
Dar es Salaam. Mwaka mmoja baada ya kuundwa kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), makada watatu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wamefungua shauri kupinga sheria hiyo.
INEC imeanzishwa mwaka 2024 chini ya Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), namba 2 ya mwaka 2024.
Sheria hiyo iliyopitishwa na Bunge Februari 2, 2024, ikasainiwa na Rais Machi 7, 2024 na kuwa sheria rasmi imeleta marekebisho na au mabadiliko kadhaa kwa taasisi hiyo yenye dhamana ya kuratibu na kuendesha uchaguzi nchini.
Kesi hiyo ya kikatiba kupitia kwa mawakili wao walioandaa nyaraka za kesi hiyo, Mpale Mpoki na Hekima Mwasipu imefunguliwa Jumanne Aprili 29, 2025, Mahakama Kuu, Masjala Kuu, Dodoma na makada hao wa Chadema kutoka mikoa tofautitofauti, dhidi ya INEC na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Makada hao wa Chadema waliofungua kesi hiyo ni Moses Fanuel Omari kutoka jimbo la Singida Mashariki mkoani Singida; Amina Abrahamani Kanyama, kutoka Wilaya ya Bahi, mkoa wa Dodoma na Shija Samweli Shibeshi kutoka Wilaya ya Misungwi, Mkoa wa Mwanza.
Wadai hao ambao pia wanajitambulisha kama raia wa Tanzania waliosajiliwa kama wapigakura tangu mwaka 2010 wanadai wameshiriki katika uchaguzi unaoendeshwa au kusimamiwa na tume hiyo, katika majimbo yao.
Omari anadai uchaguzi mkuu wa 2015 aliteuliwa na Chadema kugombea udiwani wa Issuna huku Amina akidai aliteuliwa na Chadema kugombea ubunge wa Bahi katika uchaguzi mkuu wa 2020 lakini aliondolewa na mdaiwa wa kwanza (Tume) kugombea.
Shibeshi kwa upande wake anadai aliteuliwa na Chadema kugombea ubunge wa Misungwi katika uchaguzi mkuu wa 2020 lakini aliondolewa na Tume kugombea nafasi hiyo.
Wanadai sheria hiyo inakusudiwa kuwa chombo cha kuwapeleka kwenye uchaguzi mkuu ambao ni wa kuaminika, huru na wa haki, utakaoendeshwa kwa kuzingatia maadili ya kidemokrasia
Hata hivyo, wanadai masharti yanayopigiwa upatu katika sheria hiyo yanakiuka misingi ya demokrasia, uhuru wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na uwazi.
Wanadai masharti hayo yanawazuia kushiriki kikamilifu katika chaguzi ambazo ni huru, haki na za kuaminika ambazo zitawawezesha kuwachagua wawakilishi wao katika Bunge na madiwani, na kushiriki katika masuala mengine yanayohusu utawala wa nchi hii kwa kuonesha matakwa ya wapigakura.
Hivyo wanadai wamechukua hatua hizo za kisheria kufungua kesi kupinga katika kutekeleza wajibu wao wa kikatiba na kiraia kwani masharti hayo ambayo yanawahusu wao na umma kwa ujumla, yanakiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika kesi hiyo wanapinga vifungu namba 4, 5, 7, 8, 9, 10, 11, 13, 14, 17, 18, 19, 21, 25 na 27 vya Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 2 ya 2024 wakidai kuwa vinakiuka masharti ya ibara mbalimbali za Katiba ya nchi.
Wanabainisha ibara hizo kuwa ni Ibara ya 5(2)(a), (b), (c), (d) na (3)(a), (b), (c), (d), Ibara ya 13(2) na 13(6)(a), 21(1) na (2), 26(1) na 64(5).
Hivyo wanaiomba mahakama itamke vifungu hivyo vya sheria hiyo vinakiuka masharti ya ibara hizo walizoziainisha, na hivyo ni batili, havina nguvu kisheria na iamuru vifutwe kwenye kitabu cha sheria.
Pia wanaiomba mahakama hiyo iiamuru INEC ianzishe mara moja mchakato wa kurekebisha vifungu hivyo kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Msingi wa madai yao
Kwa mujibu wa hati yao ya madai na kiapo chao cha pamoja kinachounga mkono madai yao, wanadai sheria hiyo inapaswa kuzingatia masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 [Sura ya 2 Rejeo la 2002 bila kuikiuka.
Lakini wanadai baadhi ya vifungu vya sheria hiyo iliyochapishwa kwenye Gazeti la Serikali Machi 22, 2024 vinakiuka Katiba.
Wanadai ukiukwaji huo wa Katiba umesababisha kukiukwa kwa haki za msingi za kikatiba na haki za binadamu, ikiwamo ya kuchagua wawakilishi na kushiriki katika masuala ya umma kupitia wawakilishi waliochaguliwa katika Bunge na Mamlaka za serikali za mitaa.
