu wachezaji wote. Mimi si kocha wa kulalamika kwamba sina huyu au yule hapana nitampa nafasi kila mchezaji. Hiyo ndiyo njia pekee ambayo itatuwezesha kufika mwezi Mei tukiwa imara, kwa sababu kila mchezaji atakuwa amepewa muda wa kucheza. Hilo ni jambo muhimu sana kwangu. Asanteni sana,” amesema Hamdi.

Akizungumzia mechi ya kesho, Hamdi amesema anaamini itakuwa ngumu lakini watajitahidi wapate ushindi.

“Lazima tuwe makini sana, tushinde kila mechi. Pia, tumefanya mikutano ya kiufundi, tumeangalia video na kufanya mazoezi ya kiufundi ili kujiandaa vizuri.

“Ninawaambia mara nyingi nyota wa mchezo ni mfumo. Wachezaji wote wakielewa mfumo, tutashinda mechi nyingi. Tuna wachezaji wenye uwezo wa kufanya mfumo ufanye kazi lakini jambo la kwanza ni kuelewa mfumo.

“Kwa hiyo mchezaji anapobadilishwa au kuingia uwanjani, lazima ajue moja kwa moja anachotakiwa kufanya na kile asichopaswa kufanya na kuelewa wa Wachezaji wangu naamini tutaendelea kufanya vizuri kwenye kila mchezo,” amesema Hamdi.

Mchezo wa mzunguko wa kwanza baina ya timu hizo ulimalizika kwa ushindi wa mabao 5-0 ambao Yanga iliupata.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *