Wanawake, vijana watakiwa kujitosa uchaguzi mkuu

Dar es Salaam. Wakati vyama vya siasa vikiendelea na maandalizi ya uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na urais utakaofanyika Oktoba 2025, baadhi ya wadau wa haki za binadamu wamewahamasisha vijana na wanawake kujitokeza kushiriki uchaguzi huo.

Lengo ni kuhakikisha kundi hilo linaingia kwa wingi katika vyombo vya uamuzi.

Utafiti uliofanywa na Shirika la Mazingira na Haki za Binadamu na Jinsia (Envirocare), umeonesha baadhi ya changamoto za kiuchaguzi kwa kundi hilo, mila potofu na rushwa ya ngono ni miongoni mwa sababu zinazochangia wengi kutojitokeza.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na shirika hilo kwa takribani miaka mitatu walibaini idadi ya wanawake na vijana katika uongozi ni ndogo ikilinganishwa na wazee.

Utafiti huo uliofanyika katika wilaya za Kinondoni, Kigamboni na Ubungo kwa miezi 18, ulibaini ushirikishwaji wa wanawake na vijana katika ngazi zote za uongozi ni mdogo kutokana na baadhi ya vikwazo wanavyokumbana navyo katika kugombea nafasi hizo.

Hayo yamesemwa na Msimamizi Mradi wa Shirika la Mazingira na Haki za Binadamu na Jinsia (envirocare), Godlisten Muro katika semina ya siku mbili kwa waandishi wa habari iliyoanza Jumanne Machi 4-5, 2025 ikiwa na lengo la kutoa kwa waandishi ili kuhamisha wanawake na vijana kujitokeza kushiriki katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.

“Katika wilaya tajwa, tulifanya utafiti kwa kuwashirikisha vijana kutoka kwenye vyama vya siasa na dini mbalimbali wenye nia dhabiti na sifa za kugombea nafasi hizo kwa mujibu wa sheria za nchi,” amesema.

Amesema utafiti huo ulihusisha njia ya moja kwa moja kwa kuwafikia jumla ya watu 500, wanawake wakiwa ni 400 na vijana 100.

“Kwa njia za mitandao tuliweza kuwafikia watu 10,000 kutoka sehemu mbalimbali nchini,” amesema.

Muro amesema katika kuendeleza kampeni ya kuhamasisha wanawake na vijana viongozi kuanzia mwishoni mwa mwaka jana mpaka sasa wanatarajia kuwafikia watu 300 katika wilaya za Ubungo na Kinondoni pekee.

“Tunatarajia kuwafikia watu 300 kwa njia za moja kwa moja na wanawake watakuwa 150 na vijana 150 huku kwenye mitandao ya kijamii tukitarajia kuwafikia watu 1,300 wa wilaya hizo na mpaka kufikia 2026 mradi huu utakuwa umewafikia wanawake na vijana wengi zaidi na kuwapa uthubutu katika uongozi,” amesema.

Muro amesema hali ya kiuchumi ya vijana na wanawake ni ngumu ukilinganisha na wazee ambao ni wastaafu, ambao wanafedha za kuendesha kampeni za nafasi hizo.

Amesema kupitia elimu wanayoitoa wanatarajia kuona ongezeko la wanawake na vijana katika nafasi hizo.

“Utafiti wetu unaonyesha bado jamii haina uelewa wa kutosha, wengi huamini ili uwe na busara ya uongozi lazima uwe na mvi kitu ambacho si sahihi,” amesema.

Wakichangia kwenye wasilisho hilo la utafiti, mmoja wa washiriki Tedy Nkonyoka amesema tangu kuanza kwa semina hiyo amejifunza faida ya ushiriki sahihi wa wanawake na vijana katika uongozi.

Amesema kupitia semina hiyo, anaamini kutakuwa na mabadiliko mpaka kufikia Oktoba 2025.

Naye Lugendo Madege amesema kama mwandishi wa habari, semina hiyo imempa somo la namna bora ya kuripoti taarifa zilizojificha katika jamiii.