Pia wanadai Bunge limepitiliza mamlaka yake kwa kutunga sheria nje ya mipaka iliyowekwa na Katiba hivyo kukiuka Ibara ya 5(2) na (3) ya Katiba.
Wanadai chini ya Ibara ya 64(5) ya Katiba, Bunge lina wajibu wa kutunga sheria zisizokiuka Katiba na chini ya Ibara ya 26(1) lina wajibu wa kuheshimu masharti ya Katiba.
Wakifafanua kasoro za vifungu hivyo wanadai kuwa kifungu cha 4 cha Sheria hiyo kinaunda Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.
Hata hivyo, wanadai hakitoi uhuru halisi kwa kuwa wajumbe wake wote saba wanateuliwa na wanaapishwa na Rais, na wanapendekezwa na watu walioteuliwa na Rais ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama tawala kinachoshiriki uchaguzi.
Wanadai kuwa tume hiyo ni tofauti na iliyotajwa kwenye Katiba na kwamba hivyo kinakiuka Ibara ya 5(2)(3), 13(2), 13(6)(a), 21(1)(2), 26(1) na 64(4) ya Katiba.
Kifungu cha 5 kuhusu muundo wa tume na jinsi Rais anavyoteua wajumbe na kamati ya uteuzi wanadai hakina mipaka ya idadi ya majina na hakuna masharti ya idhini ya Bunge.
Kifungu cha 7 kuhusu sifa za wajumbe wa tume hakizingatii hali ya kisiasa hivyo kuhatarisha uhuru wa tume kinyume na Katiba.
Kifungu cha 8 kuhusu muda wa wajumbe wanadai kinampa Rais mamlaka makubwa ya kuwaadhibu wajumbe, kuunda kamati ya ushauri kwa hiari na kuruhusu kuteuliwa tena bila kikomo.
Kifungu cha 9 kuhusu kamati ya uteuzi, wanadai kuwa Kamati hiyo na Katibu wake inateuliwa na inaapishwa mbele ya Rais, jambo ambalo wanadai linahatarisha uhuru wa tume na kukiuka Katiba.
Kifungu cha 10 kuhusu majukumu ya tume, wanadai kuwa kinaipa tume hiyo mamlaka kupita kiasi mfano 10(1)(l) na 10(2), na kuzuilia vyama visishiriki uchaguzi kwa kutosaini maadili ya uchaguzi.
Kifungu cha 11 kinawafanya wajumbe wa tume kufuata sheria za utumishi wa umma ambapo mkuu wa utumishi wa umma ni Rais ambaye pia ni mwenyekiti wa chama kinachoshiriki uchaguzi.
Kifungu cha 21 kinahusu bajeti ya tume kutoka bajeti ya serikali jambo wanalodai kuwa utegemezi wa bajeti ya Serikali unadhoofisha uhuru na mamlaka ya Tume.
Kifungu cha 25 kinataka tume kuomba ushauri kwa Waziri wa Utumishi wa Umma kuhusu ajira ya watumishi, hivyo wanadai kuhatarisha uhuru wa tume na kukiuka Katiba.
Kifungu cha 27 kinahusu kuendelea kwa majukumu ya wajumbe walioteuliwa chini ya sheria iliyofutwa jambo lisilo na maana.
Pia wanadai kuwa vifungu hivyo vinakiuka ibara za mikataba na matamko mbalimbali ya kimataifa ambayo Tanzania pia imeiridhia.
Mikataba na matamko hayo ni Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu (1981)Ibara ya 13(1), Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa (1966) Ibara ya 25(a) na (b) na Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu (1948) Ibara ya 21(1) na (3).
Wanadai Bunge halikuwa na mamlaka kutunga sheria yenye masharti hayo yakiwemo kibadili jina la Tume hiyo tofauti na inavyosomeka katika Katiba.
Wanadai pia sheria hiyo imeiondolea Tume kinga ya kutokushtakiwa kwa utekelezaji wa majukumu yake kinyume na Katiba.
Wanabainisha haki zinazotolewa na Ibara hizo Katiba ambazo zinakiukwa na Sheria hiyo kuwa ni haki ya wananchi kupiga kura na kushiriki katika masuala ya umma na haki ya kusikilizwa kwa haki.
Pia wanadai kuwa inakwaza misingi ya demokrasia na uchaguzi wa ushindani, kupunguza uwajibikaji wa vyama vya siasa na wagombea wao kwa wananchi.
Vilevile wanadai vinatoa upendeleo kwa chama kimoja kwa kuwa wajumbe wa tume wanaoteuliwa na mshiriki wa uchaguzi.