
Dar es Salaam. Simba itawakosa wachezaji wake wanne kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya KMC utakaochezwa leo saa 10 jioni kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.
Kocha wa Simba, Fadlu Davids amethibitisha kuwa Joshua Mutale, Valentino Mashaka, Yusuph Kagoma pamoja na Abdulrazack Hamza ambae bado hajawa fiti licha ya kuanza mazoezi mepesi kuwa watakosekana katika mechi ya leo.
Kukosekana kwa Joshua Mutale ambaye mara nyingi huwa anaanza kwenye kikosi cha kwanza kutamfanya Fadlu Davids pengine kuanza na Kibu Denis au Awesu Awesu ambao huwa anawatumia kwenye nafasi hiyo.
Simba wanaingia kwenye mchezo huo ikiwa zimepita siku nne wakitokea Mkoani Kigoma walipokuwa na kibarua kigumu mbele ya Mashujaa ambapo walipata ushindi mwembamba wa bao 1-0 ambalo lilifungwa na mshambuliaji wao Steven Mukwala akitokea benchi kuchukua nafasi ya Leonel Ateba.
Kwa upande wa KMC wanaingia kwenye mchezo huu wakiwa na historia ya ushindi kwenye mechi yao ya mwisho ambapo waliupata dhidi ya Namungo wa bao 1-0 ambalo lilifungwa dakika za mwanzoni na Rashid Chambo kwenye uwanja wa KMC Complex.
Kocha wa KMC Abdihamid Moallin amesema: “Simba wanatimu nzuri, tutajaribu kupunguza makosa ili kuwanyima nafasi ya kufunga, tunataka kila mtu afrahie mchezo wakati malengo yetu yakiwa ni kupata ushindi”
Kwa upande wa kocha wa Simba Fadlu Davids amesema “KMC wana kikosi bora pamoja na kocha wao lakini tumejiandaa vizuri kuwakabili na kuondoka na alama zote tatu”
Simba na KMC zimekutana mara 12 kwenye michezo ya Ligi Kuu ambapo Simba wameshinda michezo 10 huku wakitoa sare mara mbili wakati KMC wao wakiwa hawajawahi kupata ushindi mbele ya wekundu wa msimbazi.